Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Adios amigo Eden ‘the baller’ Hazard

Eden Byeee hazard

Sat, 14 Oct 2023 Chanzo: Mwanaspoti

“...kidogo kidogo ni muda wa kufurahia maisha na ndugu na marafiki. Kunywa bia kadhaa..” Anasema Eden Hazard katika taarifa yake ya kustaafu soka mapema wiki hii. Ndiyo! Mambo hufika mwisho. Eden Hazard amefika mwisho. Mwisho ambao utaamua mwenyewe kwamba ulikuwa wa kikatili au vinginevyo.

Watu wengine wanaweza kudhani ilikuwa taarifa ya kawaida kabisa. Sio kweli. Katika dunia ya kileo inaweza kuwa taarifa ya kawaida kwa sababu maisha yanakwenda kasi hasa katika mitandao ya kijamii. Lakini taarifa ya Hazard kujiuzulu inapaswa kupokewa kama tukio linaloshtua - tukio ambalo unaweza kuliweka katika ukatili au kulifanya la kustaajabisha.

Nashindwa kuamua. Kiasi ni ukatili kiasi sio kweli. Ukatili kwa sababu Hazard anaondoka katika mpira akiwa na umri wa miaka 32 tu. Kumbuka Cristiano Ronaldo ana miaka 38. Lionel Messi ana miaka 36. Jonny Evans ana miaka 35. Kuna wachezaji wengi ambao Hazard anawaacha uwanjani wakiwa wamemzidi umri.

Lakini wenzake huwa hawastaafii Real Madrid. Wanastaafia Marekani au Saudi Arabia ama katika ligi ndogo za nchi zao kama Ubelgiji, Ureno, Serbia na kwingineko. Lakini Hazard amestaafu baada ya kuchanwa kwa mkataba wake pale Santiago Bernabeu. Majeraha yamechangia kwa kiasi kikubwa. Hakufikiria hata kwenda Saudia.

Upande mwingine sio ukatili kwa Eden kustaafu soka. Kwani tunamdai nini hasa? Hakuna. Kama Mungu alimpa kipaji kikubwa basi hakikuishia kwao La Louviere pale Ubelgiji ambako alizaliwa mwaka 1991. Eden alikileta kipaji chake duniani tukakiona na tukakiabudu. Alikuwa zawadi kwetu.

Kuna mchezaji anajua kukokota mpira kama Hazard? Wapo wachache mno. Labda kina Lionel Messi. Pale England, Hazard alikuwa anacheza katika dunia yake. Mmoja kati ya wachezaji ambao mashabiki wa timu nyingine kama Liverpool, Manchester United na Arsenal walikubaliana kwamba ndiye aliyekuwa mchezaji hatari katika Ligi Kuu England nje ya timu zao.

Ni kama ambavyo kwa sasa wanakubaliana kwa pamoja kwamba Mbelgiji mwenzake, Kevin De Bruyne ndiye mchezaji bora zaidi nje ya timu zao. Vitu vingine huwa vinafunga mjadala. Kipaji cha Hazard kilifunga mjadala. Hakuna ambaye alikuwa anaona upungufu wa Hazard uwanjani. Ulikuwa wapi? Hakuna.

Hazard anajua kukokota mpira kwa ufasaha. Anajua kupiga pasi za mwisho. Anajua kufunga. Anacheza kitimu halafu anacheza kibinafsi. Ana uwezo wa kuamua mechi moja ya soka peke yake. Moja kati ya vipaji bora vya soka ambavyo uso wa dunia umewahi kushuhudia.

Wakati mwingine namba hatuzipendi lakini pia hazidanganyi. Hazard ungeweza kumpenda kwa namna ulivyomuona, lakini pia kile ulichokiona kilikwenda sambamba na namba zake. Pale Chelsea katika mechi 352 alifunga mabao 110 na akapiga pasi za mabao 92. Kumbuka huyu ni winga lakini ameingia katika rekodi za wachezaji wachache England waliofunga mabao zaidi ya mia.

Tatizo la Hazard lilikuja pale alipojaribu kuamka kutoka katika ndoto tamu aliyokuwa anaiota Chelsea. Bora angeendelea kulala. Tatizo lilikuja pale alipoamua kukatisha boda na kwenda Hispania. Ni kweli wakati ulikuwa umefika na alikuwa na sababu nyingi za kuhama Chelsea kuliko kubakia. Alikuwa katika kilele cha ubora wake na alikuwa amefanya mambo makubwa Stamford Bridge.

Katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2019 wakati Cristiano Ronaldo akiaga Santiago Bernabeu kwenda Italia, yeye akaamua kubeba mizigo yake kutoka London mpaka Madrid kwa ajili ya kujaribu kuziba pengo la Ronaldo. Haikutafsiriwa hivi moja kwa moja kwa sababu Ronaldo ni mkubwa lakini walau Hazard tuliyemuona Chelsea angeweza kuleta kitu kikubwa tofauti pale Madrid. Haikuwezekana.

Huwa inatokea. Nuksi zinaweza kumuandama mchezaji akijaribu kubadili upepo. Unatamani angeendelea kuwa hapohapo labda nuksi hizo zisingemuandama. Kwanza Hazard aliandamwa na uzito halafu baadaye akaandamwa na majeraha ya mara kwa mara.

Hazard aliifungia Madrid mabao saba tu kuanzia mwaka huo mpaka leo. Uliwahi kufikiria hilo? Lakini ndivyo inavyokuwa kwa baadhi ya wachezaji. Kuhama kutoka katika ufalme na kujaribu kuhamishia ufalme huo kwingineko huwa kunawaletea nuksi. Kumbuka simulizi za akina Phillipe Coutinho, Fernando Torres, Alex is Sanchez na wengineo. Ilikuwa hivi hivi tu.

Na sasa Hazard ameamua kupumzika zake. Mambo ufika mwisho. Hakuna ambacho tunaweza kusema tunamdai. Kama mchezaji alituonyesha vitu vingi binafsi lakini kama mwanatimu pia ametwaa mataji mengi ya kutosha kuanzia England mpaka Madrid ambako alikwenda kutwaa taji la Ulaya hata kama alikuwa anachechemea.

Hakuna tunachomdai hasa ukizingatia kwamba katika kikosi cha timu yake ya taifa alibarikiwa kuwa katika kizazi cha dhahabu cha Ubelgiji ambacho hakikuweza kufanya maajabu yoyote ya soka. Iwe katika kombe la dunia mpaka katika michuano ya Euro.

Anaungana na akina De Bruyne, Jan Vertonghen, Vincent Kompany, Romelu Lukaku na wengineo lukuki ambao wamekiruhusu kizazi hiki kitokomee bila ya kushinda chochote. Anahusika katika lawama kama wengine wanavyohusika katika lawama. Hata hivyo asingeweza kushinda kitu peke yake.

Nini kinafuata kwake? Hatujui. Kwa sasa tumuache kwanza anywe bia zake huku akipeleka watoto shule pale Madrid ambako amelowea kwa sasa. Kama akiamua kurudi uwanjani basi anaweza kuwa kocha kama rafiki yake Kompany. Siku hizi wachezaji wengi mahiri wanaamua kuingia katika kazi ya ukocha na wanajaribu kuwa makocha wa kisasa. Hazard anaweza kuwa mmoja wao.

Lakini kwa sasa tunamuaga mmoja kati ya vipaji bora na vya kisasa kuwahi kutokea katika soka ndani ya miaka 15 iliyopita. Eden Hazard. Bonge la mchezaji. Miguu yake na ubongo wake vilifanya kazi kwa haraka sana. Vikaleta mateso makubwa kwa wachezaji wa timu pinzani. Wachezaji wa aina yake waingereza huwa wanawaita ballers. Kwaheri Hazard. Kanywe bia.

Waswahili wangesema ‘kwaheri’. Waingereza wangesema ‘Good bye’. Walatini wangesema ‘adios Amigo’. Naam, kwa sababu Hazard amestaafia Hispania sio mbaya kama tukisema ‘Adios Amigo’. Apumzike vizuri na anywe bia zake kwa amani Eden.

“...KIDOGO kidogo ni muda wa kufurahia maisha na ndugu na marafiki. Kunywa bia kadhaa..” Anasema Eden Hazard katika taarifa yake ya kustaafu soka mapema wiki hii. Ndiyo! Mambo hufika mwisho. Eden Hazard amefika mwisho. Mwisho ambao utaamua mwenyewe kwamba ulikuwa wa kikatili au vinginevyo.

Columnist: Mwanaspoti