Msanii wa Bongo Fleva, Zuchu akiwa katika picha ya pamoja na Diamond Platnumz. Kuna watu wapo kwa ajili ya kukupa moyo kwenye maisha ya kipaji. Wao watakusifia kuwa unaweza. Watakuambia wewe ni mkali sana na kwenye ‘gemu’ lazima utoboe.
Hata hivyo, wengi wao huwa ni ‘chawa’ tu kama inavyofahamika siku hizi.
Lakini vipaji ndiyo kila kitu. Angalia kina Lady Jaydee; ana vipaji, Ndivyo ilivyo kwa wanadada Ray C, Linnah, Mwasiti, Nandy, Maua Sama na Ruby.
Kwa wanaume utakutana na Q Chilla, Juma Nature, Marlaw na wengineo.
Nakumbusha tu; Mwana FA pamoja na kipaji chake hakukaa na kujisifu kabla ya kumuonyesha njia Maua Sama.
P Funk hakutaka sifa ili kumtoa Juma Nature. Ndivyo kwa G Lover (Guru), alikiona kitu ndani ya Mr Blue kisha akamuonyesha njia sahihi na kutoka.
Jide na Ray C, walikuwa watangazaji kabla ya kujikita jumla katika muziki baada ya kushauriwa na Ruge Mutahaba.
Sasa tumtazame Zuchu, msanii wa kike mwenye kipaji cha muziki aliyeshikwa mkono na Diamond Platnumz.
Binti huyu ana kipaji, ambacho anakiendeleza, ana usimamizi mzuri na nyota ya kupendwa muziki wake. Hili ni jambo alilonalo Zuchu.
Wapo watu au wasanii wenye vipaji sana lakini nyota inakosekana.
Zuchu ni msanii asiye na miaka hata mitano katika gemu yaani tangu aanze kuimba lakini leo hii akitoa ngoma hata mwalimu wake kimuziki Mondi anakaa chini kusikiliza kipaji.
EP yake Mondi aliyofanya na Zuchu pekee ndiyo ilikimbiza zaidi baada ya WCB huko nyuma kutamba sana na ngoma ya Harmonize ‘Kwangwaru’.
Hapo kati hakuna ngoma iliyovuka mipaka wa ngoma hiyo hadi alipokuja Zuchu na kutoa ngoma ya ‘Sukari’ ambayo ilitikisa kwelikweli kimuziki.
Nje ya ‘Kwangwaru’ na ‘Sukari’, ndani ya WCB hakuna ngoma iliyotikisa zaidi kushinda ngoma hizo. Mwenendo wa Zuchu kimuziki uko safi kwani kila akitoa ngoma, wafuasi wa Bongo Fleva wanafuatilia kwa wingi hivyo kupata watazamaji wengi kwenye mtandao wa YouTube na kuingiza mkwanja mrefu.
Binti huyu ana vitu vinne kamili vya mwanamuziki wa sasa.
Kipaji cha kutunga, sauti nzuri, ujuzi wa kucheza na uongozi bora alionao na zaidi ana nyota yake kali.
Lakini nimekuwa nikiwaza mara kwa mara kwamba hiki kipaji cha binti huyu wa Kizenji, kingekutana na akili za Ruge Mutahaba mambo yangekuwaje?
Kwa sababu kushikwa mkono na mtu anayejua ukitakacho, hilo nalo ni neno!
Kwa mfano; Wengi hawajui kama Afande Sele ni zao la Sugu kwamba ndiye aliyeona kitu ndani yake na kumshika mkono.
Dunia ya muziki wetu haikumjua Afande Sele kabla ya Sugu kumleta kwetu kwa kumshika mkono. Kama ambavyo na Sele alikiona kitu kwa Dogo Ditto naye kumshika mkono.
Kuna wanamuziki wengi sana ambao wameshiriki kuinua wasanii wenzao, akiwamo Dully Sykes, ambaye kwa kiasi kikubwa alikuwa taa kwa vijana wa Kariakoo na Ilala akiwemo Ali Kiba. Hakuna staa wa Ilala asiyetambua nguvu ya Dully.
Kuna Juma Nature, mpaka kesho anaendelea kuwa daraja la masela kibao kule Temeke. Na siyo kwa masela wa Temeke tu, hata Chegge kutoka Kigoma huko alishikwa mkono na Nature.
Hata hivyo, kiukweli kuwa na kipaji ndio jambo la msingi kisanaa. Kukiendeleza ni suala mtambuka. Usimamizi na watu sahihi wa kukuongoza ni bahati nasibu sana.
Mondi licha ya kumuongoza vizuri kimuziki Zuchu, chachu imeongezeka zaidi wawili hao baada ya kuinga katika penzi.
Upo uwezekano kuwa wanatunga ngoma wakiwa wametulia usiku mnene.
Ukitaka kuamini maneno yangu sikiliza ngoma yao ya ‘Mtasubiri’, imeeleza mengi kuhusu uhusiano wao na mipango yao ya baadaye na ndio maana nasema kutamba kwa Zuchu sio bure.