Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yaliyotikisa upande wa burudani Bongo 2022

Billnass Na Nandy Msadc Yaliyotikisa upande wa burudani Bongo 2022

Mon, 9 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Ni wazi imekuwa ni safari ndefu yenye milima na mabonde, mafupi na marefu, furaha na huzuni katika kiwanda cha burudani Bongo ambapo historia imeandikwa na rekodi kuvunjwa.

Haya ni miongoni mwa matukio yaliyotikisa, kubamba na kupewa uzito katika kiwanda burudani Bongo kwa mwaka 2022 unaolekea kuisha.

1. Harusi Nandy, Wolper

Tukio la Billnass na Nandy kufunga ndoa hapo Julai 16, 2022, ni miongoni mwa mambo yaliyoteka mazungumzo kwa kiasi kikubwa mwaka huu upande wa burudani Bongo kutokana na nguvu ya ushawishi walionao wasanii hao.

Ndoa nyingine iliyochukua usikivu wa watu wa kiasi chake ni ile ya Rich Mitindo na Jacqueline Wolper iliyofungwa Novemba 19, 2022, wawili hao walifikia hatua hiyo baada kujaliwa watoto wawili.

2. Kurejea TMA

Baada ya kukosekana kwa miaka saba, hatimaye mwaka huu zilirejea Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) ambazo ilitolewewa Aprili 2, 2022, huku Alikiba akiwa ndiye msanii aliyeshinda tuzo nyingi zaidi zikiwa ni tano.

Hata hivyo, kitendo cha wasanii wa WCB Wasafi ambao wana ushawishi mkubwa katika Bongofleva kususia tuzo hizo kwa kile walichodai kutoridhishwa na mchakato wake, ni moja ya mambo yaliibua mijadala sana.

3. Rayvanny kuondoka WCB

Ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kuanzia lebo yake, Next Level Music (NLM) inayomsimamia Mac Voice, Julai 12, 2022 Rayvanny alitangaza kuondoka WCB Wasafi, lebo iliyotoa kimuziki mwaka 2016.

Kabla ya tangazo lake, tayari kulikuwa na tetesi kuwa angeachana na lebo hiyo yake Diamond Platnumz kama walivyofanya Rich Mavoko na Harmonize, ila Rayvanny kwa nje inaonekana aliondoka kwa amani.

4. Mtikisiko Konde Music

Katika miaka yake mitano ndani ya Bongofleva, mwaka huu Konde Music Worldwide yake Harmonize ndipo hasa imepita kwenye tanuru la moto!, wasanii wameondoka wenyewe na wengine lebo imeamua kuwapa mkono wa kwaheri.

Januari Country Boy alitangaza kuachana na Konde Music, Oktoba lebo hiyo ikavunja mikataba na wasanii wawili, Cheed na Killy, huku Anjella naye akidaiwa kuondoka, kwa sasa lebo imesalia na msanii mmoja, Ibraah wakati ilianza mwaka na wasanii watano!.

5. Rais Samia kwa Sugu

Mei 31, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa ndiye mgeni rasmi katika tamasha la Msanii wa Hip Hip Bongo, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’, The Dream Concert ambapo alikuwa anasherekea miaka yake 30 katika muziki.

Rais Samia alizundua kitabu cha Sugu ‘Muziki na Maisha’ pamoja na kumpatia tuzo, huko Lady Jaydee, Nikki wa Pili, Mwana FA, Joh Makini, Lord Eyes, AY na G Nako wakitoa burudani.

Ni tukio la kihistoria katika Bongofleva ambalo tasnia itajivunia kwa wakati wote.

6. Kikwete kwa Ommy Dimpoz

Novemba 5, 2022 Rais mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alizindua albamu ya kwanza ya Ommy ‘Dedication’ ikiwa ni miaka 10 tangu atoke kimuziki na ngoma yake, Nai Nai akishirikiana na Alikiba.

Hata hivyo, Ommy Dimpoz sio msanii wa kwanza Bongo kwa albamu yake kuzinduliwa na Kikwete, Machi 2020 JK alizindua albamu ya kwanza ya Harmonize ‘Afro East’ yenye ngoma 18.

7. Zuchu na Simba Day

Ikiwa ni mara yaka ya pili kutumbuiza Simba Day, Zuchu mwaka huu alikuja na ubunifu ambapo haukutarajiwa, nao ni kushuka na kamba katika uwanja wa Mkapa na kutumbuiza katika shughuli hiyo iliyofanyika Agosti 8, 2022.

Utakumbuka Agosti 2020 Harmonize alitumbuiza kwenye kilele cha Wiki ya Mwananchi, tukio lake la kushuka uwanjani na kamba na kile kinachodaiwa alidondoka, haviwezi kuwatoka akilini mashabiki ila kwa Zuchu hilo halikutokea.

8. Tuzo za Filamu Tanzania

Ukiwa ni msimu wake wa pili tangu kurejeshwa na serikali, mwaka huu zimefanyika tena Tuzo za filamu Tanzania, hafla hiyo ilifanyika Arusha hapo Desemba 17, 2022 huku mgeni rasmi akiwa ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa.

Mastaa kama JB, Lamata, Lody Music, Joti, Mkojani, Dorah na wengineo walipokea tuzo, huku JB akisema kwa sasa imetosha kwake apumzishwe katika tuzo hizo.

9. EP ya Diamond Platnumz

Wasanii wengi wametoa EP ila ya Diamond Platumz, First of All (FOA) iliyotoka Machi 11, 2022 ikiwa na nyimbo 10 imetikisa, tayari ina ‘streams’ zaidi ya milioni 15.8 Audiomack, huku Boomplay ikiwa ni milioni 84.4, hii ndio EP iliyofanya vizuri zaidi mwaka huu ikiwa na video saba.

Licha ya ngoma zake kali, bado iliteka mazungumzo mtandaoni kwa kukosolewa kwa madai Diamond katoa albamu na sio EP kwani hakuna EP yenye nyimbo 10, wasanii wa Tanzania walioshirikishwa ni Zuchu na Mbosso pekee na hapa ndipo ulipoanzia ajadala wa Rayvanny kuodoka WCB Wasafi.

10. Albamu, EP za wasanii

Mwaka huu wasanii wa Bongofleva ametoa albamu na EP kwa wingi kama ilivyokuwa miaka mitatu iliyopita, kuimarika kwa njia za mauzo mtandaoni ndipo hasa kumechochea hilo.

Albamu na EP za wasanii zilizotoka na kufanyiwa hafla ya uzinduzi (listening party) ni pamoja na; Khan EP (Mbosso), Goddess (Rosa Ree), King of Hearts (Jux), FOA EP (Diamond Platnumz), Yours Truly EP (Hamisa Mobetto), The Kid You Know (Marioo), Dedication (Ommy Dimpoz), First Born (Beka Flavour) na Cinema (Maua Sama).

11. Harmonize na Kajala

Baada ya kuachana Aprili 2021, Harmonize mwaka huu alianza kampeni (Take Me Back) ili kurudisha mahusiano yake na Kajala, akafanikiwa kufuatia kumtungia nyimbo kama; Vibaya, Mtaje, You na Deka.

Kurudiana kwao ilikuwa ni habari kubwa kutokana waliachana kwa ugomvi hadi kufikishana Polisi, hakuna aliyetegemea Kajala atarudi kwa Harmonize kufuatia madai kuwa Konde Boy alikuwa akimmezea mate Paula, na sasa inadaiwa wameachana tena!.

12. Wema Sepetu tena!

Licha ya kula kiapo cha kutoweka tena wazi mahusiano yake, Wema Sepetu, Miss Tanzania 2006, Agosti mwaka huu kikozi hicho kikamshinda na kuamua kukiri mbele ya umma kuwa hajiwezi na Staa wa Bongofleva, Whozu.

Ikumbukwe Whozu anaingia kwenye orodha ya Mastaa ambao wamewahi kuwa na mahusiano na Wema baada ya Mr. Blue, TID, Steven Kanumba, Chaz Baba, Diamond Platnumz, Idris Sultan, Calisah na Staa wa Big Brother Africa kutokea nchini Namibia, Luis Munana.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live