Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

AMRI SAID: Tulisaini kocha mkuu na Matola

Amri Saidi Pic Kocha wa KVZ, Amri Said

Fri, 6 Jan 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Maisha ya soka yanaweza kujenga undugu kwa wachezaji. kama anavyoeleza Kocha wa KVZ, Amri Said kupitia mchezo huo ni kama wamezaliwa tumbo moja na Seleman Matola ambaye ni kocha msaidizi wa Simba.

Katika mahojiano yake anawashauri wachezaji wa sasa kuishi kwa upendo wakitambua wanaweza wakakutana sehemu nyingine ya kusaka riziki.

“Hakuna kitu kibaya kama kuishi kwa hila, soka ni mchezo unaomfanya mchezaji asiwe na makao maalumu, hivyo ni vyema wakaishi kwa upendo kuna siku watasaidiana, kama ilivyotokea baina yangu na Matola.

“Ushindani wa kazi haimanishi wafanyiane mambo yasiyofaa, maana hakuna anayeijua kesho ya mwingine zaidi ya Mungu, ndio maana hata makocha leo unamkuta huku kesho kule.”

STAM LILIANZIA HAPA

‘Stam’ alilopachikwa na mashabiki wa Simba, akifananishwa na beki wa kati wa zamani wa Man United aliyekuwa akifanya vizuri kipindi hicho, jina lake kamili aliitwa Jaap Stam.

“Huyo Stam ambaye ni raia wa Uholanzi alikuwa beki mahiri duniani, hata mimi nilimfuatilia sana, lakini nikashangaa mashabiki wamenipachika jina hilo hadi leo hii wapo wanaoniita hivyo,”anasema.

MAISHA YAKE NA MATOLA

Anasimulia ukaribu wake na Kocha Matola wamekuwa pamoja, wamecheza na kufundisha pamoja na hawaitani marafiki badala yake wamegeuka kuwa ndugu.

Nani alikuwa kocha mkuu Lipuli? Anajibu “Wakati nakwenda Lipuli nilitangazwa kama kocha mkuu, lakini Matola alikuwa ameishasaini mkataba kama kocha mkuu, baada ya kuungana naye tulifanya kazi kwa pamoja tukiyaishi malengo ya Lipuli bila kujali nani ana cheo.

“Matola ndiye aliyenipigia simu kwenda Lipuli ni kipindi nilichotoka kumaliza Leseni B, baadaye nilienda Mbao FC na bado tuliwasiliana maana sisi ni tunashauriana mambo ya kimaisha na kisoka.”

SOKA LA BARA NA VISIWANI

Anasema Bara wachezaji wanachoshwa na safari ya kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine na kuna wakati wanatembea usiku kwa usiku ili kuwahi kituo cha kuchezea mechi.

“Pamoja na Zanzibar hakuna sapoti kubwa ya soka tofauti na Bara ambako kiuchumi wapo juu, ila mechi zinachezwa uwanja mmoja wa Amaan, kwa siku zinaweza kuchezwa mbili ama tatu, hivyo mchezaji anaweza akajiandaa saa 10:00 jioni mchezo ukawa saa 2:00 ama saa 3:00, hivyo wanakuwa hawana uchovu.

“Kiufundi Zanzibar kuna vipaji vya hali ya juu, nimeona viungo na washambuliaji wenye uwezo mkubwa na kama timu za Bara zikija kuwekeza skauti huku baada ya miaka kadhaa zitafanya makubwa zaidi, wachezaji wa Bara wengi wanajituma lakini vipaji vipo vichache.”

KVZ anayoinoa inashiriki Kombe la Mapinduzi kwa mara ya kwanza anazungumzia hilo “Niliwahi kushiriki huko nyuma nikiwa na Majimaji, Simba kama mchezaji na kocha msaidizi, hivyo nina uzoefu ni fursa kwa wachezaji kuonyesha vipaji vyao.”

Anasema ya timu yao iko katika michuano hiyo ni kuwasaidia kuwajenga zaidi ili watakaporejea kwenye ligi waweze kuendeleza vichapo kwa wapinzani wao.”

Kiukweli nguvu zetu tumezielekeza kwenye ubingwa wa ligi kwani mkuu wa kitengo hiki anatamani tuandike historia hiyo, hivyo Kombe la Mapinduzi litatuweka fiti zaidi.”

Amri ambaye ana Leseni B na anaisaka A, anasema licha ya zamani kucheza kwa umahiri mkubwa, haimanishi kwa sasa akiwa kocha wachezaji watumie mfumo wa uchezaji wake badala yake anapenda kuwaona wakifanya makubwa na anajitahidi kuwajenga na kuwapa maarifa zaidi.

“Nafurahi zaidi kuwaona wachezaji wanafanya makubwa na wakiwa chini ya viwango ni kazi yangu kuwaelekeza ili wawe bora, kila mtu Mungu amempa kitu chake, hivyo hawawezi kucheza kama nilivyocheza mimi, hivyo wale niliyocheza nao zamani walijue hilo mambo yamebadilika,” anasema.

Ili kuthibitisha zamani haiwezi kulinganishwa na sasa, ni uchumi wao nyakati hizo ambapo walizichezea timu bila mikataba, tofauti na kipindi hiki ambacho soka limekuwa biashara kubwa duniani.

“Ndio maana mafanikio wanayoyapata huwezi kulinganisha na sisi, wanaocheza kwenye viwango vya juu ni matajiri, nyakati hizo tulijulikana na kupewa zawadi na mashabiki lakini siyo pesa za usajili,” anasema.

UBAHARIA

Je, unataka kujua isingekuwa soka Amri Said angekuwa nani? Anajibu: “Ningekuwa baharia ni kitu ambacho nilikisomea na vyeti ninavyo, ingawa sijawahi kuifanya kazi hiyo zaidi ya kuvuavua samaki nyakati hizo, kabla sijabobea kwenye soka.”

Anasema kutokana na kupenda soka, kunamfanya kijana wake Amza (17), amuunge mkono baada ya kuona anajikita zaidi na fani hiyo na sasa amempeleka kufanya mazoezi na kikosi B cha JKT Tanzania, baada ya kumaliza kidato cha nne.

“Nina watoto wawili, kwa namna ulimwengu ulivyoharibika siwezi kuwalazimisha wafanye kitu wasichokitaka, huyu wa JKT ni mchezaji mzuri ipo siku kila mtu atakiona anachokifanya uwanjani,” anasema.

UBONDIA VIPI?

“Nyumbani kwetu Kinondoni kuna mabondia wengi na makocha wao ni marafiki zangu, kuna wakati wananiita kwenda kuwapa sapoti ya kuwafundisha mazoezi ya stamina na najua sheria za mchezo huo vizuri sana,” anasema.

KIKOSI CHAKE

Kikosi Mohamed Mwameja, Said Sued, Kureshi Ufunguo, Amri Said, Boniface Pawasa/ George Masatu, Seleman Matola, Steven Mapunda, Shekhan Rashid, Madaraka Seleman, Yusuf Macho, Ntenze John, kikosi hiki kwa Simba kilikuwa bora sana.

Amri Said anasema mastraika waliokuwa wanamsumbua ni kutoka Mtibwa Sugar kina Monja Liseki na Noah.

“Hao jamaa waliniwanyima usingizi walikuwa na vipaji vikubwa sana, kipindi hicho nilikuwa Majimaji ya Songea.”

Columnist: Mwanaspoti