Wanandoa waliobadili jinsia kutoka jimbo la kusini mwa India la Kerala, ambao picha zao za ujauzito zilienea katika habari za kimataifa, wamemkaribisha mtoto wao kwa "machozi ya furaha".
Ziya Paval alisema mpenzi wake Zahad alikuwa amejifungua mtoto huyo Jumatano asubuhi.
Bi Paval aliweka habari hiyo kwenye Instagram, akiweka picha ya mtoto huyo ambaye alizaliwa karibu mwezi mmoja uliopita.
Waliambia BBC kwamba Bw Zahad na mtoto huyo, ambaye hawajataja jina na jinsia yake, walikuwa sawa.
Bi Paval na Bw Zahad, ambaye anatumia jina moja pekee, wamesema ilikuwa ndoto yao kuwa wazazi.
Wenzi hao walikuwa wamesitisha matibabu yao ya homoni wakati wa ujauzito.
Mimba yao ilionekana kuwa ni adimu nchini India kwa sababu "hakuna mtu mwingine ambaye amejiita mzazi wa kibaolojia katika jamii ya watu waliobadili jinsia tunavyojua," wenzi hao waliambia BBC mapema wiki hii.
Wawili hao walikuwa katika hatua tofauti za mabadiliko ya kijinsia walipoamua kupata mtoto mwaka mmoja na nusu uliopita.
Kisha walikuwa wamesitisha matibabu yao ya homoni kwa ushauri wa daktari.
Siku ya Jumatano, walipokuwa wakishiriki picha ya mtoto huyo, wenzi hao wa ndoa walisema wanashukuru kwa maombi na uungwaji mkono kutoka kwa watu wao wa karibu.
Tangu kutangazwa kwa mtoto huyo kuzaliwa, pongezi zimemiminika kwa wanandoa hao kwenye kurasa zao za mitandao ya kijamii.
Bw Zahad, mhasibu, alisema alipanga kurejea kazini baada ya miezi miwili huku Bi Paval akimtunza mtoto.