Kijamii

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Lifestyle

SIL

MenuKijamiiMaoni
Articles

ACT-Wazalendo dhihirisheni uzalendo, acheni akina Lissu wapige kelele

D813c06891955ffd990d49af00f3f25e ACT-Wazalendo dhihirisheni uzalendo, acheni akina Lissu wapige kelele

Wed, 9 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

NIANZE makala yangu kwa kumpongeza Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo, Seif Sharif Hamad ambaye juzi aliteuliwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Mwinyi, kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na jana ameapishwa.

Aidha, Dk Mwinyi amewateua Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Nassor Ahmed Mazrui na Mwanasheria Mkuu wa chama hicho, Omar Said Shaaban, kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Hii ndiyo inanifanya niseme: “ACT- Wazalendo mmeonesha uzalendo kwa nchi kama jina la chama chenu linavyosema, sasa shirikianeni na Watanzania wazalendo kuijenga Tanzania; acheni Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wenzake, waendelee kupiga kelele za kutafuta huruma kwa wasio na macho, au walio nayo, lakini hawayatumii kuuona ukweli.”

Hali hii leo inanikumbusha moja ya mazungumzo na gazeti hili mintarafu sababu za watu kuua wenza wao katika ndoa ambapo mtaalamu wa saikolojia katika Jeshi la Polisi ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Maboresho, Kamishna Msaidizi Mwanadamizi wa Polisi (SACP), Englibert Kiondo, alisema katika jamii wapo watu ambao kisaikolojia huitwa ‘sadist.’

SACP Kiondo akasema: “Siku zote watu hawa hufurahia kusababisha au kuona watu wengine wanapata maumivu na kuwa katika uchungu na masikitiko. Kwao hao, huona hayo ni mafanikio. Huwa hawapendi kuona furaha na utulivu. Ni watu wabaya sana katika jamii.”

Nimemkumbuka SACP Kiondo takribani mwezi mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani uliofanyika nchini Oktoba 28, 2020 na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuibuka na ushindi wa kishindo kwa kiti cha urais, idadi ya wabunge na hata madiwani.

Chadema kilipata kiti kimoja cha ubunge katiba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Jimbo la Nkasi Kaskazini, kilichochukuliwa na Aida Khenan.

Chama cha Wananchi (CUF) kilipata wabunge watatu wawili kutoka Zanzibar na mmoja kutoka Bara huku ACT-Wazalendo kikipata wabunge wanne kutoka Zanzibar.

Baada ya uchaguzi huo ambao Chadema walistahili kuwa na wabunge 19 wa viti maalumu, chama hicho kinachoongozwa na Freeman Mbowe (Mwenyekiti), Tundu Lissu aliyegombea urais wa Tanzania na sasa yuko nje ya nchi (Makamu Mwenyekiti) na John Mnyika (Katibu Mkuu), kilizuia wabunge wake kwenda bungeni kikidai hakikubaliani na wala hakiutambui uchaguzi huo.

Hali hiyo inayoonesha kuwa kuna mawazo tofauti ndani ya Chadema, lakini kwa kuogopana, ilisababisha wabunge hao 19 walioapishwa na Spika Job Ndugai, kuvuliwa uanachama wa Chadema.

Wakiongozwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee, hivi karibuni, wabunge hao wamesema wanakata rufaa dhidi ya uamuzi huo ndani ya chama.

ACT-Wazalendo nao wakiongozwa na Kiongozi Mkuu wa Chama, Kabwe Zitto, Mwenyekiti (Maalim Seif Sharif Hamad) na Katibu Mkuu Ado Shaibu, waliingia katika msafara huo wa kugomea matokeo ya uchaguzi na kuzuia wateule wake kwenda bungeni.

CUF chini ya Mwenyekiti wao, Profesa Ibrahim Lipumba, kilionesha ungwana na kutoa baraka zote kwa waliochaguliwa kwenda bungeni kulitumikia taifa.

Wakati umma ukizidi kushangaa tukio la wabunge wa viti maalumu kuapishwa na kisha chama kuwavua uanachama kwa madai wamekwenda kinyume na msimamo wa chama, ACT-Wazalendo wamechukua ‘akili za kuambiwa, wakachanganya na zao.’

Wakatambua hakuna mantiki wala busara kuendekeza msuguano na ubabe usio na tija huku mioyo ya wanachama wao na Watanzania wengine wapenda amani na maendeleo ‘ikiumia.’ Kwa hili ni kama vile wamesema wazi kuwa, wao si ‘ma-sadists’.

Jumapili iliyopita, ACT- Wazalendo kupitia kwa Katibu Mkuu wake, kilitangaza kuwa Kamati Kuu ya itapeleka jina la Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) ili kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) sambamba na majina ya madiwani, wawakilishi na wabunge waliopatikana kutokana na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 28, 2020.

Kwa mujibu wa chama hicho na wadadisi wengine wa mambo ya kisiasa nchini, uamuzi huo wa kamati ulilenga kulinda matakwa ya kitaifa ya ujenzi wa amani licha ya kuwa chama hicho hakikubaliani na matokeo ya uchaguzi huo.

"Kamati Kuu imeona iyafanye haya baada ya kuona kuwa hali ya uhasama Zanzibar imerudi upya kutokana na makovu ya Uchaguzi wa Mwaka wa 2020 na kuona Zanzibar inahitaji busara kubwa kutokana na uchaguzi huo," alisema Shaibu.

Wanasema hatua hiyo imelenga kuhakikisha kuwa matukio hayo zikiwemo chuki hayajirudii katika uchaguzi mwingine nchini na pia, kuendelea kulinda amani na utulivu ulilodumu nchini tangu uhuru.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, historia ya Zanzibar kila baada ya uchaguzi imekuwa ikigubikwa na vurugu hasa baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa hali ambayo wakati mwingine, husababisha vifo kwa baadhi ya watu hivyo, ACT-Wazalendo haipo tayari kuona hali hiyo ikijirudia wala kuendelea.

Ndipo ACT-Wazalendo inaanza kujijengea heshima na imani kama chama cha siasa baada ya Shaibu kusema, chama hicho kitaendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuhakikisha ustawi na maisha ya wananchi yanaendelea kulindwa.

Kimsingi, hatua ya ACT-Wazalendo inajibu ungwana na utawala bora wa kidemokrasia wa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kukiandikia barua chama hicho kutaka jina la makamu wa kwanza wa rais na kutenga nafasi mbili za uwaziri kwa chama hicho ambazo ni waziri wa afya na waziri wa viwanda.

Dk Mwinyi alisema ametimiza utashi wa kikatiba wa kukiandikia chama hicho ili kitoe majina kwa ajili ya nafasi hizo.

Ikumbukwe kuwa, katika Uchaguzi wa Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi alishinda kwa asilimia 76.27 huku mpinzani wake Maalim Seif akiwa mshindi wa pili kwa asilimia 19.87 zinazokiwezesha chama chake kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Ili kuunda serikali hiyo, mgombea ambaye ni mshindi wa pili anapaswa kupata zaidi ya asilimia 10 ya kura zote.

Katiba hiyo ya Zanzibar inataka ndani ya siku 60 tangu kufanyika uchaguzi mkuu, chama cha upinzani kinachounda serikali ya umoja wa kitaifa kiwe kimepeleka jina la makamu wa kwanza rais na kwa mujibu wa utaratibu huo, ACT ilitakiwa iwe imeshapeleka jina kabla ya Desemba 27 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Katiba ya ACT, anayekuwa makamu wa kwanza wa rais si lazima awe yule aliyegombea urais Zanzibar, bali mwanachama yeyote. Hata hivyo, tayari Seif ameteuliwa kushika wadhifa huo na kuapishwa kulitumikia taifa. Hongera Rais Dk Mwinyi, hongera Maalim, Seif.

Leo nimeandika makala haya nikishangaa kwani wakati Watanzania wanapongeza ukomavu wa ACT-Wazalendo katika suala hili kiasi cha kuamua kushirikiana na serikali kulijenga taifa kwa ustawi wa Watanzania, mmoja ameweka katika mtandao wa Jamii Forum, chapisho linaloanza kwa maneno, “Anaandika Mhe. Tundu Lissu.”

Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, badala ya kupongeza, andiko hilo linaonesha namna anavyobeza hatua ya ACT-Wazalendo kujitoa kujenga taifa.

Nashindwa kuyarudia ‘maneno taka’ aliyoyaandika Lissu (kama kweli ni yake) kwa kuwa, nitakuwa sehemu ya wanaopoteza uzalendo kwa taifa kiasi cha kuumizwa eti ninapoona Watanzania Bara na Zanzibar wanaimarisha umoja na upendo wa kidugu.

Hii ni kwa kuwa napenda watu wafurahi, wapendane, waungane, washirikiane na kuwa na umoja.

Sitaki kuyarudia kwa kuwa mimi si ‘sadist’ ninayependa kuona kila wakati Watanzania ama wa Bara, au Zanzibar, wana majeraha mioyoni mwao eti nikilenga kuifanya nchi hii ya ‘asali na maziwa’ isitawalike; ndoto za mchana mtu akitembea.

Hata hivyo, moja ya aya alizoandika inasomeka hivi: “…Masikitiko yangu ni kwamba amekubali (Seif) kutumika namna hii katika uzee wake. Baada ya miaka karibu arobaini ya kusimamia maslahi ya Wazanzibari, sasa amekubali kutumikia maslahi ya Tanganyika!”

Mungu wangu! Huyu ndiye aliyekaa ughaibuni, kisha akaja kugombea urais wa Tanzania huku akiwa na tiketi mkononi ya kurudi ughaibuni; ndiye anayesema maneno taka namna hiyo dhidi ya nchi anayotaka kuiongoza. Maneno taka hayo ni mengi. Hivi kama Watanzania wangesinzia na kumpa urais, angelifanyaje taifa hili!

Miongoni mwa maneno taka anayoyaandika ni kuwa, nafasi ya makamu wa kwanza wa rais ni kama mfupa maana haina mamlaka yoyote ya maana kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar! Na kwamba, amepewa ili atulie na awatulize Wazanzibari wanaomuunga mkono na jumuiya ya kimataifa.

Hii nayo inanifanya nianze kuamini kuwa Lissu ni sadist. Kama kufanya hivyo kutawatuliza Wazanzibar na wataungana kuijenga nchi, Lissu anaumia nini? Hataki watulie! Anataka wawe wasaliti wa nchi yake kama anavyofanya?

Anasema: “Maalim Seif atalipwa mshahara na marupurupu mengine na kupigiwa saluti na mapolisi…. Zaidi ya hapo hatakuwa na chochote.” Heee! Angekuwa Lissu angetaka chochote kipi? Kuleta mabeberu kunyonya uchumi na rasilimali za taifa?

Ndiyo maana ninasema, ACT- Wazalendo mmefikia uamuzi mzuri, unganeni na Watanzania wenzenu Bara na Zanzibar kujenga Tanzania.

Acheni Tundu Lissu apige kelele baada ya kukosa urais maana maneno mengine, yanaonesha wazi kuwa bado anaweweseka na jinamizi la uchaguzi alipodhani majeraha ya kushambuliwa, aliyoyatumia kutafuta ‘kura za huruma’, ndiyo yangempa urais na si utumishi bora na uadilifu hata katika namna anavyozungumza.

Acha yeye na Mnyika watumie nguvu yao ya maneno katika chama kuwakomoa wanachama 19 waliokwenda kuwawakilisha wanawake wa Tanzania bungeni, waliokwenda kuongeza sauti ya kukosoa serikali.

Acha wazidi ‘kukikaanga chama chao juu ya mafuta wakidhani wanakikirimu, kumbe wanakiunguza’ maana kama kweli wana msimamo, basi hata ruzuku hawatapokea na pia, chama hakitakuwa na pa kusemea wala kusikika. Acha wasidi kuziba midomo kwa plasta wakijidai ni mabubu.

Hata hivyo wajue kuwa, hawalikomoi Bunge wala Serikali, bali wanawakomoa Watanzania ambao wana macho na akili zao hivyo, wanawasubiri katika ngwe nyingine watakapokuja kuomba kura nyingine za huruma kwa staili nyingine.

Columnist: habarileo.co.tz