Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wema Sepetu: Nilitamani kuwa mhudumu wa ndege,umaarufu ukanitibulia kila kitu

9365 Pic+wema TZW

Mon, 18 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wema Sepetu ni role model (mtu wa kupigiwa mfano) wa mabinti wengi nchini, lakini wasichofahamu kuwa hakutaka awe alivyo sasa.

Kama watoto wengine alikuwa akitamani kuwa mhudumu wa ndege, lakini umaarufu alioupata akiwa binti mdogo ulimpeleka katika ulimwengu mwingine kabisa. Umaarufu!

“Nilikuwa binti mwenye ndoto za kufanya kazi ya uhudumu wa ndege. Mbali na hiyo nilikuwa naagalia pia kila fani ambayo inanivutia kama urembo, uigizaji na muziki. Sijawahi kufikiria kabisa kama nitakuwa staa kama hivi,” anasema Wema.

Kitu gani kilichobadili maisha yako?

“Baada ya kuwa Miss Tanzania maana nilipata taji nikiwa na umri mdogo, nilikuwa kila kitu nachukulia poa tu niliona ustaa freshi tu, hivyo nilikuwa nafanya vitu bila kuhofia kuwa ni kibaya. Waliokuwa wanafuatilia maisha yangu ndio walizidi kuyabadili kwa kuwa kila sehemu nayoingia nakuwa naangaliwa.”

Kuna wakati wowote uliwahi kujutia maisha ya ustaa baada ya kuwa Miss Tanzania?

“Yes, nimewahi kujuta lakini mwisho wa siku huwa nasema Mwenyezi Mungu ndiye anapanga kwa sababu nisingefika hapa kwanza. Kwa hiyo kujutia kunatokea kwa kila mtu,” anasema.

Vipi kuhusu matibabu India?

Siku chache baada ya kurudi kutoka India kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji mdogo, Wema Sepetu ameliambia Mwananchi kuwa anaendelea vizuri japo maumivu yapo madogomadogo.

Akipiga stori mbili tatu na gazeti la hili, japo hakuwa tayari kufungukia ugonjwa uliompeleka India, anasema anaendelea vizuri kiasi.

Hata hivyo meneja wake, Martin Kadinda aliwahi kuliambia gazeti hili kwa kifupi kuwa ugonjwa wa Wema unahusiana na ‘masuala ya wanawake’.

Mwandishi alipombana kuhusu ugonjwa huo, Kadinda alimjibu: “Magonjwa yenu wanawake si unayajua,” huku akimsisitiza kuongelea uzinduzi wa filamu ya mrembo huyo utakaofanyika Juni 30, mwaka huu.

Ni kweli umekimbia kesi?

Kuna madai kuwa hakusafiri kwenda India, bali ilikuwa mbinu ya kutohudhuria kesi yake inayomkabili.

“Hapana siwezi kukimbia kesi, mimi nimeanza kuumwa kabla hata ya kesi jamani na kwa nini nikimbie wakati nataka, naomba iishe hata kesho. Sasa nisipohudhuria kwa makusudi si muda utazidi kuongezeka wa kuisha,” anasema.

Kukubali kutumika na WCB

“Nasikia tu watu wanasema hivyo, ila naweza sema ni kweli ila katika kazi na kazi hiyo huwa anapata malipo, tofauti na watu wanavyodhani kutumika kwa mapenzi au kiki zisizokuwa na faida na ndio maana niliwaambia Diamond nipo naye kikazi tu na sio mapenzi. Watu waache na ushabiki wa mitandao hauna maana.”

Wema anasema pindi alipoachana na Diamond walikaa muda mrefu bila kupeana salamu, lakini walikaa chini na kumaliza tofauti zao na wakakubaliana wawe wanafanya kazi.

Kitu gani ambacho hukipendi?

“Kitu ambacho sikipendi kwanza kuambiwa mimi nina uhusiano wa kimapenzi na Diamond wakati nilishaachana naye na kwa sasa ukaribu wetu ni wa kikazi.

“Pili watu wa mitandaoni kuunganisha matukio na kufanya kuwa ya kuyaongelea vibaya, huwa nachukia sana mambo machafu ya mitandaoni,” anasema Wema.

Chanzo: mwananchi.co.tz