Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Aina 3,000 za wanyama, mimea ziko hatarini kutoweka

Mimea Wanyama.png Aina 3,000 za wanyama, mimea ziko hatarini kutoweka

Thu, 30 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati utafiti ukionyesha aina 3,000 za mimea na wanyamapori wakiwa hatarini kutoweka miongoni mwa aina milioni 10, hifadhi ya Taifa ya Ruaha imetoa mafunzo kwa majaji wa Mahakama Kuu, mahakimu wa ngazi mbalimbali, waendesha mashtaka na wapelelezi ya namna bora ya kuendesha kesi za wanyamapori.

Kulingana na wataalamu wa hifadhi ya Taifa ya Ruaha, uharibifu wa mazingira ni miongoni mwa mambo yanayowaweka rehani wanyamapori na mimea hiyo.

Akifungua mafunzo hayo, Jaji Mfawidhi Mahakama kuu Kanda ya Iringa, Ilvin Mugeta amezitaka sekta za uhifadhi kuhakikisha kuwa wanalinda wanyama na viumbe hai vya misitu dhidi ya ujangili kwa kuzingatia sheria.

Akizungumza katika mafunzo hayo yanayoendelea katika Ukumbi wa Royal Palm Mkoani Iringa, Jaji Mugeta amesema ni kweli kwamba utafiti unaonyesha kuwa miongoni mwa aina 10 milioni za wanyama na mimea, aina 3,000 zipo katika hatari ya kupotea.

"Idadi hiyo ya mimea na wanyama walio katika hatari ya kupotea zinatupa ujumbe kwamba, kama hatua hazitachukuliwa viumbe hivyo vitapotea na wasio katika hatari ya kupotea watapotea," amesema Jaji Mugeta.

Amesema jukumu la kulinda wanyama na viumbe hai ni jukumu kubwa na linahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali ikiwamo wa sekta ya uhifadhi.

Naye mhadhiri msaidizi chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto, Roggers Cletus amesema suala la uhai wa wanyama pori ni jukumu la kila mmoja.

“Hili linahitaji watu wenye uzoefu na mafunzo ya kina ili kuhakikisha wanyama wanakuwa salama pia mfumo wa haki jinai umekuja kuzuia na kusimamia uhai wa wanyama pori.

"Shughuli za kibinadamu kama uwindaji haramu, usafirishaji haramu wa wanyamapori unatishia uwepo wa wanyama hawa hivyo utunzaji wa wanyamapori unahitaji watu wenye weledi na waliopata mafunzo kwa kina ili kuhakikisha wanyama wanalindwa," amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Pams Foundation, Samson Kassala amesema mafunzo hayo yatawaongezea washiriki uwezo wa kazi zao kwa ufanisi zaidi.

"Makosa ambayo yalikuwa hayapo Tanzania hususani yahusuyo maliasili sasa hivi tunayaona yapo, sababu ya mabadiliko na hata mbinu za kuyakabili pia zinabadilika, kwa hiyo haya mafunzo yatawaongezea washiriki uwezo zaidi wa kufanya kazi zao kwa ufanisi,” amesema.

Columnist: www.tanzaniaweb.live