Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Sh2 milioni zilivyomnusuru Wema kifungo cha mwaka mmoja jela

Video Archive
Sat, 21 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Nyota maarufu wa filamu nchini, Wema Sepetu amefanikiwa kulipa faini ya Sh2 milioni na hivyo kuepuka kifungo cha mwaka mmoja jela.

Wema alilipa faini hiyo jana baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumtia hatiani mlimbwende huyo kutokana na mashtaka ya kukutwa na kutumia dawa za kulevya aina ya bangi.

Katika hukumu hiyo, Wema alipaswa kufanya mambo mawili; kulipa faini ya Sh1 milioni kwa kila kosa au kutumikia kifungo cha mwaka mmoja jela.

Wakati Wema akikutwa na hatia, washtakiwa wenzake katika kesi ya kukutwa na dawa za kulevya na matumizi ya dawa hizo ambao ni wafanyakazi wake wa ndani, Angelina Msigwa na Matrida Abbas waliachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

Akisoma hukumu hiyo iliyochukua zaidi ya dakika 45, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba alisema upande wa mashtaka ulipeleka mashahidi watano ambao walithibitisha mashtaka hayo.

Hakimu alisema baada ya upande huo kufunga ushahidi wake, washtakiwa wote walikutwa na kesi ya kujibu na walijitetea wakiongozwa na Wakili Albert Msando.

“Unajua ni jukumu la upande wa mashtaka kuthibitisha mashtaka bila ya kuacha shaka na sio mshtakiwa,” alisema Hakimu Simba.

“Pia upande wa mashtaka unapaswa kuthibitisha kuwa Wema anatumia dawa za kulevya pasi na kuacha shaka lolote.”

Aliendelea kusema kuwa, “mshtakiwa wa pili na wa tatu hawakushiriki kwenye upekuzi katika nyumba ya Wema na bangi zilikutwa jikoni, chumbani na kwenye kiberiti ndani ya nyumba ya Wema.”

Alieleza kuwa mshtakiwa mwenyewe katika ushahidi wake alikiri kwamba alikutwa na bangi nyumbani kwake, alitia saini katika barua ya upekuzi na alikubali kwamba mkojo wake ulichukuliwa na kupelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali.

“Nawaachia huru mshtakiwa wa pili na wa tatu kwa kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao, lakini kwa upande wa Wema hakuna shaka lolote kwamba alipatikana na dawa za kulevya,” alisema hakimu.

Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Hakimu Simba alisema katika ushahidi uliowasilishwa na shahidi wa kwanza, Elias Mulima ulieleza kuwa bangi iliyokutwa katika mkojo wa Wema ilikuwa ya siku 28.

Kabla ya kutolewa hukumu hiyo, Wakili wa Serikali, Constantine Kakula alidai kuwa matumizi ya dawa za kulevya yamekithiri katika Taifa na kwamba mshtakiwa ni msanii na ni kioo cha jamii na pia ana watu wengi wanaomuangalia na kumfuata.

“Naiomba Mahakama yako itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa huyu kwa sababu mashtaka yanayomkabili yamekithiri katika Taifa letu, vijana wengi wanaangamia kwa kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya,” alidai Kakula.

Kakula alidai kuwa mshtakiwa anatakiwa kupewa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwa wanaotumia au wanaotegemea kujihusisha na matumizi ya dawa za kulevya.

Baada ya wakili wa Serikali kueleza hayo, wakili anayemtetea Wema, Albert Msando alidai kwa mujibu wa sheria aliyoshtakiwa nayo mteja wake kifungu namba 17 (1) b ya mwaka 2015, inaelekeza kwamba adhabu zake ni faini isiyopungua Sh500,000 au kifungo cha mwaka mitatu au vyote kwa pamoja.

Msando alidai mteja wake hana makosa ya zamani na kwamba Mahakama ina uwezo wa kutoa adhabu nafuu ili kumsaidia kujirekebisha kufikia malengo ya sheria hiyo ya kudhibiti matumizi ya dawa za kulevya nchini.

“Tunaomba mshtakiwa apewe nafasi ya kujirekebisha kwa makosa aliyoshtakiwa nayo, apatiwe adhabu ya kulipa faini ili ahamasishe wengine kujiepusha na dawa za kulevya badala ya kumsweka gerezani,” alidai Msando.

Baada ya kusikiliza maelezo ya pande zote, Hakimu Simba alitoa hukumu ambapo alisema mfumo wa sheria unaelekeza kuwa si busara kumpa kifungo mshtakiwa kwenye kosa la kwanza, lakini Mahakama inatoa adhabu.

Katika hati ya mashtaka, Wema alikuwa anakabiliwa na mashtaka mawili ya kukutwa na kiwango kidogo cha dawa za kulevya na kuzitumia.

Inadaiwa Februari 4, 2017 katika makazi ya msanii huyo eneo la Kunduchi Ununio wilayani Kinondoni, washtakiwa walikutwa na msokoto mmoja na vipisi vya bangi vyenye uzito wa gramu 1.08.

Kwa mara ya kwanza, Wema alifikishwa Kisutu, Februari 9, 2017, kujibu mashtaka hayo.

Hali ilivyokuwa mahakamani

Mashabiki wa Wema walifurika katika mahakama hiyo kwa ajili ya kusikiliza hukumu, huku wakionekana kuwa na wasiwasi.

Mbali na mashabiki waliofika katika Mahakama hiyo, mama yake Wema, Miriam Sepetu; meneja wa nyota huyo, Martine Kadinda, dada na jamaa zake ni miongoni mwa watu waliohudhuria mahakamani hapo na kusikiliza hukumu hiyo, huku muda wote wakionyesha nyuso za upole tofauti na siku zilizopita.

Chanzo: mwananchi.co.tz