Wizara ya Usawa wa Jinsia na Familia ya nchini Korea Kusini imetangaza kwamba itatoa Won 650,000 ($500) ambazo ni sawa na TZS 1,172,500 kwa mwezi kwa kila kijana anayepitia hali ya upweke kwa nia ya kuwasaidia kwenye mfumo wao wa kisaikolojia kuimarisha afya zao za akili.
Mambo mbalimbali yanayofikiriwa kwenye kuchangia hali hii ya upweke ni pamoja na ugumu wa upatikanaji wa fedha, magonjwa ya akili, matatizo kwenye ngazi za familia au changamoto za afya.
Hatua hizo mpya zinalenga hasa Vijana kama sehemu ya Sheria kubwa ya Usaidizi wa Ustawi wa Vijana ambayo inalenga kusaidia Watu waliojitenga sana na jamii pamoja na Vijana wasio na Mlezi au ambao hawahudhurii masomo wakiwa hatarini kujihusisha na uhalifu.
Posho ya kila mwezi itapatikana kwa waliojitenga na wanaopitia hali ya upweke wenye umri wa kuanzia miaka 9 hadi 24 ambao wanaishi katika Familia zenye mapato ya chini ya wastani wa mapato ya kitaifa.
Vijana wanaweza kutuma maombi kwa ajili ya programu hii katika ofisi za Ustawi wa Jamii lakini pia Walezi wao, Washauri au Waalimu wanaweza pia kutuma maombi kwa niaba yao.