Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

Adhabu zimepungua, vichekesho havikosi

Karia, TFF President Rais wa TFF, Walace Karia

Wed, 12 Oct 2022 Chanzo: Mwanaspoti

Wiki iliyopita tulishuhudia adhabu kwa wadau na klabu za soka baada ya kufanya makosa ambayo yalistahili kufanyiwa maamuzi.

Wamo waamuzi ambao walishindwa kutafsiri vizuri sheria za soka, yupo msemaji aliyefanya kosa la kutuhumu waamuzi kuwa waliingia matokeo ya baadhi ya mechi na zipo klabu ambazo zilihalalishiwa makosa na baadaye kuadhibiwa kwa kufanya makossa.

Angalau tumeanza kuelewana katika suala la adhabu za kukomoa. Kamati zetu sasa zimeanza kurudi kwenye utamaduni wa soka, tena la kulipwa kwa kutoa adhabu zinazofikirisha kwa aliyekosa na kama ana busara basi ajirekebisha akijua anaweza kuadhibiwa vikali zaidi asipojirekebisha.

Msemaji wa Azam FC, Thabiti Zakaria amefungiwa miezi mitatu kujihusisha na soka baada ya kuwatuhumu waamuzi kuwa waliingilia matokeo ya mechi zao na kusababisha wanyimwe penalti.

Kwa kawaida si kosa kukosoa mwamuzi kwa kuwa nao ni binadamu na wanaweza kufanya makosa wakati wowote. Lakini ukosoaji huo usifikie kiwango cha kuonyesha kuwa makosa yao ni makusudi na yalilenga kufanikisha kitu fulani. Hiyo itamaanisha mwamuzi alishiriki kupanga matokeo, kitu ambacho ni kigumu kuthibitisha.

Unaweza kufikia hatua ya kutoa kauli kama hiyo pale utakapokuwa na ushahidi usioacha shaka. Huyu alistahili adhabu ndogo inayompa fundisho kuwa si vizuri kurusha tuhuma zinazochafua watu bila ya kuwa na ushahidi, maana huku nje ya soka angepelekwa mahakamani na kuna uwezekano akilipishwa fidia kwa kumdhalilisha mtu.

Sioni tatizo kwa adhabu yake, ingawa Haji Manara anaweza kunyoosha kidole na kusema ìunaona? Angekuwa Haji angelipishwa Sh 20 milioni na kufungiwa miaka miwili juu hata kama makosa hayalingani.

Kitu kilichonisikitisha kwake ni kitendo chake cha kuponda klabu nyingine zinapolalamikia uamuzi. Msimu uliopita alisema redioni kuwa Azam ni klabu ambayo haiwezi kulalamikia waamuzi, licha ya kwamba inaona makosa mengine kwenye mechi zao. Alisema hivyo baada ya Manara kulalamikia maamuzi dhidi ya Yanga.

Huu umekuwa ndio mtindo wa wasemaji na hata baadhi ya viongozi wa klabu. Kuchekana na kucharurana. Matatizo ya waamuzi yanahusu klabu zote, hivyo si vizuri kuchekana bali kuungana na kutoa sauti moja kuwa kuna tatizo katika uamuzi ili mamlaka zichukue hatua.

Wakati Lucas Paqueta alipoonyeshwa kadi ya njano kwa kupiga kanzu ya kunyanyulia mpira kwa kisigino (rainbow flick), ulimwengui ulistuka na kusema sasa burudani kwenye soka imekwisha. Tukio lilitokea Brazil, lakini wachezaji wengi Ulaya walizungumzia wakipinga kuwa hilo litasababisha ladha ya soka iondoke. Ndivyo klabu zetu zinavyotakiwa kuhamaki wakati maamuzi mabovu yanapozidi.

Kuhusu waamuzi, pia baadhi ya wadau tumekuwa tukipiga kelele muda mrefu kuwa wanaowaadhibu hawana ufahamu wa masuala ya uamuzi. Uamuzi ni taaluma maalum inayohitaji wanataaluma washughulikie wakosaji. Ndio maana hata mahakimu na majaji wana vyombo vyao vya kuwashughulikia. Taratibu za kumuondoa jaji ni ngumu mno kwa nchi yenye weledi.

Tatizo langu ni kama Kamati ya Waamuzi ina programu za kurekebisha waamuzi wanaofanya makosa yanayosababisha waondolewe kwenye ratiba. Sijui kama Kamati ya Waamuzi ina mfumo wa kufuatilia waamuzi na kujua mwenendo wao wa makosa, kiasi kwamba wakiletwa mbele yao wajue wanachotakiwa kufanya ni nini hasa. Hivi ni vitu ambavyo TFF inatakiwa iviandae ili waamuzi wetu wafuatiliwe na programu ziwepo za kuwaboresha wakati wanapopelekwa mbele yao kwa ajili ya kuadhibiwa.

Tunahitaji waamuzi walio na muda mrefu kazini ili uzoefu wao uongeze ubora katika soka na si wale wanaobadilikabadilika kila siku, huku kila mmoja akija na tatizo lake jipya. Tukifanya hivi tutakuwa tunaadhibu waamuzi kila siku huku ubora wa uamuzi ukizidi kuporomoka.

Ndio maana mashabiki wa soka wanaweza kutaja hata waamuzi 10 wa Ligi Kuu ya England kwa kuwa wanawaona kila mara. Na hao wako kwenye kundi la elite au select group, yaani waamuzi wenye viwango vya juu.

Kama ilivyo kwa Waingereza, Professional Game Match Officials Limited (PGMOL), humpangia kila mwamuzi mwandamizi mstaafu ambaye kazi yake ni kuchambua kila uamuzi akitumia video na taarifa za matukio kupima kiwango cha mwamuzi. Wachezaji na waamuzi wa zamani hupima usahihi wa maamuzi na usimamizi wa mchezo. Hii husaidia kujua ubora wa waamuzi na udhaifu wao ambao pia husahihishwa kwa kubadilishana uzoefu. Ni vigumu kwa mazingira kama haya makosa kujirudia. Hivi ndio vitu vya kuiga na si kulinganisha ukali wa adhabu kuhalalisha tunachofanya huku.

Kichekesho ni adhabu kwa Singida Big Stars na Tanzania Prisons kufungiwa kusajili kwa angalau dirisha moja. Singida ilimsajili Metacha Mnata wakati ikijua alikuwa na mkataba na Polisi Tanzania, wakati Prisons ilimsajili kipa Mussa Mbissa akiwa hajamalizana kimkataba na Coastal Union.

Hapa ni kama kasisi afungishe ndoa ya mwanamke ambaye ni mke wa mtu, halafu kesho amuadhibu mwanaume aliyeoa mke wa mtu kwa madai kuwa ametenda dhambi. Hata kama kanuni zinatetea vipi suala hili, lakini kuna kitu hakijakaa sawa kabisa.

Kanuni hiyo itakuwa inaondoa umuhimu wa mkataba na kuwapa kiburi wachezaji wanaweza kuingia mkataba na klabu mpya, wakijua adhabu haitawakumba wala kuathiri kazi yao ya uchezaji, huku klabu zikiona kuwa kama adhabu ni kufungiwa dirisha moja, basi zifanye kila ziwezavyo kumnyakua mchezaji zinayemtaka kwa hali na mali zikiwa zimeshajipanga kutosajili dirisha linalofuata.

Klabu ndogo pia hazitakuwa na nguvu ya kunufaika na vipaji zinavyovipandisha kwa kuwa wakati wowote zinaweza kupokwa.

Hapa kuna vichekesho ambavyo ni lazima viondolewe mapema ili heshima ya mikataba ibakie kama vile inavyomzuia Ronaldo kuondoka Manchester UJnited, au Manzoki kujiunga na Simba.

Columnist: Mwanaspoti