Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wako wapi waliosema Beyonce anapendelewa na baba yake

Beyonce Grammys Record Win 020523 643a564f3a1d41d8a222df995b14bd19 Beyonce

Wed, 15 Feb 2023 Chanzo: Mwanaspoti

Usiku wa kuamkia Jumatatu ya Februari 6 mwaka huu nchini Marekani kulikuwa na utoaji Tuzo za Grammy kwa wanamuziki waliofanya vizuri mwaka 2022.

Mwanamama Beyonce maarufu kama Queen Bey, mke wa gwiji Jay Z akashinda tuzo nne usiku huo zilizomfanya afikishe jumla ya tuzo 32 za Grammy na kuweka rekodi mpya.

Rekodi ya tuzo nyingi za Grammy ilikuwa ikishikiliwa na mwanamuziki kutoka Hungary, Georg Solti aliyekuwa na tuzo 31 na kudumu nayo tangu 1998. Hata hivyo, Solti alifariki dunia mwaka 1997 lakini muziki wake ukashinda tuzo hadi mwaka mmoja baadaye.

Kwa Beyonce, haya ni mafanikio makubwa sana. Lakini safari yake ya muziki haikuwa rahisi hata kidogo. Alianza harakati hizi akiwa na umri wa miaka saba aliposhiriki mashindano ya shuleni kwao ‘school talent show’ huko Houston, Texas. Aliimba wimbo wa mwanamuziki John Lennon ulioitwa Imagine na kushika nafasi ya kwanza.

Wazazi wake, Mathew Knowles na Tina Knowles walikuwa mhimili mkuu kwake wakihakikisha wanamsaidia kufikia malengo yake. Knowles akaamua kuwa meneja wa mwanaye na ili kumsaidia afanikiwe zaidi akawakusanya watoto wengine wenye vipaji na kuwaunganisha katika kundi moja aliloliita Girls Tyme.

Watoto hao walikuwa Kelly Rowland ambaye alikuwa rafiki wa karibu wa Beyonce na wengine wanne LaTavia Roberson, ndugu wawili Nikki na Nina Taylor pamoja na Tamar Davis. Mama yake Beyonce, Tina, ambaye alikuwa akimiliki saluni ya kike ambayo ilikuwa kubwa zaidi kwa ajili watu weusi ndiye alikuwa akiwapamba na kuwaruhusu kufanya mazoezi kwenye saluni yake.

Prodyusa mmoja mkubwa wa R&B wa wakati huo, Arne Frager alipopata sifa za watoto hawa akafunga safari hadi Houston kuonana nao. Ili kuwapromoti zaidi akawatafutia nafasi kwenye mashindano maarufu ya kutafuta vipaji ya Star Search (kama BSS hapa kwetu) yaliyoonyeshwa na televisheni ya taifa.

Lakini kwa bahati mbaya wakashindwa na kundi lingine la watoto wa kiume la Skeleton Crew. Kushindwa kwenye Star Search kulimtia hofu Knowles, baba yake Beyonce, huenda mwanaye asifanikiwe bila usimamizi sahihi.

Akaacha kazi yake iliyokuwa ikimlipa vizuri kama mkurugenzi wa masoko katika Kampuni ya Xerox ili apate muda wa kumsimamia mtoto wake na kundi kwa ujumla. Kazi yake ya kwanza ilikuwa kulijenga upya kundi hilo. Akawapunguza wanamuziki watatu, wale ndugu wawili Nikki na Nina Taylor pamoja na Tamar Davis. Nafasi yao ikachukuliwa na LeToya Luckett pekee.

Kutoka kuwa na watu sita kundi la aliloliita Girls Tyme likabaki na watu wanne tu ambao meneja Knowles aliamini wangeweza kutoboa. Kazi iliyofuata ikawa kutafuta jina ambalo litapenya kutoka lile lenye gundu la Girls Tyme ambalo liliwafanya washindwe kwenye Star Search.

Wakapitia majina kadhaa kama Something Fresh na The Dolls kabla hawajatua kwenye jina lililowatoa la Destinyís Child. Jina hili lilikuwa na upako kidogo kwani mama yake Beyonce, Tina alipendekeza neno Destiny ambalo aliliona kwenye Biblia. Lakini wasingeweza kuliwekea hakimiliki, hivyo wakaongeza neno Child ambalo lilikuwa wazo la baba, Mathew.

Ndipo likapatikana jina la Destiny’s Child...likapenya! Madili yakaanza kuja wakianza na Kampuni ya Elektra Records lakini baada ya muda mfupi wakavunjiwa mkataba.Baada ya maanguko mengi hatimaye wakasaini mkataba na Kampuni ya Columbia Records mwaka 1997.

Wakatoa albamu yao ya kwanza ya Killing Time ambayo ilitamba sana kiasi cha kutumika kama wimbo wa kusindikizia (sound track) filamu ya Men in Black. Mwaka 1999 wakatoa albamu nyingine ya Bills, Bills, Bills iliyoshika namba moja kwenye chati za Billboard.

Nyakati zote hizo, Beyonce ndiye alikuwa mwimbaji kinara wa kundi.

Hii ikaleta chuki kwa wengine na kuzua mzozo kutoka kwa wenzao wawili, LeToya Luckett na LaTavia Roberson.

Wawili hawa walilalamika kwamba meneja wao, Knowles ambaye ni baba wa Beyonce anampendelea sana mwanaye kwa kumpa nguvu nyingi kwenye kundi.

Lawama hizi zilimkera meneja wao na kuwatimua kundini. Kundi likabaki na wanamuziki wawili tu Beyonce na rafiki yake wa tangu na tangu Kelly Rowland. Meneja akamtafuta mwimbaji mwingineili angalau wawe watatu ndipo akapatikana Michelle Williams.

Wale wawili waliotoka wakaenda kufungua kesi mahakamani wakianza na meneja wao, Mzee Knowles na Beyonce na Kelly.

Kesi hiyo ilidumu hadi mwaka 2002 walipoyamaliza nje ya mahakama bila kutolewa taarifa zozote za makubaliano.

Misukosuko hii ndiyo iliyowafanya Destiny’s Child watunge wimbo wa Survivor ambao ulitamba sana mwaka 2002. Maana ya jina la wimbo huu ni manusura, na wao walijiona manusura wa misukosuko ya mahakamani.

Wale waasi waliposikia mashairi ya wimbo huu wakarudi tena mahakamani wakisema wenzao wamewapiga kijembe ilhali walikubaliana kwenye yale mapatano ya nje ya mahakama kusiwe na aina yoyote ya chokochoko baina yao.

Mwaka 2004, Kundi la Destiny’s Child (Beyonce, Kelly na Michelle) likasambaratika na kila mmoja kufanya kazi kivyake.

Tangu hapo Beyonce amekuwa akifanya vizuri huku wenzake wote wakipotelea kusikojulikana. Hata wale waasi hawajulikani kabisa waliko. Hii inathitisha kwamba Beyonce hakuwa akipendelewa na baba yake bali alistahili kwa uwezo wake.

Ndio maana watu wanasema ‘Kama unajua - unajua tu.’

Chanzo: Mwanaspoti