Dar es Salaam. Msanii Vanessa Mdee jana Jumamosi Julai 27, 2019 alifanya sherehe ndogo ya kukutana na watu wake wa karibu lakini kati ya mambo ambayo hakutaka kuyazungumza ni kuhusu mpenzi wake wa zamani, Jux.
Pamoja mambo mbalimbali alitambulisha albamu yake yenye nyimbo sita, baadhi akiwa ameimba na wasanii Rayvanny na Mboso.
Katika sherehe hizo zilizofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watu wasiozidi 50 wakiwemo wasanii maarufu, nyimbo hizo zilipigwa na kuonekana kuwakuna vilivyo.
Baada ya kuingia ukumbini, Vanessa alisalimiana na kila aliyehudhuria, baadaye kuitwa jukwaani na mshereheshaji, Perfect Crispin na kuanza kutumbuiza.
Moja kati ya nyimbo alizoimba ni wimbo Moyo unaotesa katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni nchini.
Mwananchi lilipotaka kufahamu kuhusu sababu za kuvunjika kwa uhusiano wake na Jux, msanii huyo aligoma akitaka kuulizwa mambo yanayohusu sherehe hiyo.
Pia Soma
- Lugola amvua madaraka mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Arusha
- VIDEO: Khadija Kopa awakaribisha JWTZ Mwenge taarabu kwa kishindo
- Mbatia achaguliwa tena uenyekiti NCCR-Mageuzi
Hivi karibuni Jux ameonekana katika mitandao mbalimbali ya kijamii akiwa na mwanamke mwingine wakila raha maeneo mbalimbali ndani na nje ya Tanzania.
“Hapa nimekuja kukutana na watu wangu wa karibu na kuwaonjesha albamu yangu, sijaja kumzungumzia Jux naomba uulize swali jingine,” amesema Vanessa.
Baadhi ya wasanii waliohudhuria sherehe hizo ni Shilole, Navy Kenzo, Mimi Mars na Whoze.