Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Vijana kutoka nchi sita kuchuana Tanzania jinsi ya kuandika mashairi ya Kifaransa

Vijana kutoka nchi sita kuchuana Tanzania jinsi ya kuandika mashairi ya Kifaransa

Sat, 7 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wanafunzi wa Sekondari kutoka nchi sita wamekutana nchini Tanzania kwa kambi ya siku tatu kwa ajili ya maandalizi ya shindano la uandishi wa mashairi ya Kifaransa.

Kilele cha tamasha lililobuniwa na kisiwa cha Mayotte linatarajiwa kufanyika leo Jumamosi Desemba 7, 2019 katika mgahawa wa soma ambapo vijana hao zaidi ya 15 wataonyesha vitu mbalimbali ambavyo wameviandaa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi mtendaji na Mwenyekiti wa Soma, Demere Kitunga amesema kuandaliwa kwa shughuli hiyo ni mwendelezo wa matamasha mbalimbali ambayo yamekuwa yakiandaliwa na kisiwa cha Mayotte yaliyo na lengo la kukuza utamaduni wa usomaji na uandishi.

“Vijana hao wanatoka Tanzania, Msumbiji, Djibouti, Commoro, Madagascar na kisiwa cha Mayyote na walishindana katika shindano la kuandika hadithi, ushairi, hadithi za kimapokeo.”

Vijana hao kabla ya kufikia tamati ya tamasha walikaa pamoja kwa siku tatu, wakishirikiana kusomeana na kupeana mirejesho katika hadithi zao.

“Na katika siku hizo walizokaa pamoja walizalisha kazi ya fasihi moja wapo kwa pamoja na kutunga wimbo wa Kiswahili ambavyo vyote vitaonyeshwa,” amesema

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utamaduni na Matukio kutoka Mayotte, Dk Alain Henry amesema lengo lao ni kuwaleta pamoja waandishi wadogo kutoka katika ukanda huo ili waweze kushirikiana katika kufanya kazi zao.

“Mwaka huu tumekuja nchini Tanzania ikiwa ni mara ya kwanza katika historia, tunatumia na Kiswahili ili kuweza kupanua wigo wa mawasiliano na kubadilishana uzoefu ili kufanikisha kilichokusudiwa,” amesema

Chanzo: mwananchi.co.tz