Mashabiki wa muziki nchini Nigeria hatimaye watapata fursa ya kuwaona nyota wawili wanaopendwa zaidi nchini humo, Davido na Wizkid wakitumbuiza pamoja kwenye ziara ya pamoja ya muziki.
Siku ya Jumatano, Wizkid alitumia ukurasa wake wa Instagram na kuweka tangazo lililowashangaza wengi kuwa atafanya maonesho ya muziki na nyota mwenzake wa muziki, Davido.
Katika ujumbe wa Instagram, Wizkid aliandika, “Baada ya ziara yake ya ‘MLLE (More Love, Less Ego)’ !! Mimi na Davido tutafanya maonesho kwa pamoja! ili kuokoa pesa yako!
Inakumbukwa kuwa Wizkid aliripotiwa kuahirisha kutoa albamu yake ya 5 ya 'More Love, Less Ego' kufuatia kifo cha mtoto wa Davido, Ifeanyi.
Mashabiki walimsifu sana kwa kumuunga mwenzie mkono na kutoa heshima ya kipekee.
Wizkid na Davido waliwahi kutumia jukwaa moja mwaka 2017 mwezi Disemba katika tamasha la Wizkid ambapo Davido alikuja kama mgeni rasmi kutumbuiza.