Lifestyle

Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

SIL

Wahudumu wa baa walalamika kunyanyaswa kazini

Baa Wahudumu Pic Wahudumu wa baa walalamika kunyanyaswa kazini

Wed, 21 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wahudumu wa  baa wilayani Nachingwea Mkoa wa Lindi, wamelalamika kunyanyaswa na baadhi ya wateja na wengine wakiwalalamikia waajiri wao kuwakata mishahara, jambo linalotajwa kuwarudisha nyuma kimaisha.

Wakizungumza katika kikao cha mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Mohamedi Moyo, jana Februari 19, 2024, wahudumu hao wamelalamika kufanyiwa ukatili na baadhi ya wateja ikiwa pamoja na kutukanwa, kebehi na kukatwa fedha na waajiri wao wanapopata udhuru.

Anna Hamis, mhudumu wa baa amesema asipofanya usafi anatoa Sh20,000 na endapo atachelewa kazini atakatwa Sh5,000, hivyo mpaka siku ya kupokea mshahara hakuna fedha inayobaki.

"Kwa hali kama hii unakuta hakuna unachokifanya na maisha yanazidi kuwa magumu. Wengine tun awatoto tumewaacha kijijini, tumekuja huku kufanya kazi ili tupate fedha za kuendesha maisha," amesema Anna.

Kwa upande wake, Neema Baraka amesema baa nyingi zinajulikana malipo yake, lakini hadi inafikia mwisho wa mwezi unakuja kulipwa Sh25,000 au Sh20,000 kwa kuwa fedha yote inakuwa imekatwa kwenye makato ambayo hayaeleweki.

"Licha ya makato yasioeleweka, pia unamkuta bosi anakutukana matusi mbele ya mteja, huo ni unyanyasaji ambao haukubaliki kabisa, kwani hata sisi tuna haki zetu," amesema Neema.

Akizungumzia malalamiko hayo, meneja wa baa, Teddy Mayunga amekiri kuwepo kwa shutuma hizo akisema kuwa makato ni makubaliano baina ya mhudumu na mmiliki na kwamba wasipowakata wahudumu wanaofanya makosa, husababisha hasara.

Naye Frank Ujamaa, meneja wa baa wilayani humo, amesema, "Kuna baadhi ya wamiliki ni wakandamizaji kwa wahudumu, hilo halifichiki, lakini sisi tunapata shida na aina ya wahudumu, kwani tunapokea dada wengine ambao wameshindikana huko walipotoka. Kama tungekuwa tunafanya mahojiano haya mengine yasingekuwepo.”

Akizungumzia malalamiko hayo, Mkuu wa Dawati la jinsia na Watoto Wilaya ya Nachingwea, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Asha Mponda, ametoa onyo kwa askari na raia wanaowanyanyasa wahudumu hao.

Amewataka wahudumu hao kutoa taarifa mara moja wanaponyanyaswa, ili mhusika achukuliwe hatua.

"Nitoe onyo kwa wote wanaowanyanyasa wahudumu wa baa, kutoa taarifa katika vyombo vya sheria na kuwachukulia hatua stahiki," amesema Asha.

Mkuu wa dawati la jinsia na watoto, wilaya ya Nachingwea, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Asha Mponda (aliyesimama) akiwa na mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Mohamed Moyo walipokuwa wakizungumza na wahudumu wa baa.

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamedi Moyo amesema kwa sasa wilaya hiyo  inakuwa kwa kasi na kwamba Serikali inafanya jitihada kubwa kuitangaza na kuvuta wageni.

“Raha ya bia inatokana na mhudumu, ndio watu watakuwa na hamu ya kuja. Mtu anatamani kutoka Lindi aje kujirusha Nachingwea, lakini kama hakuna kinachovutia hakuna atayekuja, watu wanatoka Ulaya wanakuja Tanzania kwa sababu wanavutiwa na mazingira na huduma,” amesema DC Moyo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live