Bukoba. Jana, saa 10.01 jioni jeneza lenye mwili wa Ruge Mutahaba lilishushwa kaburini wakati vilio vikitawala katika Kijiji cha Kiziru wilayani hapa.
Ilichukua takriban dakika moja kwa jeneza hilo kufika chini lilipokuwa likishushwa taratibu na waombolezaji.
Ruge aliyefia nchini Afrika Kusini Februari 26, amehitimisha safari yake hapa duniani na kitabu cha hadithi yake kufungwa rasmi.
Maelfu ya watu walishuhudia safari hiyo ya mwisho ya Ruge aliyekuwa mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, ambapo kila mmoja alionyesha alivyomgusa kwa vitendo au maneno yake.
Katika tukio hilo baadhi ya watu waliinuka na kuweka maua ndani ya kaburi lake isipokuwa mama yake mzazi, Christiana Mutahaba ambaye alikataa kuweka udongo juu ya jeneza la mwanaye likiwa kaburini.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alichukua takriban sekunde 30 akilitazama kaburi la Ruge baada ya kuweka maua kisha aliondoka akiwa ameinamisha kichwa.
Wapo watu waliopiga ishara ya msalaba vifuani, walioinama na waliopiga saluti hasa vijana kama ishara yao ya heshima.
Baada ya kuweka maua ndani ya kaburi, mtangazaji wa Clouds FM, Hamis Dakota alipiga saluti.
Ibada ya mazishi ya Ruge iliongozwa na katekista wa Kanisa Katoliki Kigango cha Rwakagongo, Parokia ya Itahwa, Edward Rwegoshora huku nyimbo za Kihaya zikipamba tukio la mazishi.
Awali wakati wa tukio la kuaga mwili wake katika viwanja vya Gymkhana, maaskofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba walimtaja Ruge kama kijana jasiri, mzalendo na mfano wa kuigwa.
Askofu Desderius Rwoma aliitaka jamii kuenzi mambo mema aliyoacha huku msaidizi wake, Methodius Kilaini akisema vijana wengi wamepata mafanikio kutokana na uthubutu wake na ujasiri wa kusimamia aliyoyaamini.
Ruge aliyebobea katika masuala ya burudani na utangazaji, mazishi yake yalihudhuriwa na vigogo zaidi ya kumi wakiwemo mawaziri, wabunge na wakuu wa mikoa.
Baadhi ya mawaziri walioshiriki mazishi yake ni Dk Hamis Kigwangalla (Maliasili na Utalii), Dotto Biteko (Nishati), January Makamba (Ofisi ya Makamu wa Rais), Angellah Kairuki (Uwekezaji) na Juma Aweso ambaye ni Naibu Waziri wa Maji.
Pia, baadhi ya wabunge walishiriki mazishi hayo akiwamo Ridhiwani Kikwete, Aeshi Hilary na wengine wote wa Mkoa wa Kagera pamoja na wakuu wa wilaya.
Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Simiyu, Mwanza, Mara na mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Oseah Ndagala.
Tukio la kuuaga mwili wa Ruge katika viwanja vya Gymkhana lilikuwa lianze saa nne asubuhi, lakini lilicheleweshwa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha muda huo.
Clouds yazimwa kwa dakika tatu
Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha takribani miaka 20, Redio Clouds FM haikuwa hewani kwa dakika tatu baada ya kuzimwa wakati mwili wa Ruge ukishushwa kaburini.
Watangazaji wa redio hiyo, Hassan Ngoma na Baby Kabaye walisema ingeondoka hewani kwa heshima ya kiongozi wao huyo.
Ngoma alisema Clouds FM ingekosekana hewani kwa muda huo kwa kuwa Ruge alishiriki kuanzishwa kwake na mpaka alipofariki dunia alikuwa akiitumikia.
Baby Kabaye aliwataka wasikilizaji wa redio hiyo kutumia dakika hizo kumuombea kiongozi wao ambaye alizaliwa nchini Marekani miaka 49 iliyopita.
Kwa nini historia haitamsahau?
Ruge atakumbukwa kwa mengi, lakini miongoni mwa hayo ni kuasisi kwake tuzo kadhaa ikiwamo ya Malkia wa Nguvu na kuiendesha chini ya Clouds Media Group inayolenga kutambua juhudi za wanawake katika nyanja mbalimbali za maisha na kuwatambulisha kwenye jamii.
Tuzo sita zimekuwa zikiwaniwa katika kampeni hiyo ambazo ni sayansi na teknolojia, kilimo na biashara, mwanamke mhamasishaji, afya, usambazaji na mauzo ya rejareja na ile ya heshima
Kampeni za Fursa na Kipepeo
Kampeni ya Fursa nayo imeanzishwa na Clouds Media chini ya Ruge ambayo ilikuwa na kaulimbiu ya Kamata Fursa Jitathmini, Jiamini, Jiongeze.
Fursa imekuwa ikilenga kutoa dira kwa makundi tofauti juu ya namna ya kujikwamua kupitia shughuli mbalimbali za kiuchumi kwa kupambana na changamoto.
Kwa upande wake kampeni ya Kipepeo imekuwa ikifanyika katika shule mbalimbali nchini ambapo enzi za uhai wake, Ruge aliwahi kusema wamezunguka kwenye zaidi ya mikoa 16 kuzungumza na watu mbalimbali.
Alitoa mfano wa hatua za ukuaji wa kipepeo kuwa umeakisi uhalisia wa maisha ya mtoto wa kike katika hatua mbalimbali za maisha na kwamba ukuaji wa kipepeo katika hatua za mwanzo siyo wa kuvutia.
Alisema watoto wengi wa kike hatua wanazopitia wanashindwa katika hatua za mwanzo na kushindwa kufikia malengo yao kwa kukata tamaa, hivyo kampeni hiyo inakwenda kuwa na mtazamo mpya juu ya maisha yao.
Tunakufungulia Dunia
Tunakufungulia Dunia pia ni kampeni ambayo imekuwa ikisisimua ikiwa na kishangilio cha “Inakusubiri dunia” ambayo ilikuwa ikizungumzwa na wadau mbalimbali wakimuombea Ruge.
Ruge ndiye aliyeasisi kaulimbiu hiyo ambayo inatumiwa na Clouds Media Group.
Katika kaulimbiu hiyo, Ruge alikuwa akiwahamasisha watu hasa vijana kufuata ndoto zao kwa kufanya mambo wanayoyapenda ili kujikwamua kutoka kwenye umaskini.