Video ya mtoto aliyezama kwenye kidimbwa cha watoto kuogelea sio ya mtoto wa msanii nyota wa Nigeria Davido, mamlaka imesema.
Video hiyo inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii inavuma kwa kasi huku baadhi ya watu wakisema mwathiriwa ni Ifeanyi Adeleke ambaye kifo chake cha Jumatatu katika makazi ya babake huko Lagos kinachunguzwa na polisi kwa sasa.
Msemaji wa polisi alitaja video hiyo kama "feki".
"Bado hatujaanza kukagua CCTV iliyopatikana nyumbani kwa Davido. Video yoyote unayoona mtandaoni si kitu halisi. Ni bandia,” msemaji wa polisi mjini Lagos, kitovu cha kibiashara cha Nigeria Benjamin Hundeyin aliambia BBC.
Kitengo cha habari cha upotoshaji cha BBC kimethibitisha kuwa video inayoonyesha tukio la kuzama la Ifeanyi Adeleke ni picha ya CCTV ya mvulana wa miaka miwili akizama nchini China.
Tukio lililoonyeshwa kwenye video hiyo lilitokea Uchina mnamo Agosti 23, 2019.
Kisa cha mtoto mchanga kufa maji ilienea kwenye vyombo vya habari wakati wa tukio.
Davido na mchumba wake Chioma Rowland, mpishi maarufu na mvuto, bado hawajatoa maoni yoyote kuhusu kifo cha mtoto wao.
Siku ya Jumanne wafanyikazi wanane wa nyumbani wa mtu mashuhuri walialikwa kuhojiwa, sita kati yao wameachiliwa.
Hundeyin alithibitisha utambulisho wa mmoja wa mshukiwa ambaye bado anazuiliwa kuwa yaya wa marehemu Ifeanyi.
"Tunatumai kuwahamishia katika idara ya upelelezi wa jinai ya Serikali leo [Jumatano] kwa mahojiano zaidi," alisema.