Viongozi wa dini Zanzibar wamesema kuwa katika Uislamu ni dhambi na haramu mwanaume kusuka nywele au kutumia mapambo ya mwanamke kwa sababu ni sawa na kujifananisha na mwanamke.
Shekhe Shaban Khamis, akizungumza na Nipashe Digital leo Julai 11,2023 amesema katika sheria ya usilamu kuna mambo mawili ikiwemo katazo lisilo na hukumu na lenye hukumu kisheria.
Amesema kusuka nywele kwa wanaume ni katazo lenye hukumu ambapo dini imetoa maelekezo kuwa inahaki ya kufuata hukumu iliyowekwa na serikali hivyo ni sahihi kwa Zanzibar kuweka kifungo cha miezi sita au faini ya shilingi milioni 100.
Askofu wa Kanisa la RGC, Charles Kiyengo, amesema mwanaume kusuka linaendana na utamaduni. Mfano tamaduni za kiimasai ambazo zinaruhusu jambo hilo.
Aidha amesema kama mtu tamaduni yake inakataza mwanaume kusuka ni busara kutosuka kama ilivyo kinyume na tamaduni ya mtanzania kwamba hairuhusu mapenzi ya jinsia moja.
Viongozi hao wa dini wamesema hayo baada ya kuzuka kwa mjadala mkubwa katika mitandao ya kijamii kuhusu katazo la baraza la Sanaa, sensa, filamu na utamaduni kuhusu katazo la kisheria la mwanaume kusuka ambapo adhabu yake ni shilingi milioni moja au kifungo cha miezi sita jela au adhabu zote mbili.