Mwigizaji mkongwe Wema Sepetu amekiri kujuta jinsi alivyotumia pesa ambazo alizipata nyingi miaka ya nyuma kwa mambo ambayo hakufaa kuzitumia.
Sepetu akizungumza katika mahojiano ya kipekee na Haji Manara, alisema kwamba mpaka sasa hivi hamiliki gari aina ya Range Rover wala kumliki mjengo wa kifahari kutokana na makosa ya kifedha ambayo alifanya kipindi cha nyuma.
Sepetu aliweka wazi kwamba kipindi hicho alikuwa na karibia shilingi milioni 300 za Kitanzania lakini alishawishiwa kuingia katika siasa ili kugombea na baadae akapoteza kiti lakini pia na pesa zake katika kununua tikiti ya chama.
“Wakati ambao watu walikuwa wameniona kwamba nimeshika sana pesa, na kweli nilikuwa na hela si mchezo. Mimi niliingia kwenye siasa na nikagombea ubunge. Ilinirudisha sana nyuma. Watu wakisema kwamba leo hii matumizi yangu ndio yanafanya labda nisiendeshe Range, naweza nikasema hapana. Ni kwa sababu niliingia kwenye siasa,” Wema alikanusha dhana kwamba ana matumizi ghali ndio maana amefilisika.
“Ni kwa sababu niligombea na kule ndio mimi nilienda kutoa hela nyingi. Nilitoa mimi karibia milioni 320 na mimi kwenye akaunti yangu nilikuwa na milioni 280. Baada ya hapo nilijikuta nimerudi sifuri kabisa, ni kama nilicheza Kamari – niliingia nikidhani nitapata halafu sikupata,” Sepetu aliongeza.
Mrembo huyo alisema kuwa huo ndio ulikuwa mwanzo wa kimbunga katika maisha yake lakini hakuchukulia kama changamoto bali alijikung’uta na kujipunga vumbi na kuanza safari ya maisha upya tena.
Ikumbukwe mwaka jana Aristote aliibua mapya mitandaoni akisema kwamba Sepetu alikuwa maskini wa kutumia magari ya usafiri wa umma kwani hakuwa na gari lake binafsi kutokana na kufilisika.
"Naweza nikasema kwamba kupanda na kushuka kwangu katika maisha ndiko kumechangia sana kaitka umaarufu wangu," Sepetu alikiri.