Wakati Serikali ikiendelea kutafuta mwarobaini wa matumizi ya vilevi kwa watoto, inaelezwa kuwa watoto wamebuni mbinu mpya ya kutumia saa za mkononi na 'Lipstick' kuvuta na kutumia kilevi aina ya shisha.
Biashara ya uuzaji wa shisha ambayo inahusishwa na madawa ya kulevya inadaiwa kuanza nchini mwaka 2016 huku baadhi ya viongozi wa Serikali kati ya mwaka 2016 na 2017 wakikaririwa kupiga marufuku matumizi ya kilevi hicho ili kuokoa nguvu kazi ya taifa.
Pamoja na viongozi kupiga marufuku lakini shisha imeonekana kuwa mwiba mgumu kutafuna baada ya watumiaji wake kubuni mbinu na njia mbalimbali za kutumia kilevi hicho hata kwenye maeneo ya umma bila kutambulika.
Akizungumza leo Ijumaa Novemba 25, 2022 kwenye Maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Mkoa wa Mwanza, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika lisilo la Kiserikali la Kutetea Haki za Wanawake na Watoto la Kivulini, Yassin Ally amesema uchunguzi waliyoufanya umebaini matumizi ya saa na 'lipstick' kwenye uvutaji wa shisha.
"Ukiona mtoto unaona amevaa saa kumbe ni kifaa cha kuhifadhia shisha, pia zimeingia 'Lipstick' na zenyewe ni hivi hivi ukiona mtoto anayo unajua ni urembo kumbe ni kifaa cha kuhifadhia shisha au ndiyo shisha yenyewe, hili nalisema kwa sababu watoto wanatuonyesha wenyewe," amesema Ally.
Mbali na matumizi ya shisha kwa watoto chini ya miaka 17 nchini, Ally amesema wamebaini kundi hilo hasa watoto wa kike wanavuta ugoro huku akisema baadhi yao huchanganya na pombe ili kulewa kwa haraka.
"Watoto wanavuta ugoro kuzidi bibi kizee, wanaziita Zanzibar na Mombasa, ikiwa imechanganywa na pombe ya Santiana wanaiita, Zanzibar na Kvant wanaiita Mombasa. Wengine wanahifadhi ugoro kwenye kasha za dawa za malaria," amesema.
"Watoto wetu tuwachunguze wanakunywa pombe wakiwa sebuleni, ukimuuliza anasema anakunywa kinywaji kumbe ni pombe. Tuwachunguze kwa karibu ili kuwaepusha na madhara ya matumizi ya vileo," amesema.
Akitumia neno la Mungu kutoka Kitabu cha Wakoritho sura ya kwanza 5:23, Mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Amani Mkoa wa Mwanza, Askofu Charles Sekelwa amesema mwili wa mwanadamu umeumbwa na mifumo mitatu yaani roho, nafsi na mwili hivyo ili kukomesha uovu huo binadamu anahitaji zaidi msaada wa kiroho.
"Wangapi tumeshuhudia mwizi anaiba anakamatwa anauawawa kesho anatokea mwingine anaiba. Mungu atusaidie kwa njia ya mafundisho, kukemea na kuomba tutokomeze uovu huu unaoikumba nchi yetu," amesema Askofu Sekelwa.
Naye, Mchungaji Mutash amewaasa wazazi akisema mmonyoko wa maadili kwa watoto na jamii unachangiwa kwa kiasi kikubwa na wazazi huku akiwataka kutimiza wajibu wao.
"Wazazi tukubali kulaumiwa tunahusika hapa," amesema Mutash.
Maadhimisho hayo yamefanyika leo katika Ukumbi wa Mwanza Hotel na kuhudhuriwa na mamia ya viongozi wa dini, siasa, wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wakiwemo Shirika la Kutetea Haki za Wafanyakazi wa Ndani la Wotesawa pamoja na wakazi wa mkoa huo.