Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

'Wataka mashauri ndoa, talaka, miradhi yaanzishiwe divisheni yake '

99aea170c4c544ddd6e52e11ce2210fb.jpeg 'Wataka mashauri ndoa, talaka, miradhi yaanzishiwe divisheni yake '

Fri, 5 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SERIKALI imeshauriwa kuanzisha divisheni ya familia ambayo itashugulikia mashauri ya ndoa, talaka na mirathi ili kuwaondolea wananchi adha wanayopata kwa mashauri yao kuchelewa katika mfumo wa kawaida wa mahakama.

Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Mkoa wa Kigoma, Zainab Katimba wakati akiuliza swali la nyongeza lililotokana na swali la msingi lililohoji Mpango wa Serikali wa kubadili sheria kandamizi ili ziendane na wakati?

Katimba amehoji kama ambavyo serikali ilivyoanzisha mahakama ya rushwa na mahakama ya ardhi, je haioni kuna umuhimu wa kuwa na mahakama ya familia, kwani kucheleweshwa kwa mashauri ya familia kwenye mfumo wa kawaida wa mahakama ni sawa na kuwanyima wahusika haki yao.

Akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda amesema ushauri huo ni mzuri na kwamba ataufikisha katika mamlaka mbalimbali zinazohusika ili uweze kufanyiwa kazi.

Hoja ya Katimba imekuja ikiwa ni siku chache baada ya Msajili wa ndoa na talaka kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Jane Barongo kutoa takwimu mwaka 2020, zinaonyesha kuwa talaka 511 zilisajiliwa Tanzania nzima kati ya hizo 221 kutoka Dar es Salaam pekee. Idadi hiyo ni ongezeko la talaka 69 ikilinganishwa na talaka 442 zilizosajiliwa mwaka 2019.

Pia Utafiti wa kufuatilia kaya Tanzania, wa mwaka 2014/15 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) unaonyesha kuwa kiwango cha talaka kiliongezeka kwa asilimia 1.1

Hii ina maana kuwa kwa kila watu 100 wenye umri wa kuoa au kuolewa waliopo Tanzania, wawili wametalakiwa kutoka mmoja mwaka 2008/09.

Chanzo: habarileo.co.tz