Unaweza kumuita vyovyote lakini kwa mashabiki wa soka jina la Bugatti ndio linabamba zaidi pindi unapomzungumzia Haji Manara. Usiku wa kuamkia leo Bugatti ameteka tena mitandao ya kijamii na vyombo vya habari baada ya kutangaza kuwa atafunga ndoa na mpenzi wake mpya, Zaiylisa.
Katika usiku huo wa Bugatti alimvalisha pete mpenzi wake huyo, ambaye pia ni staa wa tamthiliya ya Juakali ambayo inabamba sana kwenye king’amuzi cha Dstv.
Kabla ya hapo Bugatti na Zaiylisa walikuwa wameteka vichwa vya habari baada ya kutangaza kuwa ni wapenzi na kuachia picha na video wakiwa mapumzikoni.
Hata hivyo, kwenye tukio hilo Bugatti alitoa ahadi kwamba, kwa Zaiylisa ndio itakuwa ndoa yake ya mwisho kwake.
Kauli hiyo imepokewa kwa mtazamo tofauti na mashabiki wa Bugatti huku baadhi wakimpongeza na kumtakia kila lenye heri.
Licha ya kuahidi kuwa itakuwa ndoa yake ya mwisho, pia aliahidi kumpenda mkewe huyo mtarajiwa na kumpa kila furaha anayostahili. Hiyo inatokana na kile kinachodaiwa kwamba, ndoa za Manara zinaweza kufika tano mpaka sasa na Zaiylisa itakuwa ni ya sita.
Japo ndoa yake na Ruby na Rushaynah ndizo zilivuma, mama yake mzazi aliwahi kunukuliwa mwaka 2022 akibainisha kuwa kijana wake huyo amefikisha ndoa ya tano.
Ilikuwa ni kwenye ndoa yake na mke wa pili, Rushaynah ambayo mama mzazi huyo alipodokeza akisema alishtushwa pindi alipoletewa taarifa kuwa kijana wake anataka kuoa.
Kilichomshitua ni kuwa haikuwa imepita muda mrefu tangu Manara alipofunga ndoa na Rushaynah, ambaye kwa sasa wameachana na inaelezwa yuko kwenye penzi jipya na msanii wa Singeli.
Jana katika hafla ya kumvisha pete Zaiylisa, Manara alisema:"Ndoa zote nilikuwa nataka ziwe za mwisho, lakini binadamu tunapitia mitihani, katika hii naomba Mwenyezi Mungu anivushe iwe ndoa yangu ya mwisho."
Alisema, kimaadili sio sifa nzuri kusifiwa kuoa hata kama sheria inaruhusu, akiahidi ndani ya siku chache zijazo ambazo hazitazidi 10 atamuoa Zaiylisa.
Manara, ambaye alianza kwa kumsifia mkewe mtarajiwa huyo kwamba gauni alilokuwa amevaa ni la bei mbaya na limenakishiwa kwa vito vya Tanzanite, alisema toka wamejuana si muda mrefu.
"Lakini wanaokuona kwenye muvi, mitandaoni na uhalisia wako ni tofauti na hauiigizi, nakupenda sana," ilikuwa ni kauli ya Manara katika hafla hiyo iliyokwenda sanjari na siku yake ya kuzaliwa.
Alisema, watu hawajui ni yapi wanapitia, dunia haijui ni yapi wanayokutana nayo lakini katika tukio lake na Zaiylisa anamuomba Mungu amuepushe na mitihani na hiyo iwe ndoa yake ya mwisho.
"Chuki ni nyingi, lakini tunaombeni dua zenu," ilikuwa ni kauli ya Manara akiwambia wageni waalikwa ambao, walilipuka kwa furaha huku mwenyewe akiahidi kumfanya kuwa miongoni mwa wanawake wenye furaha nchini.
"Ninachokihitaji kwako (Zaiylisa) ni heshima, nipe heshima yangu kama mwanaume wa Kiafrika na nitakuheshimu kama mwanamke," ilikuwa ni kauli ya Manara kwa mkewe mtarajiwa huyo, kauli ambayo imeibua gumzo.
Baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii wametofautiana kuhusu hilo, wengine wakiwaombea kila lenye heri katika safari hiyo ya ndoa na kuamini itakwenda kudumu, huku wengine wakiponda na kudai walimshamzoea na hata kwa Zaiylisa itakuwa kama zilizotangulia.
Miaka miwili iliyopita (2022) Manara alikuwa akiambatana na wake zake, Ruby na Rushaynah kwa pamoja katika maeneo mbalimbali, ikiwamo kwenye usiku wa muziki wa dansi ambako aliingia nao pamoja na kuwa gumzo kuhusu maisha yake na wake zake hao. Hata hivyo, Januari mwaka jana, minong'ono ilianza kuzagaa kuwa Manara amemwagana na 'bi mdogo' Rushaynah, ambaye chanzo cha minong'ono hiyo ni baada ya mkewe huyo kufuta picha zote alizokuwa amepiga na mumewe.
Siku kadhaa baadaye, Manara kupitia ukurasa wake wa Instagram aliachia ujumbe mrefu akimuomba msamaha mkewe wa kwanza, Ruby kwa kumletea mke wa pili., huku pia akimtakia kila la kheri katika safari yake ya ujauzito na kujifungua salama.
Julai mwaka huohuo kukawa na minong'ono ya kumwagana na Ruby kwa talaka tatu, kabla ya usiku wa kuamkia leo alipotangaza kumchumbia Zaiylisa na kubainisha kwamba, siku 10 zijazo ndoa itafungwa na itakuwa ya mwisho.
Mwanamuziki, Naseeb Abdul (Diamond) alimweleza Manara kwamba, mtarajiwa wake huyo hana makando kando na kuwaombea Mwenyezi Mungu awabariki wafunge ndoa.
Diamond aliyekuwa miongoni mwa waalikwa alisema: "Nilitakiwa nisafiri jana (Jumatano iliyopita), nikasema siwezi kuondoka kwa sababu ya jambo la kaka yangu.
"Wengi wanazungumza mambo mengi yaliyopita, nyuma ulipata kitu kiko hivi, na sasa Mungu amekupa cha juu zaidi, huyu hana makando kando, nawaombea muwe na maisha marefu mfunge ndoa na hii iwe ya mwisho.:
Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ambaye aliwataja pia kuwa kwenye hafla hiyo na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, John Kayombo alisema wamehudhuria kwa mambo mawili makubwa.
"Aliponiambia nikamwambia nitakuja, kwanza kuwa shahidi kwa hiki anachotaka kukifanya na ninaamini kitadumu zaidi katika maisha yako, pili nitakuja kujifunza mambo mengine mazuri ambayo Haji anayafanya.
"Tunawaombea kila la heri katika hili, mlichokusudia kukifanya kikadumu milele na milele," alisema Chalamila kwenye hafla hiyo.
Mama wa Zaiylisa alisema alipoambiwa kwa mara ya kwanza mahusiano ya binti yake huyo, ambaye ni wa pili kuzaliwa na Manara hakushtushwa.
"Sikuwa na wasiwasi kwa kuwa ni mwanamke na mwanamume, alikuja kujitambulisha na tulifuata taratibu za dini. Mpaka sasa jambo hili limefika hatua hii, niwatakie kila la heri kwenye ndoa yao hii mpya," alisema mama huyo akikataa kuzungumza zaidi.
Mama mkubwa wa Zaiylisa alisema binti yao huyo hapaswi kusikiliza maneno ya watu kwani kila mtu ataongea lake, lakini Manara atabaki kuwa ni mumewe. Alisema maneno ya mitandaoni hayakuipa shida familia kwa kuwa kila jambo Mungu ndiye anapanga, hivyo hayakuwapa presha kama familia.
Mama yake Manara alisema anashindwa kuongea, lakini akamsisitiza kijana wake kujenga kiwanja cha Bunju ambacho alitamka kwamba ni zawadi ambayo amempa kijana wake huyo.
"Kile kiwanja kule Bunju ukakijenge, nakwambia na Zai (Zaiylisa) ananisikia najua ni mtoto mwema nilishaongea naye, hiyo ni zawadi yangu ambayo nimekukabidhi, sina mengi ya kusema nawatakiwa kila la heri ,".