Enhee… Katika filamu ya Point of no Return, msichana mrembo alionekana. Sauti laini na mvuto wa asili alivutia kumtazama. Na kubwa zaidi ilikuwa ni umahiri wake.
Japo ilikuwa ni filamu yake ya kwanza kabisa. Alionesha uwezo wa hali ya juu. Waliotazama ile filamu kwa mara ya kwanza, walijua sanaa imepata msanii mahiri. Muite Wema Sepetu.
Kuanzia hapo Wema hakutajwa tena kama Miss Tanzania. Akatajwa kama msanii mwenye mvuto. Baada ya filamu ile na nyingine kadhaa, kila kitu kikabadilika.
Katika sanaa kuna mabadiliko na kwa Wema kama Wema kuna mabadiliko. Hatajwi tena katika umahiri ule wa uigizaji. Hayupo tena kifilamu kama zamani. Japo bado anatamba na ‘taito’ ya uigizaji.
Labda hana mahaba na uigizaji kama zamani na kunyooshewa vidole kila alipopita. Hakuna anayeweza kupinga umahiri wake, ila ni uongo kusema anautendea haki. Ndiyo, ana nyota kali, ila watu wanahitaji kazi zake.
Leo wakitajwa wasanii wenye kufanya vizuri kuna watu watamtaja Wema. Sasa kwa kazi gani? Labda atasimama kupitia filamu za zamani. Kwa umahiri wake sanaa bado inamuhitaji.
Ni mmoja kati ya watoto wa kike wenye kuitendea haki uigizaji. Kama mkazo ukiwa wa kweli namuona Wema akitamba na kufanya makubwa katika filamu.
Ni kweli ana jina kubwa katika filamu ila halijajengwa kupitia filamu. Msingi wa jina lililojengwa kifilamu ulishaanguka kabla Kanumba hajafa. Au kabla Lulu na Kajala hawajaonja adha ya gereza.
Natamani kuona Wema akionesha umahiri wake kisanii kama nilivyowahi kumuona. Sijui itatokea lini? Ni mmoja wa waigizaji bora zaidi. Utake usitake!