Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Yatima adai kuchoshwa na vitendo vya kichawi vya bibi yake

Dae7109c3d5fc0ff9be554a090b0951f Yatima adai kuchoshwa na vitendo vya kichawi vya bibi yake

Thu, 24 Dec 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

HUDUMA za ‘Mkono kwa mkono zinazotembea’ kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, zimemwibua mtoto yatima aliyekwenda kulalamika, akisema amechoshwa na vitendo vya bibi yake kusafiri naye kwa ungo usiku na kufanya mambo ya kichawi.

Kutokana na hali hiyo, Mwanzilishi na Mratibu wa Huduma za Mkono kwa Mkono maarufu ‘one stop center’ katika Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Dk Christina Onyango, amesema mtoto huyo wa darasa la nne(jina limehifadhiwa) ametafutiwa makazi salama huku taratibu nyingine zikiendelea.

Katika siku ya mwisho ya huduma za ‘one stop center mobile’ katika Viwanja vya Ofisa Mtendaji wa Kata ya Kiwalani jijini Dar es Salaam, ukiwa ni mwendelezo wa maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia yaliyoanza Novemba 25 na kuhitimishwa Desemba 10, 2020, Onyango alisema tangu Desemba 11 hadi Desemba 22, mwaka huu, huduma hizo zimewafikia wananchi 1,552 katika Kata za Chanika, Pugu, Gongolamboto, Segerea, Vingunguti, Buguruni na Kiwalani.

“Zaidi ya watu 7,800 walifikiwa na elimu kwa umma kwa njia ya mazungumzo ya ana kwa ana, vipeperushi na matangazo kwa umma,” alisema.

Kuhusu tukio la mtoto huyo wa kike, Onyango alisema: “Tukiwa Chanika, kuna mtoto alitoka shule baada ya kusikia tuko pale; akawambia wenzake nakwenda kusema mambo ya bibi...alipofika akasema kila siku bibi yake (jina limehifadhiwa) anamchukua kwa ungo usiku na kwenda kwenye mambo ya kichawi na yeye sasa amechoka na hataki.”

Wakati binti huyo wa darasa la nne anakwenda pale, watoto wenzake wa Shule ya Msingi Chanika walikwenda kumwambia bibi yake.

“Labda kwa kujua anayoyafanya, bibi akaja akiwa mkali kwelikweli anasema kwa nini mtoto wake amekuja hapo na anataka kwenda polisi kutoa taarifa, lakini tukamwambia sisi ni Jeshi la Polisi ndiyo akawa mpole,”alisema Onyango na kuongeza:

“Baada ya mazungumzo, ikabidi huyo mtoto tumhamishie katika makazi salama ili kulinda usalama wake huku hatua nyingine zikiendelea kwake na kwa bibi huyo.”

Alipoulizwa hatua walizochukua kama ni kumfungulia mashitaka bibi huyo, Onyango alisema: “Lile ni suala la imani, hakuna jinai; lazima mkae mfanye ‘case conference’ (kujadili suala) akiwamo ofisa ustawi wa jamii, polisi, wanasheria na hata daktari na tulimshirikisha ofisa elimu ili kuzungumza na kuchunguza mambo mengine yaliyo ndani ya suala hili.”

“Miongoni mwa maamuzi tuliyofikia ni ofisa elimu kumtafutia shule nyingine, mtoto kuishi katika makazi salama na mtoto huyo kupimwa afya ya akili kama yupo sawasawa; kwa vyovyote lazima mtoto ahame shule maana pale hawezi kupata utulivu wala kuwa na usalama tena.”

Katika hatua nyingine, Onyango alisema asilimia 90 ya wanaume 820 kati ya watu 1,552 waliojitokeza katika huduma hizo za siku 13, hulalamika wakisema wake zao wanawafanyia unyanyasaji na ukatili ukiwamo wa kupigwa, kutohudumiwa kwa mahitaji kama chakula na kunyimwa unyumba.

Akizungumza katika Kata ya Kiwalani, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Janeth Magomi, alisema mwitikio mkubwa wa wananchi katika huduma hizo ni matokeo ya elimu dhidi ya ukatili wa kijinsia kueleweka na watu kuongeza imani kwa Dawati la Jinsia la Jeshi la Polisi kutokana na ubora wa huduma wanaoupata.

Chanzo: habarileo.co.tz