Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Simulizi maisha ya Dj JD kambi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini

Video Archive
Mon, 19 Aug 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Wakati vijana wengi wakitamani kwenda Afrika Kusini kutafuta maisha  kwa John Dilinger  Matlou maarufu DJ JD au The Everlasting DJ hana ndoto hizo kabisa.

Neno DJ ni kifupi cha maneno Disc Jockey linalomaanisha mtu anayechezesha muziki uliorekodiwa kwa ajili ya kuburudisha mkusanyiko wa watu.

Dilinga alizaliwa mwaka 1973 katika kambi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini ya Solomon Mahlangu Mazimbu (Somafco) iliyopo mkoani Morogoro.

Baba yake ana asili  ya Afrika Kusini na alitakiwa kurejea nchini humo baada ya Taifa hilo kupata uhuru wake mwaka 1994, lakini Dilinga  alichagua kubaki Tanzania.

Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi hivi karibuni, JD anasimulia maisha yake akiwa kambini Morogoro na kueleza sababu kwa nini hakutaka kwenda kuishi Afrika Kusini.

Swali: Tueleze maisha yako na kwa nini ulibaki Tanzania baada ya kambi ya Somafco kufungwa?

Pia Soma

Jibu: Mimi nimezaliwa Morogoro katika kambi ya Somafco. Sikumbuki vizuri baba yangu alifika Tanzania lini, lakini alikuwa akija na kuondoka kutokana na kazi zake hadi alipofariki akiwa nchini Zambia.

Kwa upande wa baba yangu ni mtoto wa kwanza na kwa mama ni mtoto wa mwisho.

Swali: Maisha ya kambini yalikuwaje?

Jibu: Maisha ya kambini yalikuwa mazuri ukilinganisha miaka ile ya 1960 na 1970 hali ilivyokuwa Tanzania jinsi watu walivyokuwa wakiishi.

Sisi kama watoto wa wapigania uhuru tulikuwa tunapewa kila kitu. Kwa mfano mimi nilipokuwa mdogo kila wiki nilikuwa napewa jozi ya viatu na nguo. Maisha yalikuwa mazuri.

Kuanzia malazi, chakula na masomo kwa sababu tulikuwa tuna walimu wazungu miaka ile 1960 hadi 1970 halikuwa jambo la kawaida.

Swali: Pale Somafco ulisoma hadi darasa la ngapi?

Jibu: Nilisoma hadi unit 10 ambayo ni sawa na kidato cha tano na ndipo uhuru wa Afrika Kusini ukawa umepatikana na tukatakiwa kwenda huko.

Swali: Kwa hiyo kambi yote mliondoka?

Jibu: Tulitakiwa kurudi Afrika Kusini, lakini awali mama alinizuia akisema kule nitakwenda kutunzwa na nani? Jina langu liliendelea kuletwa ili niende, lakini mama alizuia. Lakini nilikuja kwenda baada ya miaka mitatu na nilitumia ziara hiyo kuwasalimia ndugu zangu, shangazi na wajomba na kutembelea kaburi la baba yangu.

Swali: Kwa nini umeamua kuishi Tanzania wakati ulipata mafunzo ya ukombozi na ulitakiwa kurudi Afrika Kusini kuyafanyia kazi?

Jibu: Niliamini kuishi karibu na mama yangu ili niendelee kumtunza. Mimi ni mzaliwa wa Morogoro kwa baba Mwafrika Kusini na mama Mtanzania, lakini kwa Waluguru, mtoto ni wa mama siku zote. Mimi ‘officially’ ni Mtanzania na ni Mluguru wa Morogoro.

Swali: Mkiwa Somafco katika mafunzo mlielezwa yaliyokuwa yakiendelea Afrika Kusini?

Jibu: Moja ya elimu tuliyokuwa tukipewa ni pamoja kile kinachoendelea Afrika Kusini yaani ubaguzi wa rangi, tulikuwa tunafahamu kwa nini tupo Somafco, kwa nini wazazi wako hapo na kwa nini kambi ile iko pale.

Kwa wakati ule tukiwa wadogo kila mtu alikuwa anapenda Afrika Kusini kuona kinachoendelea, lakini bado ubaguzi wa rangi ulikuwepo.

Kila mtu alikuwa natamani kuona Afrika Kusini, uzuri wake, unajua maisha ya Afrika Kusini ni kama Ulaya. Hata wale waliokimbia uhamishoni walikuwa wanatamani uhuru upatikane na mapigano yaishe ili warejee.

Swali: Kwa nini ulibadili mawazo dakika za mwisho?

Jibu: Kila mtu ana chaguo lake, mimi nilifanikiwa kwenda Afrika Kusini kuwaona ndugu zangu, watu ambao wako upande wa baba yangu na kiu nyingine ilikuwa kwenda kuona kaburi la baba yangu.

Swali: Je, kuna watu unawakumbuka ulikuwa nao kambini Somafco leo wameshikilia nyadhifa katika Serikali ya Afrika Kusini?

Jibu: Ndiyo wapo, wengine ni wanajeshi wengine ni watendaji serikalini. Tunawasiliana na tuna makundi ya WhatsApp tunawasiliana sana. Wengi hufanya safari za kuja kutembelea Mazimbu.

Swali: Mwaka 1990, Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini, Nelson Mandela alitembelea Tanzania, hali ilikuwaje, je ulimuona?

Jibu: Alikuja Morogoro lakini hakufika Mazimbu bali aliishia uwanja wa Jamhuri. Tulifika pale uwanjani tukamsikia akihutubia. Wakati huo kambi ilikuwa imeshavunjwa na watu wengi walishaondoka.

Swali: Kwa sasa wewe ni DJ na umewahi kufanya kazi kwenye vyombo vya habari. Uliisomea kazi hiyo?

Jibu: Hapana. Baada ya kambi kuvunjwa nikiwa kidato cha tano sikuendelea tena na shule. Hii kazi naifanya kama kipaji tu. Nimeshafanya kazi Radio One, East Africa radio na ITV, Club Billicanas na kwa sasa nafanya biashara zangu na kupiga disco katika project ya The Legends.

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz