Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasanii waomba 'baraka' kwenye makaburi

Wasanii waomba 'baraka' kwenye makaburi

Thu, 19 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Bagamoyo. Maji yanayodaiwa kuondoa  mikosi, kaburi linalotoa baraka na mti unaodaiwa kurefusha maisha ni miongoni mwa vivutio vitatu vya utalii vilivyotumia muda mrefu katika ziara ya wasanii wa Bongo Fleva na filamu kuvitembelea na kuomba 'baraka' maeneo hayo katika mji wa Kaole, Bagamoyo mkoani Pwani.

Wasanii hao ambao wako katika ziara ya kutangaza vivutio vilivyopo chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), wametumia takriban saa nne kupata maelezo kutoka kwa wahifadhi wa maeneo hayo na kisha kuomba 'baraka'.

Katika ziara hiyo ambayo wanaongozwa na mjumbe wa Baraza la Sanaa Tanzania (Basata), Single Mtambalike ambaye pia ni nguli wa filamu, walianza kwa kupokea maelezo ya namna vivutio hivyo vilivyo kisha wakaanza kutekeleza maelekezo.

Muongoza watalii wa TFS, Steven Japhet amewaambia wasanii hao ambao ni mabalozi wa utalii kuwa vivutio hivyo ambavyo vimekuwapo kwa takriban miaka 800 vimekuwa vikitumiwa na wenyeji pamoja na wageni kuomba 'baraka' za mafanikio, kuwaondolea nuksi na mikosi maishani na kuwaongezea maisha au kuwapunguzia wanaotaka kufanyiwa hivyo.

"Kwa mfano katika ule mti wa mbuyu wenye umri wa miaka zaidi ya 500 ukiuzunguka kwenda kulia unaongeza maisha yako na ukiuzunguka kwenda kushoto yanapungua. Sasa itategemea unataka nini," amesema Japhet.

"Pia wale ambao mathalan mtu anataka mke ama mume au amani katika ndoa yake kuna kaburi la wanandoa waliozikwa pamoja ambalo linabariki sana."

Baada ya maelezo hayo wasanii walianza kufanya kama walivyoelezwa, ambapo Kulwa Kikumba 'Dude' amewaongoza kunawa maji ya kisima cha baraka huku wakichota mengine na kuondoka nayo.

Naye Jacob Steven 'JB' amewaongoza wale waliokwenda kuzunguka mti wa mbuyu huku Mtambalike akiomba baraka kwenye kaburi la kharifa, binti wa miaka 14 anayedaiwa kufa zaidi ya miaka 800 iliyopita.

"Nimeomba baraka hapa, " amesema Mtambalike.

Meneja wa Kanda ya Mashariki wa TFS, Caroline Malundo amewataka wasanii kuwa mabalozi wema wa vivutio hivyo vya utalii akisema, " hatua hii itasaidia kuvutia watalii na kufanya Watanzania kujua rasilimali zao vizuri."

Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainab Kawawa amesema Serikali imedhamiria kwa dhati kuwafanya wananchi wapende kutembelea vivutio vya utalii kwa kuwa ni haki yao.

"Nawaomba sana wasanii wetu mtusaidie kufanikisha hili maana nchi hii ni yetu sote," amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz