Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wanawake waliong’ara 2018

33054 Wanawake+pic Tanzania Web Photo

Sun, 23 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kuna usemi usemao “Ukimkomboa mwanamke umekomboa jamii nzima’. Hii ni kutokana na namna ambavyo wamekuwa ‘wakiambukiza’ mafanikio kwa jamii nzima.

Katika makala haya inawaleta baadhi ya wanawake waliofanikiwa katika fani mbalimbali katika kipindi cha miezi 12na kuweza kuwa msaada pia kwa wanawake wenzao kama njia moja ya kuwatambua ili waendelee kusonga mbele na kuwa mfano wa kuigwa na wengine kwani hakuna linaloshindikana chini ya jua.

Rebeca Gyumi

Akiwa mwanaharakati wa kutetea haki za wasichana, Rebeca Gyumi, mwaka huu aliipeperisha bendera ya Tanzania katika masuala ya haki za bianadmu kwa kushinda tuzo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa kwa mwaka huu wa 2018.

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Maria Fernanda Espinosa, kupitia ukurasa wake wa Twitter aliwapongeza Rebeca pamojana wenzake walioshinda tuzo hiyo kwa mwaka huu kwa mchango wao wa kusongesha mbele haki za binadamu.

Tuzo hiyo ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa hutolewa kwa watu binafsi na mashirika kwa kutambua mchango wao wa kipekee katika kuendeleza na kulinda haki za binadamu na uhuru wa msingi wa binadamu kwa mujibu wa tamko la haki za binadamu la Umoja wa Mataifa .

Jokate

Julai mwaka huu Rais John Magufuli alimteua mwanamitindo, msanii na mjasiriamali, Jokate Mwegelo kuwa Mkuu wa Wialaya ya Kisarawe.

Jokate ambaye amewahi kuwa mshindi wa pili katika mashindano ya ‘Miss Tanzania’ mwaka 2006 ambapo Wema Sepetu alishinda taji hilo.

Tangu kuteuliwa kushika nafasi hiyo, ameonekana kuchapa kazi kwa kuja na kampeni mbalimbali ikiwemo ile ya kuwasaidia vijana hasa katika kampeni yake mpya ya “Tokomeza Zero’ katika wilaya ya kisarawe.

Vanessa Mdee

Msanii huyu wa Bongo Fleva amekuwa kati ya wasanii wa kike ambaye soko lake analiangalia kimataifa zaidi.

Mpaka sasa ameshafanya kazi na wasanii mbalimbali kutoka nchi za nje akiwemo Peter Okoye kutoka kundi la P Square na kutoa kibao cha Kisela kilichofanya vizuri pamoja na kuachia albamu yake Money Monday.

Ndani ya mwaka huu pamoja na mambo mengine ametambulisha rasmi bidhaa yake ya viatu vya shule alivipa jina la ‘Bora Star’.

Nandy

Mwaka huu pia ulikuwa mzuri kwa upande wa msanii, Faustina Mfinanga maarufu ‘Nandy’, baada naye kuingiza sokoni bidhaa zake za mafuta ya kupaka na sabuni za kuogea.

Mbali na kuja na bidhaa, pia msanii huyu aliandika historia kwa kujinunulia gari mwaka huu alipojizawadia gari aina ya BMW X1wakati wa hafla ya uzinduzi wa albamu yake ya African Princess iliyofanyika Novemba 9, mwaka huu.

Hata hivyo anasema kwa mwakani anatarajia kujizawadia magari mengine mawili huku aina ya gari anazoziota ikiwa ni Audi 7 na Range Rover.

Lady Jay Dee

Akiwa msanii mwenye miaka 18 kwenye muziki wa Bongo Fleva, aliandika rekodi mwaka huu kwa kuandaa shoo yake na kuleta wasanii wa kike akiwamo Bulelwa Mkutukana ‘Zahra’ kutoka nchini Afrika Kusini na Juliana Kanyomozi kutoka Uganda.

Shoo hiyo ambayo ilifanyika ukumbi wa mlimani City, ilipewa jina la ‘Vocals Night’’ na kumfanya kuwa msanii wa kike aliyeweza kuandaa shoo yake na kualika wasanii kutoka nje.

Zamaradi

Akiwa mmoja wa watangazaji maarufu, Zamaradi Mketema mwaka huu alionyesha uthubutu wa kuwatambua watu wenye mchango katika jamii ya kwa kuwapatia tuzo.

Majina ya washindi hao walio katika fani mbalimbali aliwapata kupitia kampeni aliyoifanya kwenye ukurasa wake wa Instagram.

Mbali na hiyo pia Zamaradi aliandaa kongamano lililowakutanisha wanawake mbalimbali aliyoipa jina la Wonder Woman ambapo waliweza kuzungumza mambo ya maisha zikiwemo changamoto wanazokumbananazo na namna ya kuwatoa hapo walipo na kusonga mbele.

Rita Kabati

Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Iringa, Ritha Kabati amefanikiwa kutengeneza viungo bandia ikiwamo miguu na kurejesha furaha kwa kwa watu 25 wenye ulemavu.

Kabati pia amekarabati nyumba ya familia ya watu watano wenye ulemavu wa viungo katika kijiji cha Lulanzi kata ya Mtitu wilayani Kilolo waliokuwa wakiishi kwenye mazingira magumu.

Mkakati wake ni kuwasaidia walemavu 100 waliojitokeza kupata viungo bandia ili waweze kuendelea na kazi zao kama kawaida.

“Nitaendelea kuwatengenezea viungo kwa makundi, nimeanza na hawa 25 nitafuata kundi la pili mpaka namaliza,” alisema.

Alisema kutokana na uamuzi wake wa kuwasaidia walemavu, ameanzisha kitengo maalumu kwenye ofisi yake kwa ajili ya kuwahudumia walemavu peke yao ambao anaamini wanahitaji msaada ili waweze kuendelea na kazi zao za kila siku.

Flaviana Matata

Ulikuwa mwaka mzuri kwa mwanamitindo Flaviana Matata ambaye aliendelea na kazi yake na kuimarisha biashara yake ya Lavy Nails kwa kuongeza bishaa mpya ya mafuta ya mikono.

Manamitindo huyu pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Flaviana Matata inayosaidia watoto wenye uhitaji kwa kuwapatia vifaa vya shule.

Katika kutambua mchango wake, wakati wa hafla ya Global Women Gala iliyofanyika Julai mwaka huu jijini New York, alipewa tuzo ya ‘The Most Inspirational Woman’.

Shamimu Mwasha

Mwandishi na mjasiriamali Shamim Mwasha amekuwa mwanamke wa mfano katika matumizi ya mitandao kibiashara na kuwainua wengine.

Mwanzoni mwaka huu alianzisha shindano la hiyari la Kibubu Challenge kwaajili ya kujiwekea fedha mwaka mzima huku akihamasisha kufanya hivyo kwa malengo.

Watu wengi hasa wanawake na mwishoni mwa mwaka huu walioshiriki wamekuwa wakitoa shuhuda namna shindano hilo lilivyowasaidia kujiwekea fedha.

Pia, amekuwa akitoa mafunzo ya namna watumiaji wa mitandao wanaweza kuitumia kibiashara badala ya kuitumia kwa hasara.



Chanzo: mwananchi.co.tz