Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zari ‘Uzee’, Wema ‘Ugumba’, Hamisa ‘Uchawi’

16307 Zari+pic TanzaniaWeb

Sun, 9 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Watoto siku zote wakishiba au wakikosa kitu cha kufanya wasumbufu sana. Watarukaruka, watagombana, kupiga kelele nk. Mwisho wazazi huwalazimisha kulala au kuwapa kazi ya kufanya ili watulie.

Hawa mastaa wa kike Hamisa, Zari, Wema na wengineo wengi tu. Wameshiba sana au hawana kazi ya kufanya. Kama wameshiba basi wamevimbiwa sana na wafuasi wao pia wameshiba na hawana kazi ya kufanya. Yaani wapo kama matope ya pale Jangwani jirani na ofisi za mradi wa mabasi ya mwendokasi.

Mtoto aliyeshiba au kukosa kitu cha kufanya huishia huleta usumbufu mwingi. Kama wazazi au walezi wasipochukua hatua haraka ya kumpa kazi ya kufanya au kumlazimisha kulala kama siyo kumchapa lazima afanye uharibifu kwanza.

Irene Uwoya ni miongoni mwa watoto ambao hawajashiba ila wamekosa kitu cha kufanya. Mwisho wa siku haelewi afanye nini na kuishia kutundika picha kelefu kwenye mitandao.

Kisanaa mzazi hapa ni Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA). Ndiye ambaye anapaswa kuwalea hawa watoto, kuwaongoza na kuwaamuru ama kuwaelekeza njia sahihi wanapopotoka. Mpaka sasa hili jukumu ni kama zito kwao.

Mwenye majukumu mengi sana ya kikazi ni ngumu kupata muda wa kidwanzi kwenda ufukweni, kuchojoa nguo sahihi na kuvaa zisizo sahihi, kuweka pozi tatanishi na kupigwa picha. Kama haitoshi na akatundika picha hizo mtandaoni.

Huko ni kushiba au kukosa kazi ya kufanya. Kupigwa tofauti na kupiga picha, mpigaji ana kazi ya kufanya. Ndiyo maana wanaishia kupiga picha kwenye makorido na vyumba vya mahotelini bila kueleweka kabisa kama ni wahudumu au nao ni wateja.

Achana na TCRA, kuna ujinga mitandaoni unaofanywa na wasanii ambao huhitaji rungu la Mamlaka ya Mawasiliano nchini kuchukua hatua. Ni busara za watendaji wa Basata kuamua kulivalia njuga (sijui njuga ndo nini?) na kulifanyia kazi. Wao wako kimya mpaka wasikie kelele za watu.

Lakini kwa Basata hii ya kusubiri mpaka watu wapigie kelele picha za Uwoya ndo waamke. Ni ngumu sana na siamini kama wana kitengo au mtu wa kufuatilia maisha ya wasanii mitandaoni.

Basata wapo maili nyingi nyuma. Wameachwa na nyakati hizi na umri wao hauwezi kwenda sambamba na kasi ya ulimwengu wa sasa. Usishangae kila siku wanafungia wasanii au nyimbo ambazo tayari zina zaidi ya mwaka mitaani.

Wanachelewa kujua kinachoendelea kitaa. Wamekariri kusikiliza sauti ya B Dozen wa XXL, Dullah wa Planet Bongo na wenzao ili wajue kinachoendelea kwenye muziki. Wakati dunia yote ipo YouTube ambako hayupo Adam Mchomvu wala Dj Tass, watu wakiwa ‘bize’ na Oya Jibebe Bebe.

Usishituke Kwangaru ukifungiwa. Sababu ikawa haya maneno: “Nataka kucheza chura na ingali umesimama, Aah, inama inama. Unataka maji ya kisima na mwoga kuchutama, Unataka kupiga deki wima umesimama, Si unataka vya pool table sa’ mbona unajibana, Aah, inama inama.”

Wakasisitiza kuna maneno ya uchochezi kama: “Oh, basi jilegeze, nikubebe mgongoni (iyelewi), Kitandani nikoleze, kwa miuno ya kingoni (iyelewi), Kisha nibembeleze, Nirudishe utotoni (iyelewi), Weka mate niteleze, Kama nyoka pangoni (iyelewi).

Basata wanachelewa na muda unaenda kasi sana. Siyo kwamba hawajui majukumu yao, hapana. Ofisi yao ina mazingira ya kijima ya karne ya 20 huku ikiwa na majukumu ya teknolojia ya kisasa kwenye karne ya 21. Lazima waachwe kwenye kona za Iyovi.

Sasa kama Basata walichelewa kujua makosa ya wimbo kama Halellujah au WakaWaka na nyinginezo walizofungia. Ni lini masikio yao na macho yataona na kusikia wanachofanya na kuongea mitandaoni Amber Lulu na Gigy Money?

Shilole aliwahi kufungiwa na Basata kwa kosa la picha alizopigwa (siyo kupiga) akiwa Ulaya kwenye shoo (Ubelgiji kama sikosei). Lakini tazama hiyo picha na picha za kina Amber Lulu, Gigy Money na wenzao mitandaoni. Ni kichekesho.

Ikumbukwe Shilole alikuwa Ulaya ambako mtoto anaweza kucheza nusu utupu mbele ya wakwe zake. Hawa kina AmberLulu wapo mitaa ya hapa hapa Mwananyamala uso kwa macho na vibaraza vya Basata. Au hawatambuliki kama wasanii Basata?

Watu waliotoa nyimbo zinazosikika wasitambulike Basata? Leo hii mtu unaweza kupeleka gazeti mitaani kihunihuni tu kina Dk Abbas pale Idara ya Habari Maelezo wakuache ukitanua mabega kama unatembelea magongo?

Yote haya ni kwa sababu ya kuacha mambo yajiendee tu bila kusimamiwa. Wasanii wamekuwa wakilumbana, kutukanana na kuchafuana mitandaoni lakini hakuna anayekemea wala kushituka.

Diamond na Ommy Dimpoz walivuana nguo mitandaoni, runingani, redioni na magazetini. Wanahabari wakachekelea kupata habari zao lakini Basata wakawa wanasubiri video na nyimbo za kufungia tu.

Malezi ya Basata kwa wasanii ni kuzingatia mashairi na video tu? Mambo mengine wanaachiwa wenyewe? Ndiyo maana bendi zinajifia kwa zuio la kufanya shoo kama ‘beseidei’ ya mtoto eti shoo mwisho saa sita, lakini husikii Basata wakitetea.

Anaitwa Zarina Hassan ‘The Boss Lady’. Mwanamke mwenye kila sababu sahihi ya kutolewa mfano kama mwanamke mrembo, kiasi cha mwanaume yeyote awaye rijali angemtamani. Mwenye sura na mwili laini kama nyama ya mkia wa Kondoo.

Alifanikiwa kutikisa Jiji la Dar es Salaam na Tanzania nzima, baada ya kuukabidhi mwili wake nyoronyoro kwa Simba kutoka Mbuga ya Tandale Diamond Platnumz. Wengi hawakuamini mwanadada huyo kujiweka kwa msela wa Tandale aliyehamia Madale.

Wa kuamini waliamini na wa kutoamini hawakuamini. Mpaka pale alipofyatua kiumbe kwenye tumbo lake kiitwacho Tiffah Dangote. Licha ya sifa zote hizo za urembo lakini hakuonekana lolote mbele ya swala waliotamani kutafunwa na Simba wa Tandale.

Wasichana wa kimjini (mwili mtaji). Wadangaji na wale wa kumchukulia poa Diamond kabla ya uwepo wa Zarina kando yake, wakaanza visa. Walimtoa kasoro zote Zari kana kwamba ni wasaidizi wa Mungu kwenye uumbaji. Na kujaribu kumtenga kwa Uganda wake.

Pamoja na kasoro zote, baada ya Zari kumfyatua ‘sister duu’ Tiffah, akamdondosha ‘brazamen’ safari hii wa kuitwa Nillan. Hapo sasa habari ikageuka na kuanza kumsengenya kwa umri wake akiitwa Bibi Kizee na jina akapachikwa la Bi Tukinao.

Ingawa siyo rasmi lakini ukweli ni kwamba wengi wao waliomkosesha raha mwanamke huyo wa Kiganda, ni wasichana wa mjini ambao ama walipenda Diamond awe na Wema au wao ndo Swala waliotaka kutafunwa na Simba.

Wakati mashambulizi yakiendelea kwa Zari, ndipo likaja sakata la Hamisa. Hapo ikagundulika kuwa wasichana wa Kibongo si kwamba waliona Zari mzee au Diamond anafaa kuwa na Wema. Waligundua kuwa wamechezea fursa.

Wakati wote huo waliomtetea Zari wakiamini Team Wema ndiyo wanaomtukana wakawa wanamuita Wema Mgumba. Wema alishambuliwa kwa kuitwa Mgumba sawa sawa na Zari alivyoitwa Bibi Kizee. Kumbe madem wa mjini walitaka fursa ya mkwanja wa muziki.

Zari anavyopenda kuonekana kigoli mtamu mwenye urembo wake, kuitwa Bibi Kizee hakuficha hisia zake za kuumizwa na hilo. Mara nyingi aliwajibu waliomsakama mitandaoni kama ilivyo kwa Wema alipowajibu waliomuita tasa au mgumba. Haya yaliwaumiza sana.

Mazingira haya yalitengenezwa na wasanii wenyewe. Kwa tabia zao za kutumia mitandao ya kijamii kutukanana, kulumbana na kushambuliana huku Basata wakiwa siyo tu kimya bali hawajui hata kinachoendelea kwenye mashambulizi ya wasanii mitandaoni huko.

Kama Basata wanatumia redio na runinga kutazama kazi za sanaa, sasa watambue kuwa mitandao hivi sasa ni zaidi ya runinga redio na magazeti kwenye mambo yanayohusu sanaa. Huko ndipo kwenye kila kitu kinachohusu sanaa.

Zari kumzalia Diamond akaitwa Bibi Kizee na maneno mengi mpaka kukimbia nyumba. Wema kutomzalia Diamond akaitwa tasa, mgumba na mengineyo. Hamisa Mobetto naye kaona isiwe tabu naye baada ya kumzalia Diamond kafanya vituko vingi na sasa anaitwa mchawi.

Zari alipoitwa Bi Kizee, Wema na wafuasi wake walikongwa nyoyo zao. Wema alipoitwa tasa na mgumba, ilikuwa furaha kwa Hamisa na wafuasi wake, hawataki kuona Wema anarudi kwenye himaya ya Diamond baada ya Zari kukimbia nyumba.

Leo hii Zari katulia Afrika Kusini na watoto wake, huku nyuma wakwe zake na mkwe wao new model wanashikana uchawi. Waliomuita Zari Bi Kizee mara Bi. Tukinao sasa wanaitana tasa na mchawi. Vita imebaki kwa watu wawili ‘Utasa Wema’ na ‘Uchawi Hamisa’. Usisahau msemo wa... achekae mwisho?

Chanzo: mwananchi.co.tz