Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Alama sita usalama kwa walemavu barabarani, maana na umuhimu

B2c8f8ec645448cea6f16c4a5bd299ce.jpeg Alama sita usalama kwa walemavu barabarani, maana na umuhimu

Thu, 23 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

“NIKIWA ninaendesha gari, ikaniharibikia na sasa ninaita watu wanisaidie, lakini wanaona mimi siteremki, wanaona mimi ninawadharau na kutaka kuwatumikisha ndiyo maana ninaomba msaada, lakini nimeng’ang’ania kukaa ndani ya gari; labda kukwepa mvua, jua au vumbi; hawajui hali niliyo nayo hivyo ni rahisi sana wengi kukataa.”

“Au basi chukulia mfano, kama mtu mwenye ulemavu wa viungo anavuka barabara akiwa anatambaa urefu wa kimo chake haufiki mita moja. Kwa hiyo, kama tunavuka barabara sambamba na mbuzi, dereva akiwa mita 100 anakuja, atamuona mbuzi kabla yangu na ikibidi kupiga honi, mbuzi atakimbia na kutoka, lakini mimi sitaweza.”

Ndivyo anavyosema Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Usalama Barabarani kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania (NCPDRS), Jutoram Kabatele anapozungumza na wanahabari ofisini kwake Gongolamboto, Dar es Salaam kuhusu kampeni ya kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za watu wenye ulemavu barabarani na alama sita maalumu za usalama barabarani kwa watu wenye ulemavu na umuhimu wake.

Katika mazungumzo hayo akiwa pamoja na Katibu Mkuu wa NCPDRS, Dk Hamis Nassoro Cheni na Mhasibu, Ally Tembele, Kabatele anasema, mafunzo hayo wanayotarajia kuyatoa katika mikoa ya Tanga na Mtwara mwezi Agosti 15 hadi Oktoba, mwaka huu.

“Tunalenga kuwafikia takriban watu 4,000 kupitia mafunzo haya yanayofadhiliwa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Foundation for Civil Society (FCS) na tunawashukuru sana kwa ufadhili wao,” anasema Kabatele ambaye pia ni mbunifu na mvumbuzi wa alama sita kuu maalumu za usalama barabarani kwa watu wenye ulemavu Tanzania zinazotumika sasa hata na mataifa mengine.

Anafafanua: “Tunawashukuru (FCS) maana hata mwaka jana walifadhili mafunzo kama haya na tukawafikia watu wengi katika mikusanyiko mbalimbali mikubwa na katika madarasa maalumu maana tuliwalenga na kuwafikia watu wenye ulemavu, madereva na jamii nyngine kwa jumla.”

Anasema kupitia ufadhili huo wa Foundation for Civil Society, Kamati hiyo mwaka jana iliwafikia walengwa 2,000 mkoani Dar es Salaam na Dodoma wakafikiwa walengwa 2,800 huku Zanzibar wakafikiwa walengwa wapatao 1500.

UMUHIMU WA MAFUNZO NA ALAMA HIZO

Mintarafu sababu za kuendelea kutoa mafunzo hayo Kabatele, Cheni na Tembele wanasema kwa nafasi tofauti kuwa, ingawa alama hizo zipo na zimeanza kutumika, ni watu wachache wanaozijua na kuzizingatia.

“Kwa kuwa watu ni wengi, magari na vyombo vingine vya usafiri barabarani ni vingi na barabara nyingine zinaboreshwa, huku watu wengi wakiwa hawazijui alama hizi, matokeo yake ni ajali nyingi zinazowahusisha watu wenye ulemavu kutokea,” anasema Kabatele.

Kitabu: “Je, Unazijua Alama Mpya 6 Maalumu za Usalama Barabarani kwa Watu Wenye Ulemavu?” kilichotolewa na NCPDRS kwa ufadhili wa FCS Agosti 2019, kinafahamisha katika Uk. 7 kuwa, katika kipindi cha mwaka 2004 hadi 2018, kumeripotiwa ajali 200 zinazohusishwa na watu wenye ulemevu.

Kinasema hiyo inatokana na watu hao wengi kutokujua sheria za usalama barabarani, gari la mwenye ulemavu kutokuwa na bima, gari au pikipiki kukosa alama inayoonesha kuwa ni la mlemavu na mtu mwenye ulemavu kutokufundishwa chombo anachokiendesha. “… mazingira haya yanaridhia hata inapotokea mtu mwenye ulemavu amegongwa japo si kwa makosa yake, inashindikana kulipwa bima kwani sheria haimpi uhalali wa malipo juu ya chombo chake kilichoharibika kwa kuwa hana leseni ya udereva na pia kifaa chake hakina bima itakayomwezesha kulipwa fidia. Hii ni hatari sana kwa maisha ya mwenye ulemavu,” kinasema na kuongeza: “Ikitokea hivyo, basi hutokea kama msada tu kulipwa fidia.”

Kamati hiyo NCPDRS inapendekeza vyombo vya moto kama magari na pikipiki za magurudumu matatu maarufu bajaj zitumiwazo na wenye ulemavu, zisajiliwe kwa namba maalumu zinazoanza na herufi “WT” yaani ‘Walemavu Tanzania’ ili kuonesha ni mali ya mtu mwenye ulemavu.

“Hii itasaidia pia kumfanya atakayonunua chombo hicho kutoka kwa mwenye ulemavu awajibike kulipa kodi na ushuru wa serikali anaostahili ambao ulisamehewa. Kwa kawaida vyombo vyote vya wenye ulemavu husamehewa kulipa kodi na ushuru wa serikali,” anasema Kabatele.

Anaongeza: “Hii itaepusha kutumia vibaya misamaha ya kodi ya magari na pikipiki zitumiwazo na walemavu pindi wanapohitaji kuuza kwani huenda baadhi ya watu hupenda kununua vyombo hivyo ili pengine wakatumie kimakosa msamaha huo wakati mnunuzi hahusiki na msamaha huo.”

MAKUNDI YA WENYE ULEMAVU, ALAMA NA MAANA

Watu wenye Ulemavu wa Viungo Mlemavu wa viungo ni mtu aliyepungukiwa uwezo wa baadhi ya viungo vyake kufanya kazi. Kabatele anasema: “Alama ya mlemavu wa viungo huonesha mtu mwenye ulemavu aliye katika kiti cha magurudumu maarufu ‘wheel chair.’ Watu wenye Ulemavu wa Macho (wasioona) Alama ya mtu mwenye ulemavu wa macho asiyeona ni fimbo maalumu nyeupe ya wasioona.

Fimbo hii hutumiwa na mlemavu wa macho kumuongoza njia. Anasema: “Asiyeona anapotembeza fimbo hiyo chini, ina maana anatembea tu, lakini anapoinyosha kwa mbele, maana yake anataka kuvuka…” Watu wenye Ulemavu wa Ngozi (Albino) Alama ya mlemavu wa ngozi isiyostahimili mwanga wa jua.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa, albino hutumia mwavuli au kofia aina kama ungo ili kujikinga na mwanga wa jua. Hivyo, mwavuli ni alama kuu ya albino. Albino pia huvaa shati la mikono mirefu na miwani ya kiza wakati wa mchana ili kupunguza madhara ya mwanga kwao.

Kwa mujibu wa Kabatele na Dk Cheni, albino ana ulemavu wa aina mbili. Kabatele anasema: “Kwanza ana huo ulemavu wa ngozi na pia, anao mwingine wa uoni hafifu hivyo, hawezi kuona kitu cha mbali na hiyo, mita 100 kwa albino ni hatarishi kwa dereva; lazima kuwa na alama kumtambulisha uwepo wake.”

Watu wenye Ulemavu wa Masikio (Viziwi) Alama kuu ni sikio kwa kuwa kiziwi maana yake ni uharibifu / maradhi kuharibu ngoma ya sikio, kuongea hivyo alama kuu ya kiziwi ni sikio. “Bubu na viziwi wengi wamegongwa kwa kuwa hata dereva akipiga honi, hawasikii na badala yake, wengine wanaishia kutukanwa tu…” anasema.

Watu wenye Ulemavu wa Akili Kwa mujibu wa Kamati ya Usalama Barabarani kwa Watu Wenye Ulemavu Tanzania, mtu mwenye ulemavu wa akili ni yule aliyekosa utimilifu wa akili ama iwe kwa maradhi, au kwa ajali; huitwa ulemavu wa akili.

“Alama yake ni mfano wa kichwa cha binadamu kilichochorwa na kukatiza mstari kati ya uso na kisogo, hiyo ni alama kuu ya mtu mwenye ulemavu wa akili,” anasema mwenyekiti huyo wa NCPDRS.

Stika maalumu ya utambulisho wa dereva mwenye ulemavu Uchunguzi wa maandishi wa makala haya umebaini kuwa, hii ni stika maalumu inayotambulisha kuwa, dereva wa chombo hicho ni mwenye ulemavu hivyo, kuongeza tahadhari kwa sababu wengi harakati zote za udereva huzifanya kwa mikono, ikiwa ni pamoja na kushika usukani, kuongeza mwendo na kushika breki.

Viongozi wa NCPDRS wanasema mafunzo mintarafu alama hizo ni muhimu kwa jamii ili kuimarisha hali ya usalama barabarani kwa watu wenye ulemavu kwa kuwa nao wana haki ya matumizi salama ya barabara kwani hutumia barabara kuendesha maisha yao ama kwa walioajiriwa au waliojiajiri wenyewe katika kazi au biashara mbalimbali. Viongozi hao wanasema mtu mwenye ulemavu akizijua vema sheria na alama za usalama barabarani, atakuwa dereva bora atakayelinda usalama wake barabarani na wa watu wengine.

Columnist: habarileo.co.tz