Dar es Salaam. Msanii wa muziki nchini Tanzania, Diamond Platnumz amesema kama wanawake watawakomalia wanaume kutokutumia kondomu ni wazi maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) yatapungua.
Diamond ameyasema hayo leo Jumatano Julai 10, 2019 kwenye mkutano wa wasanii wa ya lebo ya Wasafi na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS).
Msanii huyo alijikuta akisema hivyo baada ya kuulizwa kuhusu uaminifu wake na kazi ya kutoa elimu wanaoenda kuifanya kupitia Tamasha la Wasafi litakaloanza Julai 19,2019.
"Mimi naamini wanawake kama watatukomalia kutowaingilia bila kondomu ni wazi kwamba wanaume hatutaweza kulazimisha na hapo ndipo tutadhibiti maambukizi ya VVU," amesema msanii huyo.
Kuhusu TACAIDS kushirikiana nao katika tamasha la wasafi, Diamond amesema wamekuja wakati mzuri kwani tamasha hilo lengo lake si kutoa tu burudani bali na elimu kwa vijana kuhusu maisha yao.
Kwa upande wake, Jumanne Issango ambaye ni Kaimu mkurugenzi wa TACAIDS, amesema mkakati wa nne wa kudhibiti Ukimwi vijana ndio wamepewa kipaumbele.
Pia Soma
- Majaliwa ateta na Rais wa Misri Ikulu
- KESI YA KITILYA: Mkulo aomba wakili Magafu asimuulize maswali mengi
- Malecela awataka vijana wa CCM kukilinda chama hicho
"Hivyo mikakati yetu ni kuona elimu inaenda zaidi kwa vijana kwani hawa ndio nguvu kazi ya Taifa," alisema Issango.
Kwa upande wake, Ofisa Sanaa wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Bonnah Masenga amesema TACAIDS, hawajakosea kwani wasanii ni watu wanaosikilizwa na kuangaliwa na watu ikiwemo kwenye kurasa zao kwenye mitandao ya kijamii.