Kati ya moja ya kazi inayofanya vizuri Netflix ni Documentary inayoitwa ‘What Jennifer Did’. Iliachiwa tarehe 10 Aprili 2024. Inafatiliwa na watu wengi na leo nitakueleza ni kitu gani alichokifanya binti huyo mdogo akiwa na miaka 24 mwaka 2010 kwa sasa ana miaka 36 na anatumikia kifungo cha maisha gerezani.
JENNIFER ALIFANYA NINI?
8 Novemba 2010 simu ya huduma kwa wateja ‘911’ ilipokelewa kituo kimoja cha polisi huko Ontario Canada. Sauti ya msichana iliwataarifu polisi kwamba nyumbani kwao kulivamiwa na majambazi wenye silaha na walihitaji pesa.
Binti huyo kwa jina la Jennifer Pan alieleza yeye pekee ndio hakudhurika, alieleza majambazi hao walimfunga kamba, wakawashambulia wazazi wake kwa risasi na kutokomea. Ripoti ya polisi ilieleza mama yake Jennifer, Bich Ha, (inatamkwa “Bick”) alifariki papo hapo lakini baba yake alipata majeraha makubwa na kupoteza fahamu kwa siku mbili.
Katika uchunguzi wa polisi waligundua Jennifer alitoa maelezo mengi ya uongo na yenye utata. Polisi walijiuliza maswali kadhaa mfano ‘kama wauwaji walirusha risasi kwa watu wawili isingekuwa tatizo kwao kumshambulia Jennifer kwa risasi pia’ na pia katika kamera ya jirani (CCTV Camera) karibu na nyumbani kwao Jennifer, ilionyesha wauwaji hao waliingia bila kutumia nguvu yoyote. Na je aliwezaje kupiga simu polisi ikiwa amefungwa kamba?
Ilibainika ni mpango uliosukwa na Jennifer na katika mahojiano yake ya tatu alikiri kwa polisi ni kweli alilipa watu kuwauwa wazazi wake. Hata baba yake alipopata fahamu tarehe 10 Novemba 2010 alisema anadhani binti yake, Jennifer alikula njama na wauwaji hao.
KWANINI ALITAKA WAZAZI WAKE WAUWAWE
Baba yake Jennifer Huei Hann Pann yeye pamoja na mke wake walikuwa ni wakimbizi wachina kutoka nchi ya Vietnam na kuanza kuishi Ontario Canada. Na waliajiriwa katika kiwanda cha kutengeneza vifaa vya gari.
Kama walivyo wazazi wengine baba yake alitamani binti yake asome na kuwa mtaalamu wa dawa za binadamu (pharmacist) na pia mama yake alipenda Jennifer akipata muda wa ziada ajifunze kifaa cha muziki ‘piano’ kwasababu (Jennifer) alikuwa anajua sana kutumia piano tangu akiwa mtoto mdogo.
Ila kwa dunia ya leo tunaweza sema Jennifer alikuwa na mambo mengi kichwani. Mapenzi yalimchanganya kiasi kwamba shule hakuipenda. Aliwadanganya wazazi wake anasoma chuo na haikuwa kweli wakati mwingine walimshusha hadi chuoni (Toronto Metropolitani University) ila alikuwa mlaghai tu.
Jennifer alitengeneza kwa ‘photoshop‘ kadi za matokeo ya mitihani za uongo na maskini wazazi waliamini binti anapiga kitabu kumbe ilikuwa ndivyo sivyo.
Jennifer alizama katika penzi la kijana muuza ‘pizza’ na muuzaji wa dawa za kulevya pia, Danny Wong, waliokuwa kwenye mahusiano kwa miaka saba. Katika uchunguzi wa polisi walifanikiwa kupata diary ya Jennifer na aliandika wamekuwa na kijana huyo katika mahusiano ya kuachana na kurudiana kwasababu wazazi wake hawamtaki kijana huyo. Aliongeza kwamba ana mawazo sana.
Documentary hiyo ya ‘What Jennifer Did’ imepata uthibitisho kutoka kwenye uchunguzi wa polisi na kutoka Mwandishi wa habari za Jinai, Jeremy Grimaldi aliyeandika, A Daughter’s Deadly Deception: The Jennifer Pan Story.
Mwandishi huyo alibainisha katika uchunguzi wake aliona ujumbe kwenye simu ya simu ya Jennifer kutoka kwa aliyekuwa mpenzi wake Danny Wong kwamba amepata muuwaji wa kazi hiyo (kuwauwa wazazi wa Jennifer).
Katika Documentary hiyo polisi wanasema wanaamini Danny alitaka wazazi wa Jennifer wafe ili anufaike na mafao yao kupitia Jennifer ambayo yangemsaidia kukuza biashara yake ya ‘dawa za kulevya’ lakini pia kupata nyumba yao.
Disemba 13 2014 Jennifer Pann alihukumiwa kifungo cha maisha gerezani. Danny Wong na wauwaji wengine pia walihukumiwa kifungo cha maisha. Japo kuna uwezekano wa kesi hiyo kusikilizwa upya baada ya mahakama kukubali ombi la rufaa mwaka 2023 ikisemekana kulikuwa na makosa wakati wa hukumu ya mwanzo.
Baba yake na mdogo wake wa pekee na Jennifer waliomba mahakama iweke pingamizi kwa Jennifer kutoruhusiwa kufanya mawasiliano yoyote na wawili hao waliobakia katika familia. Mahakama ilikubali pia Wong na Jennifer mahakama iliamuru Jennifer asiwasiliane na Danny Wong tena.
Wadau mbalimbali kuhusu afya ya akili wameendelea kutoa maoni yao kuhusu umuhimu wa mawasiliano katika familia. Wengine wakisema inawezekana Jennifer alikuwa na mfadhaiko wa hisia na wazazi wake hawakuweza kugundua mapema.
Nini maoni yako? Je wewe mapenzi yanaweza kukunogea kiasi gani hadi ufikikie hatua kama ya Jennifer? Wangireza wanasema ‘too much is harmful’ kila jambo liwe na kiasi.