Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

WiLDAF wazindua siku 16 kupinga ukatili wa kijinsia

A6769e23da686ad29ce439a443a34dcb WiLDAF wazindua siku 16 kupinga ukatili wa kijinsia

Wed, 25 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

SHIRIKA la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali leo wanazindua siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambazo zinatarajiwa kumalizika Desemba 10.

Uzinduzi huo unafanyika jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk John Jingu.

WiLDAF inashirikiana na muungano wa mashirika ya kupinga ukatili wa kijinsia MKUKI kufanikisha kampeni ya siku hizo 16 zinazoanza leo.

Mkurugenzi wa WiLDAF, Anna Kulaya alisema jana kuwa maadhimisho ya mwaka huu watayatumia kupita mikoa mbalimbali ikiwamo vyuoni kutoa elimu kuhusu kuanzishwa kwa madawati ya jinsia.

Alisema siku ya kupinga ukatili wa kijinsia kwa mwaka huu itaadhimishwa kwa kuhamasisha uanzishwaji wa madawati ya kijinsia vyuoni ambayo yatasaidia wanafunzi pindi wanapokutana na ukatili kupeleka malalamiko yao na hatua kuchukuliwa.

Alisema takwimu zinaonesha kati ya matukio 11,726 yaliyoripotiwa, matukio ya ubakaji ni 7,617 sawa na asilimia 64.

Akizungumza katika mafunzo kwa waandishi wa habari, Kulaya alisema "Ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imeonesha asilimia 50 ya waliohojiwa wameeleza rushwa ya ngono vyuoni.

"Ndiyo maana katika maadhimisho ya mwaka huu yaliyobebwa na kauli mbinu isemayo: 'Tupinge ukatili wa kijinsia, mabadiliko yanaanza na mimi' tumeona tuende vyuoni kuzungumza nao pindi wanapokutana na vitendo hivyo wachukue hatua ya kutoa taarifa".

Pia alisema ndani ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kutakuwa na tuzo kwa wanawake 16 waliotoa maisha yao kutetea wanawake wengine.

Pia alisema wataangalia ukatili wa kijinsia unaotokea nyumbani kwa sababu ni moja ya maeneo ambayo yanatakiwa kuwa salama.

Pia alihimiza jamii kuhakikisha inapaza sauti na kufanya mabadiliko maeneo yao.

Mkuu wa Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii), Prudence Constantine alisema vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa sasa vimevuka mipaka na sasa kuna ukatili wa kisaikolojia unaohusisha jinsia zote, lakini taarifa zake siyo za kitosha.

"Serikali imechukua hatua mbalimbali ya kutokomeza vitendo hivi. Upo mpango wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto, tuna mpango wa kupunguza ukatili kwa asilimia 50.

"Yapo madawati ya kijinsia 450 yaliyoanzishwa vituo vya Polisi kwa ajili ya kupokea taarifa za ukatili wa kijinsia, waathirika 58,059 wamejitokeza kutoa taarifa."

Pia alisema Magereza nao wameanzisha madawati 162 nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz