Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wema ni mmoja tu Bongo

Wema Pic Data Wema Sepetu

Sun, 2 Oct 2022 Chanzo: Mwananchi

Katika historia ya shindano la Miss Tanzania, Wema Sepetu ndiye Miss aliyeandikwa na kujadiliwa sana na vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii, mtindo wake wa maisha na kazi vinaruhusu hilo kwa kiasi chake.

Mashindano ya Miss Tanzania kwa mara ya kwanza yalifanyika mwaka 1967 na mrembo wa kwanza kutwaa taji hilo alikuwa ni Theresa Shayo, kisha yalisimama hadi mwaka 1994 na mrembo Aina Maeda kunyakua taji hilo.

Baada ya kutwaa taji la Miss Tanzania mwaka 2006, Wema alikwenda kushiriki mashindano ya urembo ya dunia (Miss World) kama ilivyo taratibu yaliyofanyika Warsal, nchini Poland.

Matumaini yalikuwa makubwa kwa Wema, ikiwa ni mwaka mmoja tangu Mtanzania mwenziye, Nancy Sumari kushinda taji la Miss World Africa (Continental Queen of Africa), lakini Wema alishuhudia taji hilo likienda kwa Stiviandra Oliveira kutoka Angola.

Katika Miss Tanzania mwaka 2006, Jokate Mwegelo ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya Temeke ndiye alishika nafasi ya pili, huku ya tatu ikienda kwa Lisa Jensen ambaye mwaka 2012 aliteuliwa na kamati ya Miss Tanzania kupitia shindano maalumu (Miss World Second Chance) kushiriki Miss World.

Hiyo ni baada ya ratiba ya mashindano hayo kubadilika na hivyo kuathiri upatikanaji wa kawaida wa Miss Tanzania kwa mwaka huo ambao Brigette Alfred ndiye aliyetwa taji akiwa na umri wa miaka 18.

Baada ya kukabidhi taji la Miss Tanzania, Wema alielekea nchini Malaysia aliposomea Biashara ya Kimataifa (International Business) katika Chuo Kikuu cha Limkokwing. Hata hivyo, hakumaliza masomo yake baada ya kunogewa na uigizaji wa filamu, kitu kilichokuja kumpata umaarufu zaidi.

Wakati yupo Malaysia ndipo filamu yake ya kwanza kucheza ilipotoka, ‘A Point of No Return’ akitumia jina la Dina, akiwa na marehemu Steven Kanumba ambaye ndiye aliyemuingiza kwenye ulimwengu wa filamu.

Wema na Kanumba waliigiza filamu maarufu kama ‘Family Tears’ (2008), ‘Red Valentine’ (2009) na ‘White Maria’ (2010) ambazo ziliweka jina la mrembo huyo sehemu ya juu kabisa kwenye kada hiyo.

Mwaka 2017 Wema aliachia filamu yake, ‘Heaven Sent’ akiigiza kama mhusika mkuu akishirikiana na Gabo, hii ilifanya vizuri na kuchaguliwa kuwania vipengele saba katika tuzo za Sinema Zetu International Film Festival Award (SZIFF) ambapo alishinda mbili kama mwigizaji bora wa kike na chaguo la watu.

Kwa ujumla Wema ameigiza filamu zaidi ya 25, ameshirikiana na waigizaji wakubwa Bongo kama Jacob Steven (JB), Single Mtambalike, Elizabeth Michael (Lulu), Irene Uwoya, Kajala Masanja, Hemed PhD, Riyama Ally, Aunty Ezekiel, Jacqueline Wolper, Patcho Mwamba, Yusuph Mlela, Gabo na wengineo.

Urembo na filamu vimemfanya Wema kuwa maarufu kabla hata ya mitandao ya kijamii kushika kasi Tanzania na ameendelea kuwa hivyo hadi utawala huu wa Instagram, Snapchat na TikTok.

Hivi karibuni Wema ameandika rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza Tanzania kufikisha wafuasi (followers) milioni 10 katika mtandao wa Instagram baada ya Novemba 2015 kuwa mwanamke wa kwanza tena kufikisha wafuasi milioni 1.

Wema anaifukuzia rekodi ya Zari The Bosslady kutoka Uganda ambaye anaongoza Afrika Mashariki akiwa na wafuasi milioni 11. Mwigizaji wa Kenya, Lupita Nyong’o ndiye alikuwa akiongoza ukanda huo upande wa wanawake, lakini sasa kapitwa na Zari na Wema.

Kwa Tanzania wasanii wa kike wanaomkaribia Wema ni Hamisa Mobetto (milioni 9.9), Shilole (milioni 9.4), Jacqueline Wolper (milioni 9.2), Vanessa Mdee (milioni 8.3) na Irene Uwoya (milioni 7.2).

Hilo linafanya kila mwanamume anayekuja kwenye maisha ya Wema kuzidi kuwa maarufu, kuna wakati mwenyewe alidai kuwa baadhi ya wanaume humuona kama daraja la kuwavusha hadi kwenye umaarufu na amechoka hali hiyo.

Lakini sasa Wema anaishi nje ya maneno yake, hiyo ni baada ya kuzama katika penzi jipya na msanii wa Bongofleva, Whozu. Wema anasema kijana huyo anampa furaha aliyoikosa kwa muda mrefu maishani. Whozu anakuwa mwanaume mwingine maarufu kuwa katika mahusiano na Wema baada ya;

1. Mr. Blue

Kulitunza penzi lake na Wema ilikuwa ni kazi kubwa kwa Mr. Blue, kwani aliwahi kudai alikaribia kufilisika kutokana mrembo huyo kuishi maisha ya gharama zaidi kupita uwezo wake.

Wema alimkosha vilivyo Mr. Blue ambaye wakati huo bado hakuwa na uelewa mkubwa wa maisha hadi kumtungia wimbo maarufu, ‘Roho Zinawauma’ ambao ulieleza mahusiano yao.

2. TID

Mwimbaji huyo aliwahi kukiri kipindi yupo na Wema Sepetu ndio wakati aliposhika fedha nyingi kupitia muziki, lakini Wema aliamua kumpiga chini na kumuumiza sana na kumfanya kuwa mtu mwingine kabisa kitabia.

Kuwa na Wema kulimfanya TID kuandikwa sana na magazeti ya udaku, kitu ambacho hakukipenda na kilimuumiza sana, ila ilimbidi akubaliane nacho kwa wakati huo. Alikuja kueleza machungu ya kutoswa na Wema katika wimbo wake, ‘Nilikataa’ akimshirikisha Mr. Blue na Q Chief.

3. Steven Kanumba

Mahusiano na Steven Kanumba ndiyo yaliyomfungulia milango Wema upande wa filamu, Kanumba ndiye alimuambia anaweza kuigiza na kumpa nafasi na mengine kuwa historia.

Kupitia App yake Februari 2020 Wema alidai katika mahusiano yao alitoa mimba mbili za Kanumba, kitu ambacho anajutia hadi leo na anaona imekuwa kama laana kwake kutokana na kutopata mtoto hadi sasa.

4. Diamond Platnumz

Walikutana kipindi ambacho Wema yupo na Chaz Baba, akiwa Marekani Wema akawa anachati Facebook na Diamond ambaye alikuwa anamfariji baada ya kupewa habari za Chaz Baba kumsaliti.

Aliporudi wakaanza kuishi pamoja, Wema akamfanya Diamond kuwa maarufu zaidi, akatokea kwenye video ya wimbo, ‘Moyo Wangu’ na kusafiri pamoja ndani na nje ya nchi alipokuwa na shoo msanii huyo.

5. Idris Sultan

Baada ya kushinda Big Brother Africa Hotshots 2014 na kuondoka na fedha kiasi cha Dola300,000, wastani wa Sh699.1 milioni kwa sasa, Idris Sultan alizama kwenye mahusiano na Wema.

Hata hivyo, mahusiano yao hakuchukua muda mrefu yakavunjika baada ya drama nyingi na yanatajwa kupukutisha sehemu ya fedha alizoshinda Idris katika jumba la Big Brother, alipochanga karata zake kwa takribani siku 60.

Ukiachana na hao, wanaume wengine maarufu waliowahi kuwa na Wema ni pamoja na Chaz Baba, Calisah na Luis Munana ambaye ni staa wa Big Brother Africa kutoka nchini Namibia. Na sasa ni zamu ya Whozu, Staa wa Bongofleva aliyepata umaarufu zaidi na wimbo wake, ‘Huendi Mbinguni’, huyu ametoka kuachana na mpenzi wake, Tunda ambaye wamejaliwa kupata mtoto mmoja wa kike.

Baada ya kilichotokea katika maadhimisho ya siku ya kuzaliwa Wema, yanayoendelea sasa ni kama yanajirudia kwa mrembo huyo kutawala mitandao ya kijamii kila anapofanya jambo. Bila shaka hakuna ubishi Wema ni mmoja tu.

Chanzo: Mwananchi