Mapenzi ukiyapatia yana raha yake kama anavyoimba msanii wa Bongofleva aitwaye Kusah akishirikiana na Maua Sama unaokwenda kwa jina la Wenyewe, kama haitoshi kuna wanandoa wanaofanya fani moja, wanafurahia kupata wenzao wao.
Mwanaspoti limekukusanyia watu maarufu ambao wanafanya fani moja, huku, asilimia kubwa wanafurahia kupata wenza wa aina hiyo, kwani kuna muda ambao wanashauriana jinsi ya kuhakikisha kazi zao zinakuwa bora zaidi.
BILLNASS/NANDY
Wanandoa wa Bongo Fleva, William Nicholaus 'Billnass' na Faustina Mfinanga 'Nandy' wanafanya kazi moja ya muziki na kuna nyimbo ambazo wameimba kwa pamoja zinazoonyesha jinsi huba lao lilivyo nzito.
Nyimbo zao zilipata umarufu mkubwa kwenye mitandao ya kijamii ambazo ni Bugana na Bey ambayo waliimba siku ya harusi yao ambayo ilifanyika kwa ukubwa ikihudhuriwa na mastaa mbalimbali nchini.
Nandy anafurahia uwepo wa mumewe (Billnas) akimsifia ni mtu anayeisimamia familia yake kufurahia maisha "Ni mume bora na baba mzuri kwa mtoto wetu, kiukweli nimepata rafiki anayenishauri vitu vingi kwenye kazi yangu."
KESSY/ MWALALA
Straika wa Simba Queens, Asha Rashid 'Mwalala' anasimulia alivyokutana na mume wake Hassan Kessy miaka 11 iliyopita kwa mara ya kwanza ilikuwa Uwanja wa Karume ambako timu yao ya Mburahati Queens ilikuwa inafanya mazoezi.
"Hassan alikuwa kwenye kituo cha soka cha TFF (TSA), baada ya kunifuata nilimsumbua sana hadi kumkubalia, tumekaa kwenye uchumba miaka 10 hadi nimeoana na tumefanikiwa kupata mtoto wa kike, ni mume anayejali familia yake, anajali karia yangu huwa ananipa sana moyo wa kupambana," anasema na kuongeza;
"Wakati nimetoka kujifungua yapo mazoezi ambayo alikuwa ananielekeza, kubwa zaidi ananiambia mtazamo wangu kwenye kazi ndio utakaonifanya thamani yangu iwe juu, hapendi nikate tamaa, pia nje tunashabikia timu tofauti Barcelona F.C na mume wangu anashabikia Real Madrid."
MABRUK /KHANIPHA
Kipa wa zamani wa Uzuri Queens, Mburati Queens na Twiga Stars, Khanifa Idd alikutana na mume wake Mustapha Mabruk katika shule ya Makongo na ndiye alikuwa anamfundisha kucheza nafasi ya kipa wakati huo hawakuwahi kuwa na mawazo ya kimapenzi.
Anasema baada ya wawili hao kumaliza shule ya sekondari, kila mmoja alikuwa na mpenzi wake ambayo yakawashinda wakaja kukutana 2016 ambapo walianzisha uhusiano hadi kufunga ndoa na sasa wamepata mtoto.
"Huko tulikotoka kwenye mapenzi ya awali kila mmoja alijaliwa kupata mtoto mmoja mmoja na sasa tumepata wa pamoja, tunapendana na kusaidiana kazi, ingawa mume wangu kwa sasa alikwenda kusomea kozi na kwa sasa ni mwanajeshi," anasema na kuongeza;
"Kuna raha yake kufanya kazi moja, kwani kuna wakati akiona nataka kuzembea kuwa na mwili ambao haueleweki tunatengeneza programu ya pamoja kuhakikisha nakuwa vile nataka."
JABIRI/NAIMA
Straika wa Kagera Sugar, Anuary Jabir anasema miaka mitatu nyuma wakati yupo Dodoma Jiji alikutana na mkewe anayejulikana kwa jina la Naima ambaye ni mchezaji wa netiboli wa timu ya Jiji ambayo kwa sasa iko daraja la pili.
Anasimulia namna ilivyoanza safari yao ya mapenzi "Kuna siku uwanja ambao tulikuwa tunafanyia mazoezi pembeni kulikuwa na timu ya netiboli ya Jiji la Dodoma kipindi hicho ilikuwa Ligi Daraja la Kwanza, huku na kule nikapiga jicho nikamuona, nikajikuta navutiwa naye ghafla.
"Baada ya kurejea kambini niliomba Mungu nikutane naye tena, siku iliyofuata tukaenda mazoezini tena, nilipomuona sikutaka kuichezea bahati nikamfuata kumuomba namba pale ndipo mahusiano yalipoanzia."
Anasema japokuwa mkewe anacheza netiboli, anapokuwa mapumzikoni wanafanya mazoezi kwa pamoja na kushauriana jinsi ya kufanya kazi kwa viwango vya juu "Kufanya kazi zinazoendana kuna raha yake ingawa kila mtu ana sehemu yake."
RICH/WOLPER
Japokuwa Rich Mitindo mume wa msanii wa Bongo Move, Jacqueline Wolper siyo msanii ila wanafanya kazi moja ya ubunifu wa nguo wanazowavalisha watu mbalimbali.
Kuna wakati Wolper aliwahi kukiri kwamba inapofikia wakati wa biashara zao za kufanya mitindo wanashauriana ili kufanya vitu bora ambavyo vipo kwenye mtindo wa kusasa zaidi.
GUMBO/KISIGA
Hapa kuna wanandoa wengine ambao wote ni wachezaji kuna beki wa JKT Tanzania, Mani Gumbo na mkewe alikuwa beki wa Emima Queens, Maua Kisiga ambapo wawili hao wamepata mtoto wa kike mwenye miaka minne na mwanaume ambaye kwa sasa ni mwanajeshi.
MPAKALA/REHEMA
Aliyekuwa beki wa Emima Queens ambayo makao yake yalikuwa Buguruni, Rehema Chuka naye kaolewa na mchezaji wa zamani wa Biashara United, Juma Mpakala 'Kidishi' ambaye anasubiri dili kwenye kipindi hiki cha usajili kupata timu.
WENGINE Marlow na Besta waliwahi kufunika kwenye fani ya muziki wa kizazi kipya kabla ya kufunga ndoa Machi, 2011 kisha kila mmoja kupotezea fani hiyo wakipiga mishemishe nyingine kwa sasa.
Pia kuwa waigizaji wakali wa filamu Ahmed Khalfan ‘Kelvin’ na Elizabeth (sasa Fathia) Chijumba a.k.a Nikita nao walioana wakiwa watu wa fani moja na mambo kwao ni bambamu.
Kuna Nahreel na Aika wanaounda kundi la Navy Kenzo nao ni wapenzi na wote wanafanya kazi ya fani moja wote wakiwa wasanii wa muziki wa kizazi kipya wanaokimbiza nchini na Afrika kwa ujumla, ilihali huko majuu kuna wana kibao walioana au kuwa wapenzi wakifanya fani moja akiwamo Jay Z na Beyonce Wakali hao wa dunia Shawn Corey Carter 'Jay -Z' anayeimba Hip hop na mkewe Beyonce Giselle Knowles 'Beyonce' (RnB, Pop) , wawili hao walifunga ndoa yao Aprili 4, 2008 hivyo kuleta mfano kwa wasanii ambao hawadumu kwenye pingu za maisha.
Hivi karibuni wamesherehekea miaka 15 tangu kufunga ndoa yao ambapo wamepata watoto watatu ambao ni Blue Ivy na mapacha, Rumi na Sir ambapo mara nyingi wamekuwa wakionekana pamoja kwenye shoo mbalimbali.
Moja ya nyimbo zao kali zinazopenda na vijana ambao wameimba pamoja ukihusisha uhusiano wao ni ule wa 'Forever Young' ambapo mara nyingi umekuwa ukivuta hisia kwa watu wengi.