Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wasanii wa Bongofleva mmejipangaje kuwa wanamuziki?

36351 Julie+kulangwa Wasanii wa Bongofleva mmejipangaje kuwa wanamuziki?

Sat, 12 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Inasemekana kuwa muziki wa Bongofleva umekuwa na kufanikiwa kuvuka nyanja za kimataifa. Sina shaka na hilo inawezekana umekuwa na kufanikiwa kutoa ajira kwa vijana waliojitoa kwa dhati kuufanya.

Mbali ya ajira ya msanii mmoja mmoja, lakini kupitia kazi zao ikiwamo shoo, mavazi, safari wanazofanya kwenye mikoa mbalimbali wamekuwa wakizalisha ajira za muda mfupi na mrefu huku wakikuza biashara kwa wanaouza bidhaa zinazoendana na wanachokifanya.

Lakini je, wasanii wa muziki wa kizazi kipya wanajua maana halisi ya muziki? Hili ndilo swali la kwanza analopaswa kujiuliza msanii yeyote kabla ya kuingia mzima mzima kwenye tasnia hiyo inayopendwa na watu wengi duniani.

Kama hujajua maana ya muziki bila shaka huwezi kuwa mwanamuziki, hivyo unapaswa ufahamu maana yake ili unapoingia usikiuke mipaka na matakwa halisi ya fani hiyo.

Wapo wasanii wa muziki wa kizazi kipya wanaokwenda mbali na kujiita wanamuziki, bila kujua maana halisi ya muziki.

Mwanamuziki halisi ni yule anayeimba na kupiga vyombo, tofauti na hapo anakuwa hajakamilika na anadhihaki vyeo vya kina Ridhiwani Pangamawe, Hamza Kalala, Jhiko Man, Romario Mg’ande, Zahiri Zoro na wengine ambao wamekuwa wanaimba na kupiga vyombo.

Muziki siyo kutunga pekee ni pamoja na kujua angalau baadhi ya vyombo, hapo unaweza kutoka kifua mbele ukijisifu kuwa wewe ni mwanamuziki.

Wapo wasanii wa muziki wa kizazi kipya wanaojua kutunga na kuimba wakiwa studio, wakitoka nje ya studio hawawezi chochote kwa sababu hawajui kucheza vyombo vya muziki.

Ni ajabu msanii yupo kwenye tasnia ya muziki kwa miaka zaidi ya mitano hajui kupiga angalau gitaa, tarumbeta, ngoma, kinanda, manyanga.

Wasanii wa kizazi kipya jibidiisheni kujua vyombo vya muziki, hata kama teknolojia imekuwa na inarahisisha kazi, zipo baadhi hazina budi kubaki kwenye asili yake.

Inawezekana tunalalamika kupotea ladha ya muziki wa Tanzania kutokana na wasanii kuiga wa kutoka Afrika Magharibi, kumbe inatokana na watayarishaji kuona midundo ya huko ni rahisi kuchanganya na sauti zenu zinazohitaji mabadiliko ya kompyuta.

Mngejua kupiga vyombo bila shaka mngepanua wigo wa fursa, kuna wanamuziki licha ya kuwa watu wazima bado wanapiga muziki wao kwenye mahoteli makubwa kwa sababu wanajua kutoa burudani.

mekubali kutafuniwa kila kitu na umeme, hadi sauti zenu hamsumbuki tena, kwa sababu zitarekebishwa na mitambo.

Kinyaa zaidi huwa kinatokea msanii anayeitwa mkubwa anaposhindwa kuimba mubashara (live) jukwaani.

Hii ni aibu na ndiyo maana hakuna msanii wa Bongofleva anayefanya maajabu kwenye matamasha makubwa kama la Sauti za Busara kwa sababu ataimba lakini atapata taabu sana.

Kama mmeamua kuendelea kuwa wasanii sawa! Lakini kama mnataka kuwa wanamuziki mnahitaji kufanya kitu za ziada.



Chanzo: mwananchi.co.tz