Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasanii watuma ujumbe mzito kwa Magufuli

Ffbfd0e124ad8361dbb6658782dc5b87.jpeg Wasanii watuma ujumbe mzito kwa Magufuli

Sat, 27 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WASANII mbalimbali wa muziki wa kizazi kipya wameandika ujumbe mzito kumuaga Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli aliyemaliza safari yake ya maisha hapa duniani baada ya kuzikwa huko Chato, mkoani Geita jana.

Kupitia mitandao yao ya kijamii, wasanii Khaled Mohamed ‘TID’, Hamis Mwinjuma ‘FA’ na Abdulaziz Chande ‘Dogo Janja’ waliandika ujumbe mfupi jana wa kumuaga kiongozi huyo na kueleza masikitiko yao.

Kwa upande wa TID, alisema anaomba msamaha kwa kushindwa kufika Chato na kumzika kiongozi huyo.

“Hakika Ijumaa ya leo (jana) itabaki kwenye kichwa changu. Maneno peke yake hayatoshi, naomba Allah akusamehe dhambi zako. Pia, uko uliko nisamehe kwa kushindwa kufika mazikoni Chato,” alisema.

Kwa upande wake, Mwana Fa alisema kifo hakikwepeki na kwamba mwanadamu akitekeleza wajibu wake kwake na kwa watu wake anafikwa na kifo akiwa na amani.

“Naamini Mzee wangu John ‘Walwa’ Joseph Magufuli ametekeleza wajibu wake duniani ipasavyo na anakwenda akiwa amemaliza kazi iliyomleta,” alisema na kuongeza: “Anakwenda akiwa na amani moyoni mwake.”

Mwana Fa ambaye ni Mbunge wa Muheza alisema wanahuzunika kwa mapenzi waliyonayo kwa kiongozi wao huyo ila anaamini Mungu anajua kwanini yametokea.

“Tunakusindikiza ukapumzike kwa amani Baba,” alisema.

Naye Dogo Janja alisema "Leo (jana) ni siku ngumu sana kwa taifa letu la Tanzania, wananchi wako tulikupenda sana lakini Mungu amekupenda zaidi, Allah akupe kauli thabiti pumzika kwa amani baba."

Chanzo: www.habarileo.co.tz