Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Afadhali Koulibaly hajawa mnafiki, amesema kweli

Kalidou Koulibaly Money Kalidou Kulibaly

Sun, 2 Jul 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Unaweza kutoka Ulaya na kwenda kuibusu jezi ya Al-Nassr? Unaweza kutoka Real Madrid na kwenda kuibusu nembo ya Al-Ittihad? Unaweza kutoka Chelsea na kwenda kuibusu jezi ya Al-Hilal? Sio kweli. Afadhali Kalidou Koulibaly amesema kweli.

“Siwezi kukataa. Kwa pesa hizi ninazoenda kupata nitaweza kusababisha familia yangu yote iishi vizuri, kuanzia kwa wazazi wangu hadi ndugu zangu wengine. Itasababisha pia niwezekeze vema katika mfuko wangu wa hisani kule Senegal. Tulianza kujenga kliniki katika kijiji ambacho wazazi wangu wanatoka Senegal”

Haya aliyasema Koulibaly mbele ya waandishi wa habari. Hakutaka kuficha kitu. Rafiki zetu wengi wamekwenda Saudi Arabia kimya kimya. Wengi wamekwenda kwa aibu zaidi. Hawataki kusema kweli. Koulibaly amesema kwa niaba yao.

Kinachoendelea kwa sasa ni mtihani mkubwa kwa mastaa wa soka. Hatujui zoezi hili litaendelea mpaka lini. Kwa sasa linawasomba wanasoka wengi ambao umri wao umesogea. Inaonekana kama ni kitu cha kawaida kwa sababu umri umekwenda.

Huyu Koulibaly mwenyewe ana miaka 32. Inaonekana kama vile ni halali kwake kwenda Saudia. Cristiano Ronaldo inaonekana kama vile halali kwenda Saudia. Karim Benzema vile vile. Hata Riyad Mahrez inaonekana ni sawa tu.

Lakini vipi kama operesheni ya Waarabu ikihamia kwa akina Bukayo Saka, Marcus Rashford, Vinicius Junior na wachezaji wengine wenye umri mdogo? Hawa wakubwa tu wanashindwa kujitokeza hadharani kama Koulibaly na kutuambia ukweli kwamba wanafuata pesa. Vipi akina Saka watatuambia nini?

Kwamba unakwenda Saudi Arabia kwa sababu unaipenda sana Al Hilal? Chukua mfano wa Koulibaly mwenyewe. Hata kama Chelsea amesuasua kwa msimu wake wa kwanza angeweza kufanya mambo mawili. Kwanza kabisa kugombania namba yake.

Lakini kama angeamua kuondoka basi Koulibaly angeweza kuwa lulu kwa klabu nyingi ambazo zina matatizo katika eneo la ulinzi wa kati. Ni afadhali uwe na Koulibaly kuliko Harry Maguire. Ni afadhali uwe na Koulibaly kuliko Rob Holding.

Hata hivyo Koulibaly aliamua kufuata zake pesa Uarabuni. Kitu kizuri ni kwamba hajaficha. Vipi kwa wengine? Sijasikiliza mahojiano yao pindi wanapowasili Riyadh lakini ukweli ni kwamba simuoni mchezaji wa kukaa mbele ya waandishi wa habari na kusema “Ilikuwa ni ndoto yangu ya muda mrefu kuja kucheza Saudia Arabia”

Sioni mchezaji ambaye atasimama mbele ya waandishi wa habari na kudai “Imekuwa ndoto yangu ya muda mrefu kuja kucheza katika klabu ya Al Hilal”. Mchezaji wa namna hii, halafu sio mzaliwa wa Saudia Arabia tunaweza kumrushia mawe.

Naweza kukubali mastaa wanaosema imekuwa ndoto yao kumalizia soka Marekani. Kisa? Wakati mwingine wanaipenda zaidi nchi yenyewe kuliko Ligi yao ya MLS. Ndiyo, kuna wachezaji wanataka kuzurura katika fukwe za Miami au mitaa ya New York. Hawa wapo wengi. Wanavutiwa na bata la Marekani.

Lakini haitashangaza sana mchezaji akienda Marekani. Pele alikwenda mwaka 1975. Baadaye wakaenda wengi. Akina Ricardo Kaka, David Beckham, Frank Lampard, Steven Gerrard na wengineo wengi.

Haishangazi Lionel Messi kwenda. Lakini ni wachezaji gani wa hadhi hii wamewahi kwenda Saudi Arabia? Leo Saka atajiteteaje kwa kwenda Saudia Arabia? Kwamba ndoto zake zilikuwa kucheza Riyadh? Akienda Barcelona au Real Madrid tunaweza kumuelewa. Akienda Juventus au AC Milan tunaweza kumuelewa. Akienda Al Hilal hatuwezi kumuelewa.

Kinachonifurahisha ni ukweli kwamba hata Waarabu wenyewe wanatambua hili na ndio maana wametumia njia ya mkato ya kulipa mshahara mkubwa mara tatu ya ule ambao ulikuwa unalipwa Ulaya. Ni njia rahisi ya kuwakamata wachezaji hawa.

Hii ni fidia maradufu kwa baadhi ya wachezaji. Kwa mfano, kwa kwenda Saudi Arabia kuna wachezaji wengi ambao wanapoteza mambo mengi ya nje ya uwanja. Wale rafiki zangu wapenda pombe na wapenda wanawake wanabanwa na sheria kali za Kiislamu za nchi hii ambayo inafuata kwa karibu sheria hizi.

Cristiano Ronaldo alipewa ruhusa maalumu ya kuishi na mwanamke ambaye hajamuoa Georgina. Sijui kama itakuwa hivyo kwa akina Riyad Mahrez na wengineo ambao nao wanaishi na wachumba zao. Sijui itakuwa vipi pia kwa mastaa ambao wanapenda pombe.

Yote haya inabidi uyasahau ukikumbuka kiasi cha mshahara ambao unapewa. Kinachofanyika mpaka sasa ni biashara ya nipe nikupe. Waarabu wanatoa pesa nyingi kwa ajili ya kufurahisha nafsi zao. kwa ajili ya kuwaona wachezaji hawa katika sebule zao.

Alipochukuliwa Ronaldo tulikuwa tunaamini kwamba ilikuwa pia ni kwa ajili ya kuwafanyia promosheni ili waweze kuandaa kombe la dunia mwaka2030. Lakini kwa sasa inaonekana kuna kitu zaidi ya hiki. Mbona Qatar hawakulazimika kuchukua mastaa kama hawa kwa ajili ya kuandaa kombe la dunia?

Inachoonekana ni kwamba Waarabu wanataka kufurahisha macho yao katika viwanja vyao. Pesa wanazo na hawajui namna ya kuzitumia. Wamenunua timu kubwa za Ulaya na sasa wameamua kununua mastaa ambao umri umesogea na kuwapeleka kwao.

Vyovyote ilivyo klabu zao haziwezi kuwa kama Barcelona, Manchester United, Manchester City, Arsenal, Real Madrid na nyinginezo kubwa za Ulaya. Hizi ndizo klabu ambazo mchezaji anaweza kufika kisha akabusu jezi. Hauwezi kubusu jezi ya Al Hilal.

Wachina walijaribu kufanya hivi lakini mwishowe walishindwa. Tunataka kuona kama Waarabu watafanikiwa pale watakapoanza kwenda kwa wachezaji wenye umri mdogo kama akina Saka. Wakifikia huko bado hawataweza kuzifikia timu za Ulaya lakini kwa kiasi kikubwa watazivuruga klabu kubwa.

Columnist: Mwanaspoti