WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewapa tano wasanii mbalimbali wa muziki nchini kwa kuifanya nchi kuwa tulivu kutokana na nyimbo walizotunga za maombolezo za kuwafariji Watanzania.
Majaliwa alisema hayo jana kwenye mazishi ya Rais wa Awamu wa Tano, Dk John Magufuli aliyezikwa Chato, mkoani Geita.
“Hatutawasahau wasanii waliotunga nyimbo mbalimbali za kuwafariji Watanzania, utulivu tulioupata umetokana na mchango mkubwa wa nyimbo zao,” alisema.
Alisema wasanii wa muziki wa kizazi kipya, jazz, kwaya na dufu wameonesha mshikamano na mchango mkubwa kwa kutunga nyimbo za kuwatuliza Watanzania. Majaliwa aliwahimiza wasanii hao kuendelea na mshikamano huo katika kudumisha umoja na amani.
Waziri huyo kila alipopata nafasi hakuacha kutoa shukrani kwa makundi mbalimbali wakiwemo wasanii akionesha kuthamini mchango wao.
Baadhi ya wasanii waliokuwepo Chato jana wakati wa mazishi ya Dk Magufuli ni pamoja na Nassibu Abdul au Diamond, Abdul Rajabu au Harmonize, Meja Kunta, Geoge G Nako, Khadija Kopa, Kajala Masanja, Faustina Charles, Mrisho Mpoto au Mjomba, Jux na Marioo