Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Watoto wa Iringa walivyowashangaza mastaa tuzo za SZIFF

43587 Pic+filamu Watoto wa Iringa walivyowashangaza mastaa tuzo za SZIFF

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Katika hali ya kushangaza watoto kutoka mkoani iringa wamewabwaga mastaa wakubwa katika tuzo za filamu za Sinema Zetu International Film Festival (SZIFF 2019) wakiwamo Monalisa, Wema Sepetu, Johari, Gabo na Hemed Suleiman.

Watoto hao Flora Kihombo (11) na Rashid Msigala (10), wanaolelewa na kituo cha watoto wanaotoka katika mazingira magumu cha TAG Lwanga Student, waliibuka kidedea kupitia filamu yao ya ‘Kesho’.

Filamu hiyo inaelezea watoto wanaoishi katika mazingira magumu baada ya baba yao kuwatelekeza, lakini katika harakati za kusaka maisha wakafanikiwa.

Kilele cha tuzo hizo kilifanyika usiku wa kuamkia jana katika ukumbi wa Mlimani City na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson, Waziri wa Habari, Dk Harrison Mwakyembe, Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Zanzibar, Balozi Ali Karume, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Joyce Fisoo. Mgeni wa kimataifa alikuwa Shahazadi Mustafa, mmoja wa waigizaji anayewavutia wengi katika tamthiliya ya Sultan inayorushwa kupitia Azam Two.

Katika kilele hicho matokeo yalionekana kuwashangaza wengi na kutoamini kilichotokea, baada ya washindani ambao hawakupewa nafasi kubwa kuwagalagaza wale maarufu waliokuwa wakitabiriwa kubeba tuzo hizo kutokana na ushawishi wao kwenye jamii.

Vipengele vilivyokuwa vikitazamwa zaidi ni vya msanii bora wa kike, msanii bora wa kiume na filamu bora ambavyo ndivyo hasa vilitegemea kura za watazamaji.

Katika kipengele cha msanii bora wa kike, Flora alishindanishwa na wasanii wengine tisa akiwamo Blandina Chagula ‘Johari’, Ivyonne Cherry ‘Monalisa’ na Wema Sepetu.

Wengine ni Jennifer Temu, Zaudia Rajabu, Sifa Matanga, Asha Mussa, Rhoida Richard na Sasha Sebastian.

Wakati kwa upande wa msanii bora wa kiume, Rashid Msigala alitangazwa mshindi baada ya kuwashinda wasanii maarufu akiwamo Hemed Suleim na Salum Ahmed ‘Gabo’ ambaye mwaka jana alitwaa tuzo hiyo.

Wengine waliokuwapo katika kipengele hiki ni Maulid Ali (Mau), Peter Paul, Mack Daim, Sango Johanes, Salum Mpoyoka, Hassan Kazoa na Madebe Lidai ambaye alitangazwa kuwa mchekeshaji bora katika tuzo hizo.

Johari, Wema Gabo wazungumza

Baadhi ya wateule ambao hawakubahatika kushinda akiwamo Johari, katika maoni yake anasema kilichofanywa kwa wasanii wakongwe kuwekwa kundi moja na watoto sio sahihi na kusema endapo waandaaji waliamua kuwapa tuzo hizo watoto ili kuwapa moyo ingeelezwa bayana.

Johari anasema kilichofanyika kinaweza kuua tasnia, kwani hata wawekezaji wataona nchi haina wasanii imara.

Naye Wema Sepetu anakiri kuumizwa nafsi kwa kukosa tuzo, lakini anachoshukuru ni kwamba watu wanajua kwamba anajua na kwamba huenda ni wakati wa watoto nao kupewa nafasi.

Kwa upande wake Gabo ambaye filamu yake ya ‘Siyabonga’ ilitwaa tuzo mbili ikiwamo ya filamu bora na filamu yenye maudhui ya kitaifa, hakuwa na maneno mengi zaidi ya kusema anashukuru kwa madai kuwa kauli hiyo inaonyesha uungwana uliotukuka mbele za watu.

Tuzo za mwaka huu zimeonekana kuzua gumzo katika mitandao ya kijamii na kati ya watu wa mwanzo kutoa maoni ni msanii Jacline Wolper, ambaye anasema ana filamu tisa zipo ndani lakini kutokana na gharama alizotumia kuziandaa zitaendelea kukaa kabatini mpaka watakapokuja watu wenye uchungu na tasnia hiyo.

Wolper anasema kama itashindikana kuziuza watakuja kuziangalia wajukuu wake huku akilalamika kuwa katika tasnia hiyo kama huwaendekezi waandaaji wa tuzo wanapokuita ndio umekwenda na maji.

Steve Nyerere, anasema kuwa kwa siku nzima ya juzi kila msanii aliyempigia simu alikuwa saluni akijiandaa kupokea tuzo na kuhoji “ni kweli Johari, Monalisa, Gabo ni watu wa kukosa kura”.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Waigizaji, Elia Mjata, anasema ushindi wa watoto hao umefungua fursa ya kuzalisha vipaji vipya vyenye umri mdogo.

Jaji kiongozi afunguka

Rais wa jopo la majaji wa SZIFF, Martin Mhando, anasema anajua matokeo hayawezi kumridhisha kila mmoja kwani hata mwaka jana licha ya wasanii wakubwa kushinda lakini kulikuwa na malalamiko.

Badala yake Martin anawashauri Watanzania kuitazama filamu iliyotoa washindi na kuangalia uwezo ulioonyeshwa na washindi.

Tuzo zilivyofanyika

Tamasha la tuzo hizo lilianza rasmi saa 2.00 usiku na kumalizika saa saba ambapo viongozi mbalimbali walipata fursa ya kuzungumza akiwamo Waziri Mwakyembe ambaye wizara yake pia inahusika na sanaa na utamaduni, ambaye anasema ni kitu kizuri kuona ndoto ya wazo la tamasha la kimataifa la sinema za kiswahili walilokuja nalo Azam inatimia.

“Maswali tuliyokuwa tunajiuliza wakati kina Tido Mhando wanatuletea wazo la kuanzisha tuzo hizi ni kwamba kuna filamu zenye ubora wa kukubalika ndani na nje ya nchi, lakini nashukuru leo mnatueleza filamu zimeongezeka kutoka 300 zilizoletwa mwaka jana hadi 500, ni jambo la kupongezwa.

Naye Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia, anasema kufanyika kwa tamasha hilo, ni fursa kwa wadau wa sanaa zingine kuchukua hatua.

Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu, Joyce Fisoo, anasema SZIFF inatoa fursa ya kuwajenga wasanii na kwenda kwenye anga za kimataifa.

Fisoo anasema cha kujivunia zaidi ni kwamba sasa Tanzania ni ya pili kuzalisha filamu Afrika na asilimia 80 ya nchi hizo wananunua kazi za hapa nchini, hivyo anashauri sekta ya filamu kuangaliwa kwa upana zaidi.

Awali Mratibu wa SZIFF, Sofia Mgaza, alisema tamasha hilo walilianzisha kwa ajili ya kuongeza thamani ya filamu za Tanzania. Sofia anasema tamasha hilo pia linatumika kama jukwaa la kuwaweka karibu wadau wote wa filamu.



Chanzo: mwananchi.co.tz