Msanii wa Bongo Fleva, Zuhuru Othman maarufu Zuchu huenda akakamuliwa Sh500 milioni kwa kudaiwa kuiba wimbo wa msanii wa Injili, Enock Jonas huku lebo yake ikionesha kutokuwa tayari kuzilipa fedha hizo.
Katika malalamiko hayo Jonas, amedai Zuchu amechukua sehemu ya kibwagizo na staili ya kucheza katika wimbo wake wa 'Wema wa Mungu' ambao ulitoka mwaka 2012 lakini ulijulikana zaidi kwa jina la 'Zunguka'.
Taarifa za madai hayo zilianza kusambaa mitandaoni kupitia barua iliyoandikwa na kampuni ya wanasheria ya Gerpat Solution, ambapo mmoja wa wake Gerlad Magubuka, amesema leo Jumamosi Oktoba 22 kuwa mteja wao alikwenda kuwalalamikia Zuchu kutumia kionjo cha wimbo wake huo.
Magabuka amesema tayari wameshawapelekea wahusika barua ya madai hayo na nakala nyingine wamepeleka Taasisi ya Hakimiliki Nchini (Cosota) na Shirikisho la Wanamuzi Tanzania (Shimuta).
“Katika kufuata taratibu tayari jambo hilo lipo Chama cha Muziki wa Injili Tanzania na ambao hawa ndio wa kwanza hutakiwa kukaa na kama litashindikana watajua hatua zingine zipi wazifuate kwani wote wanatoka familia moja ya muziki,” amesema mwanasheria huyo.
Kwa upande wake, Enock amesema amelazimika kuchukua hatua hiyo baada ya mazungumzo na upande wa Zuchu kushindikana kwa kumwambia kuwa katika madai hayo hata Sh2 milioni hawawezi kumlipa.
Amesema majibu hayo alipewa na mmoja wa mameneja katika lebo ya Wasafi, Khamis Taletale (Babu Tale), baada ya kuzungumza naye kwa njia ya simu siku ya Jumanne.
Kwa upande wao Cosota kupitia Katibu Mtendaji wake, Doreen Sinare, amekiri suala hilo kutua mezani kwake na kueleza kilichofanyika ni wasanii wenyewe kuandikiana barua na wao wamepelekewa kama taarifa hivyo hawawezi kusema lolote kwa sasa wameacha wasanii wenyewe ndio wawasiliane kwanza na baadaye wao watakuja kuichambua na kuitolea tamko.
Kwa upande wake Babu Tale alipotafutwa kuhusiana na tuhuma hizo, alikiri kuwasiliana na msanii huyo na kumpa majibu hayo ya kutompa hela aliyoitaka.
“Ni kweli niliwasiliana na Enock kwa simu, akanimbia anataka alipwe fedha kutokana na wimbo huo na nilipomuuliza unataka Shilingi ngapi, aliniambia ngoja akate simu atanirudia, dakika chache alipopiga tena akasema anataka Sh10 milioni, nilichomjibu hata tano hupati na sio tano hata tatu hupati wala mbili,” amesema Tale.
Hata hivyo, Tale alivyoulizwa ni hatua gani wanazichukua baada ya kutolewa kwa madai hayo na wanasheria wa msanii huyo, amesema mashtaka ya muziki yana mahakama zake za kimuziki na utaratibu wake watakazozifuata.
Mmoja wa wanasheria aliyebobea katika masuala ya hakimiliki, ambaye hakutaka jina lake litajwe, amesema ukisikiliza wimbo wa Zuchu una melody zinazofanana na wa ‘Wema wa Mungu’ na kama msanii huyo atapata wanasheria wazuri wakumsimamia anaweza kushinda.
“Katika kuiga kazi ya mtu hatuangalii tu maneno, bali melody kwa kiasi kikubwa ambao ndio wimbo wenyewe, pia kipande ambacho wimbo huo umependwa zaidi kwani watu ndio hapo wanapoukumbuka wimbo uliowahi kuimbwa na unaona hata kwa Zuchu kipande cha zunguka ndicho kinapendwa na suala la maneno yaliyotumika na namna yalivyoimbwa,” amesema mwanasheria huyo.
Wimbo wa 'Kwikwi' umetoka wiki mbili zilizopita na mpaka sasa huko Youtube unafanya vizuri kwani umeshatazamwa zaidi ya mara milioni nne.Wakati wimbo 'Wema wa Mungu' ambao umetoka mwaka 2012 umetazamwa mara 342, 000.