Waigizaji wawili mashuhuri wa Iran wamekamatwa kwa kuunga mkono hadharani maandamano makubwa ya kuipinga serikali, vyombo vya habari vya serikali ya nchi hiyo vimeripoti.
Hengameh Ghaziani na Katayoun Riahi wanatuhumiwa kwa kula njama na kukaidi mamlaka ya Iran, shirika la habari la Irna linasema.
Wanawake wote wawili hapo awali walionekana hadharani bila hijabu zao - ishara ya mshikamano na waandamanaji.
Maandamano hayo yalizuka mwezi Septemba baada ya kifo cha mwanamke aliyekuwa chini ya ulinzi wa polisi.
Mahsa Amini, 22, alizuiliwa na polisi wa maadili katika mji mkuu, Tehran, kwa madai ya kuvunja sheria kali za hijab. Alikufa mnamo Septemba 16, siku tatu baadaye.
Kulikuwa na ripoti kwamba maafisa walimpiga kwa fimbo na kugonga kichwa chake kwenye gari, lakini polisi walikanusha kwamba alitendewa vibaya na kusema alipatwa na mshtuko wa moyo.
Bi Ghaziani na Bi Riahi - wote waigizaji walioshinda tuzo nyingi - walizuiliwa siku ya Jumapili kwa amri ya ofisi ya mwendesha mashtaka wa Iran, Irna inasema.
Kabla ya kukamatwa, Bi Ghaziani aliandika kwenye mtandao wa kijamii kwamba "chochote kitakachotokea, fahamu kuwa kama kawaida nitasimama na watu wa Iran".
"Hili labda chapisho langu la mwisho," aliongeza.