Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

SIL

Zembwela alia kutukaniwa familia yake kisa DP World

Dp Kitenge Zembwela Zembwela alia kutukaniwa familia yake kisa DP World

Wed, 26 Jul 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mtangazaji wa Kipindi cha Good morning kinachorushwa kwenye kituo cha Wasafi FM anayetambulika kwa jina maarufu la Zembwela ameelezea masikitiko yake kufuatia matusi na maneno yasiyokuwa ya kiungwana anayoshambuliwa yeye binafsi na familia yake iliyomzunguka kwa kile kinachodaiwa kusababishwa na uwepo wa sakata la DP World linaloendelea kushika kasi hapa nchini kwa sasa.

Akizungumza kwenye Kipindi hicho jana, Jumanne Julai 25, 2023 Zembwela ambaye hivi karibuni aliambatana na Watangazaji wenzake Maulidi Kitenge na Gerald Hando kufanya ziara ya kutembelea nchini Dubai kwa lengo la kujionea jinsi kampuni ya DP World inayotajwa kuingia mkataba wa makubaliano ya uwekezaji Bandarini baina yake na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mamlaka ya usimamizi wa Bandari.

Amesema walichokifanya Watangazaji hao ni kuonesha ubunifu wa kuandaa Kipindi chao ili kutengeneza maudhui yatakayowavutia watu wengi zaidi kuwafuatilia kwakuwa uendeshaji wa vipindi na vyombo vya Habari kwasasa unahitaji ubunifu mkubwa ili 'kuteka' watu, jambo ambalo ni tofauti na vile ambavyo baadhi ya watu wameitafsiri safari hiyo.

Ametolea mfano uwepo wa baadhi ya makampuni ambayo yaliwahi kutajwa kufanya uwekezaji hapa nchini huko nyuma lakini baadaye makampuni hayo yalikuja kugundulika kuwa ni hewa na yaliisababishia taifa hasara ya mabilioni ya fedha hivyo moja ya jambo walilolenga kulifanya kwenye ziara hiyo ni pamoja na kwenda kujionea na kujiridhisha kama kampuni ya DP World ipo na kama inajishughulisha na masuala ya bandari au la, jambo ambalo amethibitisha kuwa wamejionea na kujiridhisha baada ya kuunganishwa na baadhi ya Watanzania wanaoishi Dubai.

"Kuna wale jamaa ambao wanamiliki klabu ya Kikapu kule wakatusaidia kutuunganisha, kwahiyo tukaenda tukaiona DP, kweli tukakuta wana Ofisi na sio richmond style.

"Tukakuta kweli wanafanya shughuli za Bandari, tukatembelea Bandari yao, ila walikataa kuzungumzia hiki kinachoitwa makubaliano sijuwi mkataba kwasababu sio level yetu na wale tuliowakuta Ofisini sio level yao..."

"Return yake ilikuwa Watanzania wanataka sisi ambao hatujuwi vifungu vya sheria tukifika pale DP tuwaulize kwenye mkataba pale kifungu cha 3C, kifungu kidogo cha 4D ibara ya 5 mmesema mtachukua Bandari kwa upana gani.

"Matokeo yake Mimi, walionizunguka, Wazazi wangu, Viungo vya mwili vya Wazazi wangu na mimi mwenyewe, wote tuliingia katika vinywa na maandishi ya Watanzania na nadhani mpaka sasa bado wanaendelea kututusi, kwahiyo njia pekee ambayo mimi niliichukua ni hiyo ya kukaa kimya."

Chanzo: www.tanzaniaweb.live