Aliyekuwa mgombea wa urais katika uchaguzi mkuu uliopita kupitia tiketi ya chama cha Roots wakili msomi Profesa George Wajackoyah ameamua kuingilia mzozo wa ugomvi baina ya msanii Diamond Platnumz na baba yake mzee Abdul Jumaa.
Wajackoyah ambaye mwishoni mwa wiki hii alikuwa Tanzania kama wakili wa mkimbizi wa kisiasa, mbuunge Godbless Lema alipata nafasi ya kuzungumza na wanahabari na alitolea mfano kwamba uhusiano wake na baba yake miaka ya nyuma ulikuwa kama ule wa Diamond na mzee wake sasa hivi.
Wajackoyah alisema yuko tayari kuwapatanisha wawili hao, na kumshauri Diamond kutobeba chuki ya baba moyoni mwake kwani kaburi ni tajiri kumliko na wala hafai kusubiri mpaka pale kifo kitakapotokea ndio kutafuta upatanishi.
Alisema yuko tayari kukutana na Diamond popote pale hata kama ni kumlipia nauli ya ndege kwenda New York ili kuwapatanishi. Pia alisema kama Diamond atakanusha wito wake, basi atajaribu kumfikia mzee wake na kumualika ili kujaribu kutafuta mwafaka baina yake na mtoto wake.
“Hata awe na utajiri wa kufika wapi, niulize mimi. Nilikuwa kama yeye, sikuwa namtaka mzee wangu. Nilimchukia kwa kumkataa mama yangu. Lakini nilienda nikaongea naye, akanipatia shamba ambapo nilimzika wakati alifariki na neema zikaanzia hapo kunifuata,” Wajackoyah alisema.
“Mwambie huyu kijana mdogo Diamond, kaburi ni tajiri kuliko yeye, asingojee mpaka wakati wa kwenda kwa kaburi. Ninamuuliza akuje tukutane na nitamlipia ndege tuongee mambo na amalize hili tatizo la mzee wake wamalize. Na kama hataki mimi ninamuita mzee Kenya niombe msamaha kwa niaba ya Diamond,” Aliongeza.
Mwanasiasa huyo pia alijitapa kama ndiye shujaa mkubwa wakili wa kuwawakilisha mastaa wengine wa kimuziki kama Koffi Olomide, akisema Diamond akimtafuta pia itakuwa fursa nyingine nzuri kwake kumkutanisha na mastaa hao wengine.
Diamond na mzee wake hawajawahi patina katika kile kinatajwa kuwa ni msanii huyo kumchukia babake kwa kumtelekeza kipindi akiwa mdogo.
Kwa sasa, mzee Abdul anaugua saratani ya ngozi ambapo katika mahojiano ya hivi karibuni alisema anategemea msaada kutoka kwa wasamaria wema kwa ajili ya dawa.