Kibaha. Steve Nyerere mmoja kati ya wasanii wenye majina makubwa hapa Bongo, ndio msanii pekee aliyehudhuria hafla ya kuapishwa kwa mkuu mpya wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo.
Hata hivyo, msanii huyo ambaye moja ya sauti zilizompa umaarufu ili ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na ndio iliyompa jina hilo la Steve Nyerere, alichelewa kufika katika hafla hiyo na kukuta tayari Jokate ameshakula kiapo.
Akizungumza na MCL Digital leo Ijumaa Agosti 3, 2018, Steve ambaye jina lake halisi ni Steven Mengele, amesema amechelewa kutokana na foleni katika barabara ya Morogoro.
Alipoulizwa sababu za wasanii wenzake kutoonekana katika hafla hiyo amesema hawezi kuwazungumzia wenzake kwa maelezo kuwa huenda wanahangaika na mambo mengine ya utafutaji wa maisha.
“Wengine ambao hawajafika inawezekana mwakilishi wao ni mimi. Wote hatuwezi kuhudhuria kutokana na utafutaji huenda ndio sababu ya kutofika kwao, lakini mimi nimekuja kuwawakilisha wenzangu,” amesema.
Amemtaka Jokate kutojisikia mpweke kwa wasanii kutojitokeza kwa maelezo kuwa wanamuunga mkono na wameupokea uteuzi wake kwa mikono miwili.