Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zuchu aweka wazi maisha yake

428da06f5667a8eabe7451b497980134 Zuchu aweka wazi maisha yake

Mon, 8 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MSANII bora wa kike, Zuhura Othman Soud au Zuchu amefunguka kuhusu maisha yake binafsi ya muziki na kusema mafanikio yake ya sasa hayatokani na kubebwa, bali juhudi na uvumilivu mkubwa alionao katika shughuli za sanaa.

Msanii huyo ambaye anafanya muziki wake katika miondoko ya Bongo Fleva na Afropop ameachia ngoma nyingine mpya ya mapenzi katika mahadhi ya Pop wa Number One majuzi ingawa bado anakimbiza na kibao cha Sukari, amesema hahitaji ushindani kwani presha inayotokana na muziki wake inatosha.

Kufikia jana mchana katika mtandao wa kawaida wa Youtube, Sukari iliyoachiwa Januari 20,2021 ilikuwa na watazamaji 15,729,603 huku Number One aliyoiachia juzi tu ilikuwa na watazamaji 66,219.

“Kushindana kunaleta faida gani, mimi najenga carrier yangu, kuachia Sukari kunanipa presha..” alisema akimaanisha kazi hiyo bora inamfanya kufikiria kazi nyingine bora zaidi ili kukonga nyoyo za mashabiki wake.

Zuchu aliyejiunga na lebo ya WCB Wasafi Records mwaka 2020 chini ya uongozi wa Diamond Platnumz, amesema yeye haoni faida ya kupambanishwa kwani hapati faida yoyote.

Alisema hana mpango wa kupambanishwa wala kufanya ushindani na msanii yeyote yule, akitolea mfano wa Beyonce na Robyn Rihanna na kusema Beyonce mpaka leo bado anawika kwani hakufanya ushindani bali alijenga kazi zake.

Alipoulizwa kuhusu kujiunga na lebo ya WCB, alisema kwamba anamshukuru Mungu kwa kumwezesha kufanya uchaguzi sahihi wa lebo hiyo ambayo inamtoa.

Aidha, aliongeza kuwa uvumilivu kabla hajatoka umempa nguvu kubwa ya kutambua umuhimu wa uchapakazi. Akizungumzia uhusiano wake na Diamond, alisema ni bosi wake wala hana uhusiano wa kimapenzi kama watu wanavyofikiri na wala hajawahi kumfikiria kimapenzi kwani ni bosi wake.

Alisema kuna mipaka hata ya mazungumzo baina yao ingawa mara kadhaa bosi wake huyo alikuwa anamtania mbele ya wenzake kwamba: “Eti watu wanasema wewe ni mzigo wangu.”

Aidha, Zuchu ambaye alianza kazi ya sanaa baada ya kumaliza diploma ya juu ya CEBA nchini India, alisema kwa sasa ana mahusiano mazuri na baba yake mzee Othman Soud na kwamba askari huyo wa zamani (baba yake) wanazungumza vyema japo wakati alipoachana na mama yake hapo katikati alikuwa kimya sana.

Alimwambia mtangazaji maarufu wa kipindi cha Refresh cha WCB, kuna wakati alimwandikia barua baba yake akihoji kwanini hamtembelei au sio baba yake mzazi kitu kilichomfanya mzee huyo kufika nyumbani kumuona na kumwachia Sh 20,000 za sikukuu ya Idd akiwa mdogo.

Zuchu anasema katika mahojiano inaonekana wakati mama na baba yake walipoachana ni kama vile baba yake naye alimwacha, lakini alikuwa anaendeleza mawasiliano na mwaka jana mama yake alipomwambia baba yake anaumwa walienda kumtazama.

Zuchu aliyezaliwa Novemba 22, 1993 Zanzibar aliwahi kutunukiwa tuzo ya Silver play button na mtandao wa kijamii wa Youtube kwa kuwa msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufikisha wafuasi zaidi ya 100,000 ndani ya wiki moja.

Pia msanii huyo aliyepata tuzo ya msanii bora chipukizi wa mwaka 2020 na All Africa Music Awards (AFRIMMA), anasema si rahisi kufanyakazi na Diamond Platnumz na kolabo zake mbili za Cheche na Litawachoma na naye hazikupatikana kirahisi bali ni kwa jasho kubwa.

Zuchu pia amefanya kolabo na mama yake, Khadija Kopa wimbo wa Mauzauza na Nobody na Joe Boy. Alisema Diamond alimpa siri ya kutoka kimuziki kwa kumwambia aimbe muziki anaojua kuimba kwani waimbaji ni wengi duniani lakini aina ya uimbaji wake (taarabu) utamtoa.

Zuchu aliyezaliwa kwenye familia ya wanamuziki, mama mwimbaji wa taarabu Kopa na baba Othman anasema katika udogo wake alilazimika kujitafutia marafiki mwenyewe kwani umaarufu wa wazazi wake ulikuwa unatafsiriwa vibaya na kumletea shida.

Alisema jambo ambalo mpaka leo hana raha nalo ni kifo cha nduguye Omar Kopa kwani ndiye alikuwa mlezi wake wakati huo kwani hakuwa karibu na wazazi wake waliokuwa na shughuli nyingi.

Anasema mpaka sasa hasikilizi nyimbo za kaka yake huyo na wala hajawahi kwenda kwenye kaburi lake, kwani anahofia kurejesha machungu ya kifo chake.

“Nikimkuta mtu anasikiliza nyimbo zake huwa namwambia azime akikataa naondoka,” alisema. Zuchu aliachia albamu ya kwanza iliyotambulika kama ‘I am Zuchu’ mwaka 2020 ikiwa na nyimbo saba ukiwamo wa Hakuna Kulala.

Albamu yake hiyo ndiyo iliyosikilizwa na watu wengi zaidi nchini mwaka jana na video za nyimbo zake zimetazamwa na mamilioni ya watu duni

Chanzo: www.habarileo.co.tz