Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasanii wamuaga  Magufuli

434f2d1e113c4a37d5bf66d72ca88cd9 Wasanii wamuaga  Magufuli

Mon, 22 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

NYOTA mbalimbali wa muziki nchini walijitokeza jana kwenye Uwanja wa Uhuru kumuaga Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.

Magufuli aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu alikuwa kipenzi cha wasanii baada ya kufanya nao kazi katika shughuli mbalimbali, ikiwemo kampeni za uchaguzi na baadhi yao aliwavisha kofia kama ishara ya kukubali kazi zao.

Miongoni mwa nyota waliokuwemo kumuaga ni Mrisho Mpoto, Nassibu Abdul ‘Diamond Plutnumz’, Rajabu Abdul ‘Harmonize’, Omar Nyembo ‘Ommy Dimpoz’ na wengine kadhaa ambao pia, baadhi yao walipata nafasi ya kuimba nyimbo za maombolezo walizotunga kwa ajili ya kumuenzi.

Enzi za uhai wake, Rais Magufuli aliahidi kushughulikia matatizo ya wasanii hasa baada ya kugundua kuwa hawanufaiki na kazi zao ipasavyo.

Ili kutimiza kile alichoahidi kuwasaidia wasanii alikitoa Chombo kinachoshughulikia Hatimiliki Tanzania (Cosota) kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara na kuipeleka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Hiyo ni baada ya wasanii kudai kuwa nyimbo zao zinatumika sehemu mbalimbali, lakini hawanufaiki na chochote.

Magufuli aliwapongeza wasanii kwa kuwa sanaa yao imekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi na pia, kwa jitihada za kutangaza muziki wao nje ya nchi.

Magufuli aliwahi kuwaahidi kuwa serikali itakuza sanaa hiyo na kuhakikisha inaimarisha mfuko wa utamaduni na sanaa ili kuwasaidia wasanii ikiwemo kupata mafunzo na mikopo.

Alisema hiyo yote ni kwasababu sekta hiyo inakuwa kwa kasi na imeajiri vijana wengi, ni muhimu kwa kuwa inachangia maendeleo ya taifa katika uchumi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz