Burudani

Habari

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

VIDEO: Queen Elizabeth alivyolikwaa taji la Miss Tanzania

Video Archive
Tue, 11 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hatimaye safari ya kumsaka mrembo wa Tanzania atakayeiwakilisha nchi katika mashindano ya dunia imekamilika usiku wa Septemba 8, mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).

Queen Elizabeth Makune ndiye mlimbwende atakayeibeba bendera ya Tanzania katika fainali za Miss World, zitakazofanyika Desemba 8, mwaka huu katika Jiji la Sanya, China.

Katika fainali hizo zilizoanza saa 3.15 usiku na kumalizika saa 7.35 usiku, zilianza kwa warembo kupita kwa mavazi matatu tofauti jukwaani, ikiwemo la ubunifu, ufukweni na la kutokea usiku.

Baada ya raundi za mavazi yote kupita, walitajwa washiriki 10 bora na kisha tano bora ambapo mwisho majaji walimuona mlimbwende Queen Elizabeth ndiye aliyestahili kulitwaa taji hilo ambapo aliondoka na gari lenye thamani ya Sh15 milioni na taji lenye thamani ya Sh40 milioni .

Queen Elizabeth alipanda jukwaani hapo akichuana na warembo 20 kutoka Kanda ya Kati, Ziwa, Nyanda za Juu, Kaskazini huku akiiwakilisha Kanda ya Dar es Salaam.

Ni mzoefu katika urembo

Hata hivyo, mrembo huyo safari yake haikuanzia katika mashindano ya Miss Tanzania, bali katika mashindano ya Miss University Africa mwaka jana, ambapo kidunia alishika nafasi ya tatu.

Hakuishia hapo kwani wakati wa kuanza kutafuta warembo wataoshiriki Miss Tanzania, alishiriki katika shindano la Miss Vyuo na alianzia pale Chuo cha Uhasibu (TIA), kilichopo Temeke jijini Dar es Salaam na kutwaa taji hilo.

Kama haitoshi, walipokuja kutafutwa wawakilishi watakaowakilisha mrembo kutoka vyuo vikuu, alitwaa taji hilo kwa mara nyingine, hivyo kumpa nafasi ya kushiriki Miss Kinondoni.

Kama kawaida yake, katika hili Queen hakufanya ajizi kwani alichukua taji hilo na kuwa na sifa ya kuingia moja kwa moja kwenye shindano la Miss Tanzania ambapo usiku huo wa Septemba 8, alitawazwa rasmi kuwa Miss Tanzania, nafasi atakayoitumikia kwa mwaka mmoja kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.

Gari lazua vita ya maneno

Ilizuka vita ya maneno mitandaoni kuhusiana na zawadi ya gari kwa madai halina hadhi.

Vita hiyo ilianza juzi usiku baada ya gari la mshindi kuonyeshwa na baadhi ya watu kuanza kutoa maoni wakililinganisha na lile alilopewa mshindi wa Kanda ya Ziwa.

Muandaaji wa mashindano ya Kanda ya Ziwa, maarufu Jembe ni Jembe alihoji ubora wa gari hilo aina ya Terrios Kid na lile walilolitoa wao aina ya Passo ambalo lilizua sintofahamu takribani miezi miwili iliyopita.

Jembe ni Jembe aliingia katika misukosuko wakati wa kundaa mashindano ya mrembo wa Kanda ya Ziwa baada ya waratibu wa Miss Tanzania kudai gari hilo halina hadhi ya mashindano hayo.

Mbali na Jembe ni Jembe, msanii maarufu wa maigizo nchini, Jacline Wolper aliinunua vita hiyo, akiandika katika mtandao wa Instagram kuwa ni bora kupewa zawadi ya iPhone X kuliko gari hilo.

“Jamani mimi sina tatizo na huyu dada aliyeandaa Miss Tanzania, ila tatizo ni kwamba aliwaandama sana waandaaji wa Miss Mwanza juu ya zawadi mpaka wakapelekwa kwenye uongozi wa Serikali na kuandika barua mpaka mashindano kutaka kusitishwa,”ameandika Wolper.

Akijibu mashambulizi hayo dhidi yake, mwendeshaji wa mashindano hayo Basila Mwanukuzi, alisema yote hayo yanasemwa kutokana na hasira za yeye kukataa gari bovu kwa ajili ya shindano la Kanda ya Ziwa jambo linalowafanya watu kuwa maadui na kupinga chochote.

“Nyie hamtafanikiwa, ‘mnaedit’ picha na kusambaza, watu wamekuja wameona live (mbashara) na kusambaza. Wameona live na wataendelea kuona live. “Na kwa taarifa kumbe waliyataka mashindano ya Miss Tanzania lakini hawakufanikiwa, sasa kuharibu ndio furaha yao ‘Move on’. Kila kitu ni mipango ya Mungu,”alijibu Basila kupitia mitandao ya Facebook na Instagram.

Jinsi shindano lilivyokuwa

Baada ya watu kuingia na kutulia kwenye viti, shindano hilo lilifunguliwa na washereheshaji Hamisa Mobeto na mtangazaji wa kituo cha runinga cha EATV, Deogratius Kithama.

Baada ya hapo warembo walipita kwa mara ya kwanza kujitambulisha jukwaani kwa kucheza wakiwa wamevaa sketi fupi za rangi ya kijani na blauzi zenye ufito wa rangi ya bendera ya Taifa.

Baada ya burudani wakapita tena na vazi la ufukweni ambalo lilikuwa ni sketi za kanga na blauzi zikiwa zimeshonwa kwa mitindo mbalimbali.

Baadaye walipita na vazi la ubunifu, kisha vazi la usiku na ndipo hapo 10 bora ilipotangazwa na kutoa muda kwa majaji kwenda kuchagua tano bora na kuwaacha wahudhuriaji wakiburudishwa na msanii Ruby na Barnaba.

Hata hivyo, kulionekana ugumu katika kuwachagua warembo hao, ambapo majaji waliwataka warudi tena jukwaani ili kuwaangalia kwa mara ya pili na kisha kwenda kujifungia chumba maalum kwa ajili ya kuchagua tano bora.

Serikali yatoa ahadi

Katika shindano hilo baadhi ya viongozi kutoka serikalini walihudhuria akiwemo Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Jokate Mwegelo na Katibu wa Baraza la Sanaa la Taifa, Godfrey Mngereza.

Akizungumza katika hotuba yake, Waziri Mwakyembe alisema amefurahi kufanikiwa kwa mashindano hayo chini ya kampuni ya The Look inayosimamiwa na Basila Mwanukuzi ambaye aliwahi kuwa Miss Tanzania mwaka 1998.

Alisema baada ya kutokea sintofahamu ya mashindano hayo na serikali kuamua kuyasitisha, walihakikisha atakayeyaendesha anakuwa na weledi wa hali ya juu na hilo wameliona tayari kwa Basila ndio maana walimruhusu kuyaendesha tena kwa mwaka huu.

Akizungumzia kuhusu warembo walioshiriki, alisema sehemu kubwa ya warembo hao watachukuliwa wakafanye kazi kwenye Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), kwa kuwapatia mafunzo mafupi.

“Kama mnavyojua tuna ndege kubwa ya Dream Liner ambayo imejizolea umaarufu inahitaji warembo wa kutoa huduma na kama serikali tumeona tuanze kuwachukua warembo katika shindano hili,” alisema Dk. Mwakyembe.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo, aliwataka warembo hao wanapokwenda kwenye shindano la Miss World wasisite kuzungumza kiswahili kwa kuwa ni kati ya lugha 6,000 zinazoongelewa na watu duniani, Kiswahili ni kati ya lugha 10 zinazozungumzwa duniani.

Vilevile, hakusahau kuwashukuru waanzilishi wa mashindano hayo, kampuni ya Lino chini ya Mkurugenzi wake Hashim Lundenga.

Basata wapongeza zawadi

Wakati baadhi ya wadau wakiiponda zawadi ya gari aliyopewa Miss Tanzania, Katibu wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza, alisema suala la zawadi katika mshindi wa mwaka huu hawana wasiwasi nalo na limefuata taratibu zote.

Mastaa wengi hawakutokea

Usiku huo, pia ulihudhuriwa na watu maarufu akiwemo Miss Tanzania mwaka 2004, Faraja Kota na Miss Tanzania 2016 Diana Edward.

Japokuwa watu maarufu wengi ambao walitarajiwa kuwepo hawakutokea akiwemo Wema Sepetu ambaye amewahi kuwa Miss Tanzania mwaka 2006, pamoja na wasanii mbalimbali hususani wa filamu ambao pia ni wadau wa masuala ya urembo.

Kutokana na hilo, walijikuta wakimpa nafasi kubwa mwanamitindo Faiza Ally kuwa mmoja wa mastaa aliyehojiwa ambapo alizungumza mambo mbalimbali ikiwemo maneno ambayo amekuwa akiyaandika kwenye mitandao dhidi ya mchumba wa mzazi mwenzie Joseph Mbilinyi (Sugu).

Faiza alifunguka kuwa hayupo tayari kumpenda mtu ambaye ana uhusiano na Sugu kwa kuwa bado anampenda Mbunge huyo wa Mbeya Mjini, na ndio maana hata anapomuona akiwa na mtoto wake na kupiga picha anachukia.

Chanzo: mwananchi.co.tz