Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wema ndani ya tamthilia mpya kwenye Maisha Magic Bongo

00f3688dc29ac7e6104cc46a7163555e Wema ndani ya tamthilia mpya kwenye Maisha Magic Bongo

Thu, 30 Jul 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

*Tamthilia mpya kuanza kurindima mwezi Agosti, Wema ndani

SIKU chache tu baada ya wapenzi wa burudani hapa nchini kupata habari njema ya kurejea kwa chaneli za ESPN ndani ya DStv, upepo wa habari njema kwa wapenda burudani umeshika kasi ambapo Chaneli ya Maisha Magic Bongo (MMB) imetangaza kuzinduliwa kwa tamthilia mpya ya kukata na shoka iitwayo ‘KARMA’

Ndani ya tamthilia hiyo, Msanii Wema Sepetu ni miongoni mwa watakaoshuhudiwa miongoni mwa waigizaji mbalimbali ambao wameshiriki kwenye filamu hiyo ya aina yake iliyoandaliwa kwa viwango vya kimataifa.

Akizungumza kwenye uzinduzi wa filamu hiyo Wema amesema 'Karma' inaangazia zaidi kinadada wawili ambao wanakuwa wapinzani wa jadi – Suzanne na Veronica, ambao wote wanafanya kazi serikalini na wanaoheshimika sana kwenye jamii. Ndani ya tamthilia hiyo kuna visa na mikasa ya mahaba, siri nzito, siasa na visasi ambapo yeye mwenyewe Wema atakayeigiza kama Dr. Desire anajikuta katika vita vya kisiasa na Veronica katika mchuano wa uchaguzi mkuu ambampo visa vingi vitatokea na kuifanya tamthilia hiyo kuwa ya kusisimua.

Hivyo amewahakikishia wapenzi wa filamu kuwa tamthilia hiyo inaandaliwa kwa kiwango cha hali ya juu na kuwataka wasikose kuifuatilia kupitia chaneli ya MMB ambayo ni chaneli namba 160 ndani ya DStv Kila Jumamosi na Jumapili saa 3:00 usiku.

"Tamthilia hiyo iliyopikwa ikapikika na inayotarajiwa kupakuliwa rasmi kuanzia Agosti 1, 2020, inatarajiwa kuwa gumzo la jiji kwani imesheheni waigizaji nguli huku ikiwa na visa na mikasa kedekede ilimradi tu kuhakikisha kuwa mtazamaji wa MMB anapata burudani isiyo kifani punde tu anapoiangalia chaneli hiyo ndani ya Dstv pekee," amesema Wema.

Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania, Ronald Shelukindo amesema kitendo cha MMB kuzindua tamthilia hii mpya kinaendana na azma ya chaneli hiyo kuhakikisha kuwa watazamaji wake hawatindikiwi na burudani za kitanzania kwa kuzingatia kuwa tamthilia hii inazalishwa Tanzania na kuigizwa na wasanii wa Tanzania.

Awali, Mkuu wa chaneli ya MMB Barbara Kambogi alibainisha kuwa katika timu inayohusika katika uzalishaji wa tamthilia hiyo ni pamoja na Neema Ndepanya ambaye ni muandishi wa tamthilia maarufu ya SARAFU iliyokuwa ikirushwa kupitia MMB na ambayo ilijipatia umaarufu mkubwa. Amesema kuwa tamthilia hii mpya ya Karma ina waigizaji maarufu kama vile Wema Sepetu ambaye ameigiza katika filamu nyingi kwa umahiri mkubwa ikiwemo ile ya A point of no return iliyorushwa mwaka 2006 ambapo aliigiza kama Dina. Pia ameshiriki kuigiza katika filamu nyingi na hivyo kumfanya kuwa mtu sahihi kuongoza kwenye tamthilia ya Karma.

Wakati huo huo chaneli maarufu za michezo na burudani za ESPN zimeanza kurindima ndani ya DStv ambapo wadau mbalimbali wa michezo hususani wamchezo maarufu wa mpira wa kikapu wameelezwa kufurahishwa kwao na kurejea kwa chaneli hizo ndani ya DStv.

Chaneli za ESPN zinabeba michezo mingi maarufu Marekani kama vile ligi maarufu ya mpira wa kikapu NBAA, ligi ya mpira wa miguu NFL, ligi kuu ya Baseball MLB na nyinginezo. Chaneli hizo pia huonyesha Ligi ya Uingereza EFL, ligi ya Scotland SPFL bila kusahau ligi mbalimbali za Afrika Magharibi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Rais wa chama cha mpira wa kikapu Tanzania Phares Magesa amesema kuwepo kwa chaneli hizo ndani ya DStv ni faraja kubwa kwa wapenzi na mashabiki wa mchezo huo hapa nchini kwani sasa wataweza kufuatilia michuano maarufu kama NBAA mubashara kupitia DStv

Chanzo: habarileo.co.tz