Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zuchu: Mwaka mmoja tu kaweka rekodi na kibao na kazivunja mwenyewe

Zuchu Pc Data Zuchu: Mwaka mmoja tu kaweka rekodi na kibao na kazivunja mwenyewe

Mon, 12 Apr 2021 Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz

Msanii wa Bongofleva, Zuchu ametimiza mwaka mmoja tangu atambulishwe rasmi kujiunga na lebo ya WCB. Usiku wa Aprili 8, 2020 lebo hiyo ilitangaza kumsaini mwimbaji huyo ambaye ni mtoto wa Malkia wa Taarabu nchini, Khadija Kopa.

WCB ilikuwa hajamsaini msanii mpya toka Januari 28, 2018 ambapo walimsaini Mbosso ambaye baada ya kuvunjika kundi la Yamoto Band alipotea kimuziki. Diamond Platnumz ambaye ndiye mmiliki wa WCB alieleza kuwa Zuchu alisubiri kwa kipindi cha miaka minne ndipo wakaamua kumtoa kwa sababu walitaka aelewe kwanza maisha ya kisanii yalivyo.

Je, miezi 12 ya Zuchu ndani ya WCB ina maana gani hasa kwake kimuziki na upande wa Bongofleva kwa ujumla? Hakuna ubishi ni kipindi kifupi ambacho kimempeleka kwenye kilele cha mafanikio.

Aprili 12, 2020 Zuchu alitambulisha Extended Playlist (EP) yake ya kwanza inayokwenda kwa jina la ‘I Am Zuchu’ ambayo ina nyimbo tano. Wimbo wa kwanza kuachia unaitwa ‘Wana’ ambao ulitoka kabla ya EP hiyo, video yake ilitazamwa zaidi ya mara milioni 1 kwenye mtandao wa YouTube ndani ya siku mbili.

Zuchu ndiye msanii wa kwaza WCB kutambulishwa kwa mtindo wa kuachia EP, wenzake kama Harmonize, Rayvanny, Rich Mavoko, Queen Darleen, Lava Lava na Mbosso, hawakupata bahati hiyo.

Kutokana na kupata mapokeo makubwa, ilimchukua wiki moja kufikisha wafuatiliaji 100,000 kwenye mtandao wa YouTube. Kwa mujibu wa Diamond, Zuchu ndiye msanii wa kwanza wa kike Afrika kufikisha mafanikio hayo hadi sasa.

Hilo lilienda sambamba na mapokeo mazuri ya EP yake, ‘I Am Zuchu’ ambayo ndani ya siku 26 pekee katika mtandao wa Audiomack ilisikilizwa zaidi ya mara milioni moja.

Kufikia Agosti 5, 2020, Zuchu aliweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza Tanzania kufikisha wasikilizaji milioni tatu kupitia EP hiyo ndani ya mtandao wa Boomplay pekee.

Februari mwaka huu tayari Zuchu alikuwa amefikisha wasikilizaji milioni 14.4 katika mtandao wa Audiomack, Spotify 91,000, Boomplay akifikia milioni 21 na YouTube milioni 146.

Umaarufu wa kazi zake, kipaji na promosheni ya lebo yake, vilimwezesha ndani ya miezi mitano tu kufikisha wafuasi milioni moja kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram ambapo hadi sasa wamefika zaidi ya milioni 2.4.

Haya yameongeza thamani ya muziki wake na kukua kwa chapa yake kibiashara. Julai 29, 2020 Meneja wa WCB, Sallam SK alitangaza kuwa thamani ya Zuchu ni Sh20 milioni, hivyo yeyote atakayemuhitaji kwenye shoo, lazima alipe kiasi hicho.

Mwanzoni mwa Desemba 2020 waandaaji wa tuzo za Grammy waliripoti Zuchu kufanikiwa kuingia kwenye hatua ya kujadiliwa (consideration) kwa ajili ya kuwania tuzo ya mwanamuziki bora chipukizi.

Ingawa hakufanikiwa upande wa Grammy, takribani siku 24 nyuma alishinda tuzo kutoka African Muzik Magazine (Afrimma) kutokea Marekani akiwa msanii bora anayechipukia.

Hadi sasa ametimiza mwaka mmoja tangu atoke kimuziki, Zuchu ameshinda tuzo moja, huku akichaguliwa kuwania tatu tofauti ambazo hakufanikiwa kushinda.

Aliufungua mwaka 2021 kwa kuachia wimbo ‘Sukari’ uliotoka Januari 19, 2021, na video yake kutizamwa zaidi ya mara milioni moja ndani ya saa 22 katika mtandao wa YouTube na kuwa msanii wa kwanza wa kike Tanzania kuweka rekodi hiyo na kufikia Februari 19 mwaka huu, ilifikisha watazamaji milioni 10, ikiwa ni wiki mbili tangu itoke na kumfanya kuwa msanii wa kwanza wa kike Afrika Mashariki kufikia mafanikio hayo.

Machi 26 mwaka huu Zuchu alifanikiwa kufikisha wafuatiliaji milioni moja kwenye mtandao wa YouTube na kuwa msanii wa kwanza wa kike Tanzania na Afrika Mashariki kufanya hivyo. Kwa ujumla anakuwa msanii wa tano Tanzania kufikia rekodi hiyo baada ya Diamond, anayeongoza akiwa na milioni 5, Rayvanny milioni 2.6, Harmonize milioni 2.4 na Mbosso milioni 1.3.

Chanzo: www.mwanaspoti.co.tz